Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hizi ndizo sabaabu kupanda bei za vyakula

Bei Za Bidhaa 4.crdownload Bei za vyakula zang’ata tena

Fri, 15 Jul 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Dar/mikoani. Wananchi katika maeneo mbalimbali nchini wameendelea kuonja maumivu ya kupanda kwa bei ya nafaka -- mahindi, mchele na ngano, mazao ambayo yanagusa maisha yao ya kila siku.

Hali hiyo inatokea ikiwa ni miezi minne tangu kupanda bei ya bidhaa mbalimbali, zikiwemo za vyakula katika mikoa zaidi ya kumi, hatua iliyoongeza gharama za maisha.

Baada ya habari hizo kuchapishwa, Serikali kupitia Tume ya Ushindani nchini (FCC) na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ilianza kutafuta ufumbuzi, lakini hakukuwa na mabadiliko chanya na zimeendelea kupanda.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika mikoa takriban 10 nchini, umebaini kuwepo ongezeko la bei katika nafaka hizo muhimu kwa kati ya Sh200 hadi Sh400 kwa kilo.

Mikoa ambayo imeangaliwa sasa ni Mbeya, Dodoma, Manyara, Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mara, Kigoma, Simiyu na Morogoro.

Hata hivyo kuanzia wiki iliyopita mafuta ya kula ambayo yalikuwa yamepanda kupindukia yalianza kuonyesha dalili za kushuka katika baadhi ya maeneo.

Alipotakiwa kuzungumzia hali hiyo, Dk Ashatu Kijaji, waziri mwenye dhamana ya biashara alisema “subirini Julai 15, mwaka huu nitatoa tamko la Serikali kuhusu hilo.”

Uzalishaji mdogo

“Kuna upungufu wa uzalishaji msimu wa 2021/22, akiba ya msimu 2020/21 iliisha, sasa mahitaji yameongezeka sokoni kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, mvua zilikata zikaathiri mazao kukomaa,” alisema Geofrey Rwiza, kaimu wa Baraza la zao la Mchele Tanzania.

Hali hiyo, anaeleza Profesa Samuel Wangwe, mchumi mwandamizi nchini, kuwa inaweza kusababisha mfuko wa bei katika huduma mbalimbali nchini.

Alipoelezwa kwamba lakini mkulima anafurahia kuuza kwa bei nzuri, alisema “sawa, mlaji analia lakini mkulima anachekelea kwa sasa, hiyo ni fursa kwa wakulima kuongeza uzalishaji,” alisema.

Angalizo la Profesa Wangwe linaakisi taarifa za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zilizotolewa Julai 11 mwaka huu zikionyesha mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Juni, kuongezeka hadi asilimia 4.4 kutoka asilimia 4.0 kwa mwaka ulioishia Mei, 2022.

Hali ilivyo

Mkoani Morogoro bei ya kilo moja ya unga wa sembe imepanda kutoka Sh1,400 hadi Sh1,800, mchele kutoka wastani wa Sh2,000 hadi 2,500, maharage kutoka Sh2,400 hadi Sh2600, dagaa kutoka Sh5,500 hadi Sh8,000, sukari kutoka Sh2,600 hadi Sh2,800 na mafuta ya kupikia kutoka Sh6,000 hadi Sh6,800 kwa lita.

Akizungumza na Mwananchi, mfanyabiashara wa mjini Mbeya, Salomon Abel alisema kipindi kama hiki mwaka jana mahindi yaliuzwa kati ya Sh7,000 mpaka 7,500 kwa plastiki la kilo 20, mwaka huu yamepanda mpaka Sh14,000.

Baadhi ya wafanyabiashara wamedai miongoni mwa sababu za kupanda bei ni pamoja na kupanda bei ya petroli na dizeli.

Jijini Dodoma, Msinta Mayaoyao, mfanyabiashara katika Soko Kuu la Majengo, alisema kilo ya mahindi inauzwa kati ya Sh850 hadi 870 kutoka Sh500 na Sh580 za awali, huku mwenzake, Athuman Omary akisema kuna ongezeko la wafanyabiashara kutoka Kenya na Uganda ambao hununua mahindi katika vijiji vilivyokuwa na mavuno kidogo mwaka huu na kusababisha ongezeko la bei.

