Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hoteli sasa kupangwa kidijitali

Dad97fa08ae2ca97cff400e56fb7599c.png Hoteli sasa kupangwa kidijitali

Fri, 18 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WIZARA ya Maliasili na Utalii imezindua mfumo wa kielektroniki, utakaotumika kupanga madaraja ya huduma za malazi na chakula kwa viwango vya ubora wa nyota, jambo litakalopunguza gharama, muda na kuongeza wigo wa huduma hizo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Aloyce Nzuki alisema ikiwa ni tofauti na mfumo wa sasa wa kukagua na kupanga madaraja ya huduma, mfumo wa kidigitali unatarajia kuleta mageuzi makubwa katika sekta hiyo.

Alisema mfumo huo utasaidia kupunguza gharama na muda, lakini pia utawasaidia watathimini wa upangaji wa huduma za malazi na chakula kuepukana na vishawishi vya rushwa na kuepukana na malalamiko ya kuwapo upendeleo.

Alisema mfumo huo pia utawasaidia wasanifu majengo, wanaopewa kazi ya kuchora michoro ya majengo kuzingatia vigezo hivyo ili kuwaondola adha ya kushindwa kupata viwango kutokana na mkosa ya ujenzi.

“ Kupitia mfumo huu wasanifu majengo waweze kuwahudumia vizuri wateja wao, kwa sababu kuna mambo yanaweza kumnyima mdau hoteli yake kushindwa kupata nyota kwa sababu ilikosewa tangu mwanzo kwenye uchoraji na kujenga, kama ukubwa wa vyumba unatakiwa mita za mraba 13 na wewe umejenga mita za mraba 10, hakuna namna ya kupata nyota hata kama jengo hilo ni zuri kiasi gani,” alisema.

Alisema pia wadau wa huduma za malazi na chakula,wanaweza kutumia mfumo huo kujifanyia tathimini na kufanya maboresho endapo wanataka kupanda madaraja.

Alisema mpaka sasa wizara imekagua na kupanga huduma za malazi na chakula. Kazi hiyo imefanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Manyara, Arusha na Dodoma. Huduma zilizopangwa katika viwango vya nyota zimeongezeka kutoka 67 mwaka 2015 hadi kufikia 308 mwaka huu.

“Kasi hii ni ndogo na maeneo mengi hayajawekwa kwenye nafasi za ubora, jambo lililochangiwa na mfumo ambao umekuwa ukitumika na ambao ulikuwa na changamoto,” alisema.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Philip Chitaunga alisema mfumo huo utarahisisha utaratibu wa kupanga madaraja

Alisema baadaye utaanza hatua ya pili ya kufanya tathimini kwa kujibu maswali 24 kwa hatua ya kwanza na kutakiwa kupata alama asilimia 75.

“Ukishapata alama zisizopungua 75, unaingia hatua ya pili ya kufanya tathimini ya kupangiwa daraja kwa kujibu maswali kati ya 2,500 hadi 2,700 na hapa mdau ataweza kumtumia mtaalamu na endapo taarifa zitakidhi vigezo ndipo wataalamu kutoka wizarani watakuja kufanya uhakiki,” alifafanua.

Balozi wa Rwanda hapa nchini, Meja Jenerali, Charles Karamba alisema Tanzania imekuwa na uzoefu katika sekta ya utalii, jambo ambalo linafanya nchi jirani kujifunza kupitia Tanzania.

Alisema kwa kutumia mfumo wa kidigitali, utasaidia kuleta ushindani na kuondoa vishawishi vya rushwa kwa wataalamu wanaofanya kazi ya kutathimini vigezo vya kutoa madaraja.

Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Vyama vya Utalii Tanzania (TCT), Richard Rugimbana aliishukuru wizara kwa hatua hiyo na kuwa ni imani yake mfumo huo utakuwa rafiki.

Chanzo: habarileo.co.tz