Upatikanaji wa mayai katika maeneo mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam umepungua kutokana na utagaji mdogo wa kuku unaosababishwa na hali ya hewa ya baridi.
Mayai ni miongoni mwa bidhaa zilizoongezeka bei na huenda hali hii ikaendelea hadi Desemba mwaka huu kutokana na kuendelea kuongezeka kwa gharama za uendeshaji kwa wafugaji.
Uchunguzi wa Mwananchi katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam ikiwemo Tegeta, Mbweni, Kinondoni, Tabata, Mabibo na Ubungo umebaini bei ya rejareja ya yai lisilo la kienyeji ni kati ya Sh400 hadi 500 kwa baadhi ya maeneo kutoka Sh350 kipindi kama hiki mwaka jana. Also Read
Daladala Arusha wasitisha mgomo, wengine wasusa Kitaifa 1 hour ago
PRIME Urasimu katika utoaji vibali unavyochochea ujenzi holela Kitaifa 1 hour ago
Pia bei ya jumla kwa trei moja imeongezeka kwa kati ya asilimia 40 hadi asilimia 50 ikiuzwa kati ya Sh9,500 hadi Sh11,000 katika kipindi hicho.
Wakati bei ya bidhaa hiyo ikipaa, baadhi ya wafugaji wanasema ni fursa kwa kujiingizia kipato ili kufanya shughuli zao kwa ufanisi, kwani ni nadra mayai kufika bei iliyopo sasa.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa huduma za mifugo (DVS) katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Hezron Nonga alisema kuna baadhi ya maeneo kuna upungufu wa mayai na mengine ni wastani, lakini kumekuwa na mahitaji makubwa kuanzia mwishoni mwa Julai.
Mfugaji na mfanyabiashara wa mayai, Boniface Jacob anasema kwa sasa anauza trei ya mayai kwa bei ya jumla kuanzia Sh 8,000 hadi Sh 9,000 na kwamba kadiri siku zinavyosonga bei hiyo itapanda, kama haitapanda zaidi itaishia Sh9,000.
“Inawezekana hadi Desemba bei ikawa Sh 12,000 kwa trei moja, lakini yakishuka mwisho itakuwa Sh 9,000 hasa tunapoelekea katika sikukuu za mwisho wa mwaka. Bei ya Sh9,000 au Sh10,000 inakuwa katika msimu wa sikukuu sio siku za kawaida," anasema.
Jacob aliyewahi kuwa Meya wa Manispaa za Ubungo na Kinondoni, anayesafirisha pia mayai katika mikoa mbalimbali anasema si ajabu kwa sasa mkoani Katavi wakanunua trei moja kati ya Sh 12,000 na Sh 13,000 kutokana na bidhaa hiyo kupanda bei.
Muuza chipsi maeneo ya Mbweni, Abdallah Mfunga anasema hivi sasa bei za mayai hazieleweki kwa sababu trei inauzwa kuanzia Sh9,500 hadi Sh 10,000.
“Mwaka jana mambo yalikuwa mazuri, lakini mwaka huu yamepanda, ingawa nachukua kwa bei Sh10,000 kwa trei moja siwezi kupandisha gharama za chipsi kulingana na hali ya maisha na kipato cha watu.
“Mayai ni muhimu katika biashara yangu bila mayai hakuna chipsi, kwa siku nanunua trei tatu hadi nne,” anasema.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wa Kuku wa Nyama Tanzania (Tabrofa), Aloyce Makoye anasema sababu ya kupanda bei kumetokana na uhitaji kubwa wa mayai.
Pia, Makoye anadai bei zitapanda zaidi kwa sababu hivi sasa kuna changamoto ya upatikanaji wa dola ya Marekani.
“Asilimia kubwa ya soya inayotumika kutengeneza chakula cha kuku inatoka nje ya nchi. Pia wale kuku wanaotaga mayai kwa ajili ya kutotoresha wanatoka nje ya nchi,” anasema Makoye.
Upatikanaji wa dola umekuwa bado changamoto, inayoathiri sekta mbalimbali ikiwemo mafuta, ambapo hivi karibuni Chama cha Waagizaji na Wasambazaji Mafuta Tanzania (Taomac), kilisema hali inaweza kuzidi kuwa mbaya iwapo tatizo hilo halitatuliwa kwa haraka.
Akijibu malalamiko kuhusu uhaba wa dola hivi karibuni, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba alisema benki hiyo huingilia soko kila inapowezekana kwa kusambaza dola zaidi pamoja na kuanzisha mpango wa dhamana ya mikopo ya nje.
