NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Jim Yonazi amepongeza juhudi za Kampuni ya Mawasiliano ya Huawei za kuboresha ubora wa elimu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ili kuongeza ujuzi wa kuajiriwa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini.
Dk Yonazi alitoa pongezi hizo wakati wa sherehe za ufunguzi wa msimu wa tano wa programu ya "Seeds for the Future" ambao ulifanyika mtandaoni mapema wiki hii.
Kwa mara ya kwanza hapa nchini, programu ya "Seeds for the Future" ilizinduliwa mnamo mwaka 2016 kwa msaada wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Programu hiyo ilihusisha vyuo vikuu vinne wakati ikizinduliwa na sasa inajumuisha vyuo vikuu saba ambavyo ni Chuo Kikuu ya Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST), Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (SAUT ) na Chuo Kikuu cha Elimu cha Dar es Salaam (DUCE).
"Nimearifiwa kuwa katika kuchangia ukuzaji wa vipaji vya TEHAMA nchini Tanzania na kuendana na mipango ya kimkakati ya nchi, Huawei imeongeza kwa kiasi kikubwa shughuli na ushirikiano na vyuo vikuu na nchini. Hizi ni juhudi za kupongezwa kwa kuwawezesha vijana wa kitanzania,” alisema Dk Yonazi wakati akitoa hotuba yake kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Zainab Chaula.
Pia, aliwataka wanafunzi kutumia maarifa wanayopata kwenye programu hiyo kufundisha wengine ili kufaidisha idadi kubwa ya watu hasa wale ambao hawakuwa na bahati kama wao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Huawei Tanzania, Frank Zhou aliangazia mipango ya Huawei ya kuiwezesha Tanzania kukabiliana na mahitaji ya teknolojia kidijiti ambayo yanabadilika mara kwa mara.
Mwaka huu, ili kufikia vijana wengi zaidi nchini Tanzania, Programu ya “Seeds for the Future” itafanyika mtandaoni ili iweze kuchukua idadi kubwa ya wanafunzi kutoka mikoa tofauti na ili wanafunzi wenye mahitaji maalumu pia washiriki.
Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia wa Airtel, Prosper Mafole aliwahimiza wanafunzi kutumia fursa za kujifunza zinazotolewa na Huawei na akawakaribisha kwa msaada wowote endapo watahitaji.
Yuan Lin, Mshauri wa Uchumi na Biashara wa Ubalozi wa China nchini Tanzania, aliipongeza kampuni ya Huawei kwa kuonesha mfano mzuri katika kukuza vipaji vya Tehama nchini Tanzania kwa kuwajengea uwezo vijana wa shahada ya kwanza ambao watakuwa na msukumo wa mabadiliko ya Tehama nchini Tanzania katika siku za usoni.