Hali iko vilevile jijini Mwanza ambako Mwenyekiti wa Soko Kuu la Mbugani, Ahmed Nchola alisema mchele wa kawaida umepanda kutoka Sh1,400 hadi Sh1,800 kwa kilo, sembe kutoka Sh1,000 hadi Sh1,200, dona kutoka Sh800 hadi Sh1,000, sababu zikiwa zilezile za kupungua mavuno na kupanuka masoko nchi za jirani.

“Ili kudhibiti mfumuko wa bei ya chakula nchini, Serikali izuie uuzaji wa chakula nje ya nchi,” alisema Nchola.

Katika Wilaya ya Sengerema gunia la mpunga lilipanda kutoka Sh70,000 hadi Sh100,000 wakati lile la mahindi likipaa kutoka Sh50,000 hadi Sh120,000.

Katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Mara, kilo ya mchele imepanda kutoka Sh1,800 hadi Sh2,000 na ile ya ngano kutoka Sh1,900 hadi Sh2,200.

Hali ni ileile mkoani Tabora, ambako bei ya kilo 20 za mahindi zimeongezeka kutoka Sh15,000 hadi Sh17,000, huku mfanyabiashara katika soko la nafaka mkoani humo, Leonard Daud akieleza wasiwasi kuwa bei hiyo huenda ikaongezeka kutokana na mavuno kusuasua mwaka huu.

Kila kitu kimepanda

Mfanyabiashara wa nafaka mjini Musoma, Anna Joctan alisema “sasa hivi karibia kila kitu kimepanda bei, huko tunakochukulia pia bei imepanda lakini pia gharama za usafiri zipo juu, kwa hiyo ili kupata faida tunalazimika kuongeza bei kwenye kila kilo ya nafaka kulingana na bei ya kununulia.”

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Butiama, Revocatus Lutunda alisema bei ya debe moja la mahindi wilayani humo imepanda kutoka makadirio ya kati ya Sh8,000 hadi 10,000 hadi kufikia makadirio ya Sh17,000 hadi 18,000.

“Tunaomba viongozi wa dini kusaidia kuwahimiza waumini juu ya utunzaji wa chakula wakati Serikali tukitafuta mwarobaini wake,” alisema Lutunda.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi aliagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi kufanya tathmini ya bei za bidhaa muhimu ili kupima iwapo bei za bidhaa hizo zinaendana na uhalisia.

Katika masoko jijini Arusha, nako mahindi yamepanda kutoka kati ya Sh800 na Sh900 kwa kilo hadi kati ya Sh1,200 hadi 1,300 wakati unga wa mahindi umepaa kutoka Sh1,300 hadi 1,500, huku unga wa ngano nao ukizidi kupaa kutoka Sh1,500 kufikia Sh2,200 kwa baadhi ya maeneo.

Mfanyabiashara wa Mbauda, Simon Lesinon alisema bidhaa zitazidi kupanda, hususan mahindi na maharage ya Soya ambayo imekuwa na wateja wengi wanaovuka mipaka kutokea nchini Kenya.

Mwokozi mbogamboga

Pengine eneo ambalo unafuu umeendelea kuonekana ni kwenye mazao ya mbongamboga hazijapanda wala kushuka, ingawa baadhi ya wafanyabiashara katika masoko makubwa ya Kariakoo, Buguruni, Kimara wamekuwa wakipunguza ujazo wa mboga hizo ili kuwalinda wateja wao.

Amina Julius, mamalishe wa Buguruni alisema ‘haikuwa rahisi kutambua lakini mwezi uliopita ndio nikashtuka wanapunguza ujazo wa fungu la mchicha au spinachi.”

Imeandikwa na Hawa Mathias (Mbeya), Habel Chidawali (Dodoma), Mgongo Kaitira (Mwanza), Bertha Ismail (Arusha), Daniel Makaka (Sengerema), Beldina Nyakeke (Mara), Hapinness Tesha (Kigoma) na Samira Yusuph (Simiyu), Hamida Shariff (Morogoro), Emmanuel Msabaha (Dar) na Joseph Lyimo (Manyara).

Chanzo: www.mwananchi.co.tz