Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hizi hapa sababu miswada ya rasilimali kukwama

Wabunge EALA Wahadharisha Ubaguzi Uwekezaji Wa Bandari Hizi hapa sababu miswada ya rasilimali kukwama

Thu, 31 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imeondoa bungeni miswada ya marekebisho ya sheria za mamlaka ya nchi kuhusu umiliki wa mali na rasilimali asilia na ile ya mapitio na majadiliano kuhusu masharti hasi katika mikataba ya mali na rasilimali asilia.

Mbali na hilo, Bunge lilipitisha sheria tatu kati ya tano zilizokuwa kwenye Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 2 wa mwaka 2023 uliowasilishwa Juni 28, 2023.

Marekebisho ya sheria zilizopitishwa Agosti 29, 2023 bungeni jijini Dodoma ni ya Sheria ya Nguvu ya Atomu, Chuo cha Usafirishaji wa Majini Dar es Salaam na ya Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda.

Hata hivyo, Bunge lilianza na zuio la wabunge kujadili sakata la bandari baada ya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kusema wataendelea kuwa wasikilizaji hadi wakati utakapofika kama itabidi wataishauri na kuikosoa Serikali.

Dk Tulia alisema Bunge lilishamaliza mjadala huo, hivyo wabunge wanatakiwa kuendelea kuwasikiliza wananchi.

Alisema katika kipindi ambacho wabunge walikuwa majimboni, wamewasikiliza watu wengi na kupokea mambo mengi ambayo yamezungumzwa kwa mawanda mapana, hivyo wanapaswa kuyachukua na utakapofika wakati watayatumia kwa ajili ya kuishauri Serikali.

“Kuhusu suala la bandari tuendelee kuwasikiliza wananchi, kwani sisi Bunge tulishamaliza kwa sehemu yetu na kwa kuwa Bunge lilishafanya uamuzi wake basi wakati wetu ni pale tutakapohitaji mikataba iletwe bungeni ili tuipitie,” alisema.

Baada ya maelezo hayo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Eliezer Feleshi aliwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba 2 wa mwaka 2023, akisema umefanyiwa marekebisho kwa kuondoa mapendekezo ya marekebisho ya sheria hizo.

Alisema hatua hiyo imekuja baada ya Serikali kufanya majadiliano na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria na kukubaliana na ushauri wa kamati hiyo.

“Ili kutekeleza ushauri huu wa kamati, muswada umefanyiwa marekebisho kupitia jedwali la marekebisho na kuondoa sehemu ya nne na tano (zinazohusiana na sheria hizo mbili),” alisema Jaji Feleshi.

Katika mapendekezo ya marekebisho hayo, Serikali ilisema inafanya marekebisho hayo ili kuhakikisha utekelezaji wa sheria hizo hauathiri utendaji wa maeneo ya bandari, bandari za nchi kavu na bandari za maeneo ya maziwa nchini.

“Madhumuni ya marekebisho haya ni kuwezesha bandari katika Jamhuri ya Muungano kufikia viwango vya kimataifa vya kiutendaji na kuvutia nchi nyingi zaidi na shehena kubwa za mizigo kutumia bandari za hapa nchini,” alisema Dk Feleshi.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dk Joseph Mhagama akisema kamati yake ilifanya majadiliano ya kina na Serikali kuhusu maudhui ya marekebisho hayo.

“Baada ya majadiliano hayo Serikali ilikubali ushauri wa kamati na kuleta marekebisho kwa kufuta sehemu ya nne na tano ya Muswada (sheria hizo mbili),” alisema Dk Mhagama.

Agosti 16 mwaka huu, kamati hiyo iliita wadau kutoa maoni ya muswada, huku Dk Mhagama akisema walipokea maoni ya marekebisho ya sheria tatu kati ya tano kutoka kwa wadau na mbili zilizoondolewa jana bungeni.

Alisema hawakuwa katika nafasi ya kupokea maoni kwa sababu kuna hoja walizoomba ufafanuzi kwa Serikali.

Juni 10, mwaka huu, Bunge hilo liliridhia azimio la makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji wa bandari nchini.

Tangu kuridhiwa kwa mkataba huo, kumekuwa na mjadala mkubwa maeneo mbalimbali uliowagawa wananchi pande mbli, wanaounga mkono mkataba huo na wale wanaoupinga wakisema hauna masilahi kwa Taifa.

Kikokotoo bado kaa la moto

Sakata la kikokotoo cha mafao ya mkupuo bado ni kaa la moto na jana liliwaibua wabunge waliokuwa wakitaka Serikali kufanya marekebisho kwenye jambo hilo.

Katika kipindi cha maswali na majibu, wabunge Priscus Tarimo (Moshi Mjini), Kasalali Mageni (Sumve), Joseph Kakunda (Sikonge) na wa viti maalumu Mariam Kisangi, Mariam Nyoka na Ester Bulaya walihoji kuhusiana na suala hilo.

Mageni alihoji ni lini Serikali itapeleka haraka bungeni muswada wa kuondoa mambo ya kikokotoo kwa kuwa watumishi nchini hawakitaki.

Akijibu maswali ya wabunge hao, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi alisema kanuni hiyo iliandaliwa kwa kuzingatia haja ya kuboresha na kuwianisha mafao ya wanachama na kuifanya mifuko ya pensheni kuwa endelevu.

“Mpango wa Serikali ni kuendelea kuwaelimisha wananchi, hususan waajiri na wanachama wa mifuko ya pensheni, wakiwamo wastaafu kuhusu faida ya kanuni mpya ya mafao ya pensheni,” alisema Katambi.

Kuhusu watumishi kuwa hawakitaki kikokotoo, Katambi alisema wanaotoa kauli hiyo ni wale ambao hawajafanya utafiti kwa kuwa ni asilimia 81 ya watumishi wanapongeza na kusifia kikokotoo.

Mikopo ya Elimu ya juu giza

Jambo jingine ni Serikali itafanya mapitio ya Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kuangalia mambo mbalimbali, ikiwamo vigezo vya utoaji wa mikopo hiyo.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga alisema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa viti maalumu (CCM), Rose Tweve aliyehoji haoni kama kuna haja ya kufanya mapitio ya sheria ya bodi ya mikopo ili kutatua changamoto nyingi ambazo watoto wa Kitanzania wanapata kupata mikopo ya elimu ya juu.

Akijibu swali hilo, Kipanga alisema katika Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), wametenga fedha kwa ajili ya kufanya mapitio ya sheria hiyo kwa kuwa wanafahamu sheria hiyo ina miaka 19 tangu itungwe.

“Sasa hivi tunafanya mapitio ili kuangalia vigezo na namna gani ya kuweza kuhuisha taarifa zetu, lakini vilevile namna ya utoaji wa mikopo yetu. Naomba niwaondoe hofu wabunge hadi kufika mwisho wa mwaka huu shughuli hii itakuwa imekamilika,” alisema Kipanga.

Naye Spika Tulia alishauri wakati mchakato wa kufanya mapitio ya sheria hiyo unaendelea, Serikali iangalie namna ya kutenga fedha kwa ajili ya watoto ambao mfumo unakuwa haujawatambua, lakini wana shida ya kupata fedha za kugharamia masomo yao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live