Zaidi ya mifuko elfu sabini na nne ya mbolea ya ruzuku mkoani Songwe iliyotakiwa kuwafikia wakulima katika msimu huu wa kilimo imebainika kutoingizwa kwenye mfumo.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt. Francis Michael ametoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari wakati akitolea taarifa mwenendo wa ufuatiliaji wa mbolea hizo mkoani hapo.
Dkt. Francis amesema kikosi hicho kimebaini mfumo wa mbolea kuchezewa na watu wasio na nia njema na Serikali hasa katika kuwaletea maendeleo wakulima.
Pia amesema yapo makampuni ya mawasiliano ambayo yaliingia mkataba na serikali kwaajili ya kuwasajili wakulima nayo yamehusika katika ubadhirifu huo ambao yeye ameuita ni uwizi.
Amesema makampuni hayo yalisajili wakulima hewa ili kuidanganya serikali na kwamba tayari wafanyakazi wa kampuni hiyo ya mawasiliano pamoja na watu wengine wameshachukuliwa hatua huku uchunguzi zaidi uliendelea.