Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hizi ndizo sababu za wakazi wa Dar kuongoza kwa kukopa

Pesa Maua Hizi ndizo sababu za wakazi wa Dar kuongoza kwa kukopa

Thu, 28 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Uwepo wa shughuli nyingi za kibiashara, mzunguko mkubwa wa fedha na idadi kubwa ya watu zimetajwa kuwa sababu za Jiji la Dar es Salaam kuongoza katika uchukuaji wa mikopo.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ya mwenendo wa Uchumi wa Kanda iliyotolewa Oktoba 5, 2023, Dar es Salaam ilibeba asilimia 56.7 ya mikopo yote iliyotolewa na benki katika mwaka wa fedha 2022/23.

Kati ya Sh25.79 trilioni zilizotolewa kwa mikopo mwaka huo, Sh14.61 trilioni zilichukuliwa na watu wa Dar es Salaam, huku Kanda ya Ziwa ikifuata kwa kubeba asilimia 13 ya mikopo hiyo.

Kanda ya Kati ilikuwa na asilimia 11, Kanda ya Kaskazini (asilimia 10), Kanda ya Kusini Mashariki (asilimia 4.8) na Nyanda za Juu Kusini (asilimia 3.8).

Licha ya shughuli za kibiashara kuwa kichocheo kikubwa, lakini wachumi wanashauri kuwa ni vyema fursa hizo zikawafikia watu wa kanda zote ili kufanya uchumi wa nchi kutotegemea eneo moja.

“Dar es Salaam inachukua asilimia kubwa ya mikopo, ikifuatiwa na kanda nyingine kama Mbeya na Mwanza, hii ni kwa sababu maeneo haya yana shughuli za kiuchumi za kibiashara, watu wanaweza kuwa wanalima na kufuga lakini hawapo kibiashara,” alisema Oscar Mkude, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchumi na biashara.

Alisema mikopo mingi inayotolewa na benki inapelekwa katika sekta ya kibiashara kwa sababu watu wanakuwa na uhakika wa kurudisha kile walichochukua, tofauti na ufugaji na kilimo kwa sababu hazipo kibiashara.

Akifafanua athari za mikopo mingi kutolewa Dar es Salaam, Mkude alisema inasababisha mkoa huo kuwa tegemeo pekee kwa nchi tofauti na ikipelekwa katika maeneno mengine.

Alisema hali hiyo pia, itasababisha Dar es Salaam kuendelea kukua kiuchumi kuliko maeneo mengine, jambo litakalowachochea watu wengi wa mikoani kuhamia jijini humo na kulifanya lizidiwe.

Idadi kubwa ya watu inapoongezeka inafanya shughuli kubwa ya upanuzi wa miundombinu kufanyika ili kukabiliana na ongezeko hilo.

“Athari ya hili, Dar es Salaam ikiyumba kidogo nchi inaweza kupoteza uchumi kwa takribani asilimia 50 na itasababisha mkwamo wa juu sana na Taifa litaathirika,” alisema Mkude.

Alitolea mfano wa mtoto aliyefanikiwa katika familia ya watoto kumi jinsi anavyokuwa na kazi ya ziada ya kuhakikisha anawainua wenzake kiuchumi, jambo ambalo litafanya ukuaji wa familia kuwa kwa kiwango kidogo na ikitokea amepoteza maisha basi familia hupoteza mwelekeo.

“Uchumi mzuri ni ule uliotawanyika katika kanda mbalimbali, hii inaweza kufanya kila kanda kuleta mchango wake katika pato la Taifa na hii inaweza kusisimua utoaji wa mikopo katika maeneo hayo,” anasema Mkude.

Pia, alisema ikiwa nchi itaweza kusambaza uchumi katika kanda zote, hata kiwango cha ukuaji wake kitakuwa kikubwa tofauti na sasa, Dar es Salaam ndiyo inayokua kwa kasi.

