Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), Ephraim Mafuru amesema ugonjwa wa Uviko-19 ni chanzo cha hasara za uendeshaji wa vituo vya mikutano vya kimataifa.
Mafuru amesema wametoka kujiendesha kwa hasara ya Sh500 milioni hadi kupata faida ya Sh1 bilioni huku wakilipa kodi ya Sh1.25 bilioni huku akiahidi kufanya kazi kwa bidii ili kurudisha heshima ya kiuchumi ya vituo hivyo.
Mafuru ameyasema hayo leo Alhamisi 13, 2023 jijini Dar es Salaam katika mkutano na wahariri kwa lengo la kuelezea malengo na mipango waliyoiweka katika kukuza uchumi kupitia vituo vya mikutano vya kimataifa vya AICC na JNICC.
"Mwaka 2022 tumeandaa mikutano 18 na mwaka huu tumeandaa mikutano 4 ya kimataifa ambayo ni Human Summit, AGRF, ICMDA na PCCB,” amesema.
Mafuru amesema kwamba kituo cha AICC na JNICC vilikuwa vinafanya vizuri kipindi cha nyuma hivyo atatumia uongozi wake vyema kurudisha vituo hivyo katika soko la mikutano.
"Tumeshapanga na wenzangu kuhakikisha tunafikia malengo tuliojiwekea na sitafumbia macho kwa mtu yeyote atakayekwenda kinyume na makubaliano yetu. Sitojali ameletwa na nani na anacheo gani," amesema Mafuru.
Amesema kituo cha mikutano cha AICC kitazindua idadi ya huduma mpya na za kipekee kwa lengo la kuvutia wateja mbalimbali kwenye kituo cha mikutano.
Katika kituo cha AICC kina uwezo wa kuhudumia watu 1,350 na kuna kumbi 17 ambazo zinaingiza idadi ya kubwa ya watu kuanzia 400 hadi watu 10 kwa ajili ya mikutano na mambo mengine.
Amesema kutakuwa na uwekezaji mkubwa kwenye vituo vya mikutano ili kukidhi mahitaji na mahitaji yanayobadilika kila mara, kwa kadiri huduma ya mkutano inavyohusika.
"Katika kituo chetu cha JNICC kina beba watu 1,003 hadi 1,213 na kuna vifaa vya kisasa ambavyo vinauwezo wa kutafsiri lugha tano tofauti," amesena Mafuru.
Mbali na hivyo pia amesema wanataka kutumia rasilimali zilizopo kwenye viwanja vya vituo hivyo ikiwepo nyumba za JNICC 624 za kupangisha 48 za kukodisha na ofisi kadhaa ambazo zinahitaji ukarabati.
Mafuru amesema pia wana hospitali inayohudumia watu zaidi ya 90,000 na hivyo wanahitaji kuweka mikakati ya kuendeleza uwekezaji huo kwanini kwa sasa hospitali hiyo ina vitanda 32 pekee.
Pia katika orodha yake ya mambo ya kufanya itakuwa ni kuwasiliana na wamiliki wa hoteli na waendeshaji watalii kwa lengo la kuimarisha matarajio ya utalii wa mikutano.
"Uzinduzi wa Royal Tour umefungua nchi kipindi cha nyuma tulikuwa tunajiendesha kwa hasara na tukawa kwenye nafasi ya 18 lakini kufunguliwa kwa nchi tumekuwa nafasi ya tano kwa kufanya mikutano mbalimbali," amesema.
Kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya tano huku nafasi nne za juu zikiwa zimeshikiriwa na nchi za Misri, Afrika ya Kusini na Rwanda.
Mafuru amesema tayari walishatuma timu kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa nini wanachofanya hao waliopo katika hizo nafasi ili na wao waweze kuzitumia kwa ajili ya kubadilisha mifumo ya uendeshaji wa vituo vyao.
Kutokana na uhitaji wa kumbi za mikutano amesema wameweka malengo ya kujenga vituo vingine viwili katika jiji la Dodoma na Zanzibar.
Amesema kwa kipindi hiki wameandaa mikutano michache na kufanikiwa kuingiza Sh18 bilioni kwa mwezi Juni.
Mwandishi wa Nipashe, Restuta James ameshauri kuweka mapambo yanayoendana na mkutano husika na itasaidia kutangaza tamaduni za nchi.
"Kulikuwa na mkutano unaohusiana na masuala ya chakula mapambo yake yalioambwa na mazao ya nchi ikiwepo Karafuu hii itazidi kuvutia," amesema Restuta.
Mhariri wa Gazeti la Jamhuri, Manyerere Jackton amesema wanatakiwa kutumia vyumba vilivyopo katika maeneo ya vituo vya mikutano kuwa sehemu za hoteli ili kuwasaidia watu kutohangaika kutafuta sehemu za kulala.
"Badala ya kuongea na hao watu wa hoteli mngetumia sehemu ya majengo ili wageni wasitumie muda mwingi katika kufika sehemu zao za kulala," amesema Manyerere.