Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hofu, furaha king’amuzi kimoja

95071 Kingamuzi+pic Hofu, furaha king’amuzi kimoja

Mon, 10 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mikoani. Mpango wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA kuanzisha king’amuzi kimoja, maarufu kwa jina la super decorder, kupata matangazo ya vituo vyote vya televisheni, umepokewa kwa furaha na hofu kwa baadhi ya wateja.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Mbeya, Morogoro, Tanga, Mwanza, Mara na Dodoma unaonyesha baadhi ya wateja hawaelewi utakavyofanya kazi.

TCRA inataka kuanzisha king’amuzi hicho ambacho kitaweza kung’amua matangazo ya kituo chochote cha televisheni ambacho mteja anataka kwa kutumia kadi tu badala ya kujaza ving’amuzi tofauti nyumbani.

Wakizungumza na gazeti hili jana, baadhi ya mafundi wanaofunga madishi na ving’amuzi, wamepongeza hatua hiyo, wakisema itawawezesha kuona chaneli za bure pasipo vikwazo.

Lakini fundi wa kufunga ving’amuzi hivyo mjini Handeni, Abdallah Khan alisema changamoto itajitokeza katika satellite kwani kila kimoja kina mwelekeo wake.

Naye Joseph Kimario au Carlos, ambaye ni mtaalamu wa ving’amuzi mjini Moshi, alisema mpango huo ni mzuri kwa kuwa utawezesha kila mtu kuona chaneli za bure.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
“Unajua kinachopiganiwa hapa ni kila Mtanzania aone zile chaneli za FTA (za bure) ambazo kwa mfano kwenye DSTv nyingi hazipo. Sasa unalazimika kuwa na ving’amuzi vingine,” alisema.

Mkazi wa Mianzini jijini Arusha, Geofrey Steven alisema ni jambo zuri kuwa na mfumo mmoja wa kupata ving’amuzi vyote, lakini ni muhimu kukubaliwa na wenye ving’amuzi.

“Ni mpango mzuri unapunguza gharama kwa watumiaji kwa sababu kama mimi nina ving’amuzi vya Star Times, Dstv na Azam sasa vikiuunganishwa ni vizuri na itapunguza gharama,” alisema.

Steven, hata hivyo, alisema TCRA inapaswa kutoa fidia kwa sababu tayari imewaingiza Watanzania katika gharama za kununua ving’amuzi vingi bila sababu kama ilkivyokuwa wakati nchi ilipoingia katika mfumo wa digitali.

Mkazi mwingine kutoka Kiranyi, Janet Mollel alisema hofu kubwa kwa mpango huo wa TCRA ni kukosa matangazo ya kimataifa ya michezo na tamthilia pale king’amuzi kinapokuwa kimoja.

Mkazi wa Igoma, Mwanza, Isaya Matovu alisema mpango wa kuwa na king’amuzi kimoja si tu kwamba utapunguza gharama, lakini pia utaondoa usumbufu wa kubadili ving’amuzi.

Mkazi wa Bwilu jijini Mwanza, Nelia Kalokola alisema mbali na kupunguza gharama na usumbufu, utapunguza mrundikano wa dishi sehemu moja.

Mkazi wa Musoma, Nyamete Isaya alisema mpango huo utawasaidia ambao hawajui wachague king’amuzi gani kutokana na mkanganyiko wa upatikanaji wa chaneli za bure.

Sospeter Mabirika mkazi wa Serengeti alitaka mpango huo uje na uboreshaji wa matangazo ya baadhi ya vituo vya televisheni kwa kuwa hata malalamiko yanapotolewa hayafanyiwi kazi.

Mkazi wa Sai Jijini Mbeya, Charles Mwakipesile alisema uamuzi wa TCRA kuwa na kisimbusi kimoja ni mzuri na utawaondolea usumbufu wateja kwa kuwa hapo alipo ana ving’amuzi vinne.

“Sasa huu uamuzi wa TCRA ni mzuri badala ya kumiliki madishi mengi nje, unakuwa na kadi tu na king’amuzi kimoja,” alisema Mwakipesile.

Noel Ernest mkazi wa Kihonda mkoani Morogoro alisema pamoja na TCRA kuleta mpango huo, lakini ilipaswa kuwashirikisha wananchi kupata maoni yao kwa kuwa waliwaingizia hasara.

“Niulize tu Sasa hivi ving’amuzi tulivyonavyo vitakuwaje jamani?,maana wengine tumenunua kwa kudunduliza, tunasikia vinaletwa vingine hii hata sijui kama tutaweza kununua,”alisema.

Hata hivyo, Mohammed Ibrahim wa Kange Jijini Tanga alisema mpango huo unalenga kuwaletea usumbufu wananchi kuhangaika kama ilivyokuwa kwenye vitambulisho vya Taifa.

Chanzo: mwananchi.co.tz