Katika michango ya kikanda katika pato la Taifa (GDP), ripoti hiyo inaeleza kuwa Dar es Salaam ndio mkoa unaoongoza kwa kuchangia kiasi kikubwa cha Sh27.48 trilioni.

Fedha hizo ni kati ya Sh161.52 trilioni zilizochangiwa katika GDP mwaka 2021.

Jiji hilo pia ni kati ya mikoa 10 iliyotoa asilimia 62 ya GDP katika mwaka 2021, huku mikoa 15 iliyosalia ikipambana kujazia asilimia zilizobakia.

Akiendelea kufafanua utoaji wa mikopo kuwa mkubwa Dar es Salaam, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora anasema uelewa mpana juu ya mikopo inayotolewa ndiyo sababu ya Dar es Salaam kuongoza katika uchukuaji wa mikopo.

“Pia, idadi ya watu ni kubwa, sio watu tu, bali wanaojishughulisha na wenye matamanio ya kuongeza mitaji yao ya biashara... wanaona kuchukua mikopo ni moja ya njia inayoweza kuwasaidia,” anasema Profesa Kamuzora.

Hata hivyo, Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 inaonyesha kuwa, Dar es Salaam inaongoza kwa kuwa na wakazi wengi waliofikia milioni 5.3, ikifuatiwa na Mwanza yenye watu milioni 3.6, Morogoro milioni 3.1 na Dodoma milioni 3.08.

Alisema kusambazwa kwa uelewa juu ya umuhimu wa mikopo katika kanda tofauti ni moja ya njia zinazoweza kufanya ukuaji wa uchumi kuwa wa kasi, tofauti na watu kutochukua mikopo hiyo.

“Hela ikikaa tu benki bila kukopwa uchumi hauwezi kukua, ila wakichukua na kuzalisha na kurudisha mikopo waliyochukua uchumi utakua,” anasema Profesa Kamuzora.

Sekta zilizoongoza kwa mikopo

Ripoti hiyo ya BoT inaeleza kuwa, hadi Juni 2023, mikopo binafsi ilikuwa inaongoza kwa asilimia 43.3, ikifuatiwa na ya biashara za jumla na rejareja ambayo ni asilimia 11.2.

Kilimo kilishika namba tatu kwa asilimia 9.7, viwanda (asilimia 6.8), mikopo ya nyumba (asilimia 4.7), ujenzi (asilimia 3.8), huduma za afya na elimu, migawaha na hoteli, usafirishaji, uhifadhi na mawasiliano (asilimia 3.6), madini (asilimia 2.9), umeme, gesi na maji asilimia 2.5.

Pengo kubwa lililopo kati ya mikopo binafsi na mikopo mingine inatajwa na baadhi ya wadau kuwa ni masharti magumu yaliyowekwa katika ufikiaji wake.

Kilimo ni moja ya sehemu iliyoajiri idadi kubwa ya Watanzania, lakini baadhi ya watu walishindwa kufikia mikopo hiyo.

Obson Obadia ni mmoja wa wakulima aliyejaribu mara mbili kutafuta mkopo lakini masharti yaliyokuwa yamewekwa yalimfanya kukata tamaa.

“Nilijaribu mara mbili kukawa na masharti, likiwamo lile la vikundi, baadaye liliondolewa na mtu mmoja mmoja kuweza kukopa, lakini tayari nikawa nimekata tamaa, sasa nalima kupitia mikopo ya vikundi vya kifamilia,” anasema Obadia.

Licha ya kurahisishwa kwa masharti, Novemba 7 mwaka huu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, Afia Sigge ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), alisema utoaji wa mikopo umeongezeka kwa asilimia 36 na kufikia Sh358.56 bilioni ambayo imenufaisha wakulima zaidi ya milioni 1.6.

“Pia, TADB inashirikiana na taasisi 16 za kibenki kupitia mfuko wake wa udhamini wa wakulima wadogo na imefanikiwa kuwafikia wakulima katika mikoa 27 na jumla ya Sh228.26 bilioni zimetolewa,” anasema Sigge.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live