Kauli ya wizara
Akizungumzia suala hilo, Profesa Nonga anasema biashara ya mazao ya mifugo inaendana na msimu, akisema kuna msimu hali inakuwa nzuri kwa wafugaji, wakati mwingine hali inakuwa mbaya.
“Kwa mfugaji ni neema, lakini kwa mlaji wa mwisho ni maumivu kwake, ndio maana akiona bei imetoka kuanzia Sh6,000 hadi Sh10,000 anaona faraja. Bei zinapopanda mfugaji anaambulia chochote kama faida,” anasema.
Profesa Nonga anasema kupanda kwa bei za mayai kunatokana na mabadiliko ya hali ya hewa, akisema hali ya Dar es Salaam mwaka huu, ipo tofauti na mwaka jana.
“Msimu wa baridi kunakuwa na changamoto za kumhudumia kuku, ndio maana kiwango cha kutaga kinapungua. Kiwango cha kutaga kikipungua, uzalishaji wa mayai unakuwa mdogo.
“Uzalishaji mayai ukipungua maana yake upatikanaji wa bidhaa hii sokoni unakuwa mdogo na kusababisha bei kuwa juu,” anasema Profesa Nonga na kuongeza bidhaa yoyote ikizalishwa kwa kiwango kidogo lazima bei ipande.
Alifafanua kuwa baridi ikiongezeka kiwango cha kuku kutaga kinapungua na wakati mwingine vifaranga au kuku wanaugua mafua ya mara kwa mara
Kwa mujibu wa Profesa Nonga, upatikanaji wa mayai hivi karibuni umekuwa kwa kuweka ombi maalumu kwa sababu wanaouza au kufuga wanakuwa na maombi mengi ya wateja wanaohitaji bidhaa hiyo.
“Wakati wa baridi kuku wanakula sana chakula, lakini wanataga kidogo kwa sababu miili yao inahitaji nguvu nyingi ili kukabiliana na hali ya hewa. Ndio maana bidhaa inakuwa pungufu sokoni huku mfugaji akiwekeza fedha nyingi katika kuwahudumia kuku,” anasema.
Anasema ili mfugaji afidie gharama hiyo analazimika kuongeza bei ya mayai sokoni na kwamba lazima wafanyabiashara wanunue ili kuuza kwa sababu bidhaa hiyo ni chache.
“Endapo kukitokea mvua za el nino, basi tutarajie mayai kupanda zaidi bei kwa sababu uzalishaji utapungua kutokana na hali ya hewa. Pia kuelekea sikukuu ya Krismasi na Mwaka mpya mayai huwa yanapanda, maana yake yanaweza yakapanda hadi Januari au Februari mwanzoni,” anaeleza.
Hata hivyo, Nonga amewataka Watanzania kutambua kwamba mazao ya mifugo yanaendana na msimu, akisema msimu ukiwa yanakuwa mengi na bei zinaporomoka, lakini msimu wa mavuno yakiwa madogo bei zinapanda.
Anasema sio ajabu mayai kupanda bei kwa sababu baadhi ya bidhaa zipo juu katika masoko mbalimbali, akiwataka Watanzania kuwa wavumilivu.
“Asilimia 60 hadi 70 ya wafugaji wa kuku wapo Dar es Salaam, ukiona picha ya mkoa huu ipo hivi, basi ukienda mikoa mingine huenda bei zitakuwa juu zaidi,” anasema Profesa Nonga.
Mkazi wa Tabata, Eliza Frank anasema amejiwekea utaratibu wa kula mayai matatu kila siku, lakini kwa siku za hivi karibuni alikwenda dukani na kuambiwa bei imepanda hadi kufikia Sh 400 kwa yai moja.
“Nakumbuka nilibeba Sh1,000 nikadhani nitapata mayai matatu, lakini nikapata mawili pekee. Hata hivyo nilipoamua kununua trei moja moja nikaambiwa kwa sasa Sh12,000 kutoka Sh 8,000,” anasema Frank aliayeamua kununua ya Sh10,000
Faida za mayai mwilini
Mayai ni chakula muhimu katika mwili wa binadamu na yana virutubisho na madini mengi yenye faida.
Mayai yana protini, vitamini A, D, B na B12 na madini ya lutein na zeaxanthin yanayoweza kuzuia mtu kupata matatizo ya macho atakapozeeka.
Pia mayai yana kemikali iitwayo choline ambayo ni muhimu kwa ukuaji na afya ya ubongo wa mtoto tumboni na ndio maana mwanamke mjamzito anashauriwa kutumia yai moja hadi mawili kwa siku.