Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hizi hapa nondo tano kufikia maendeleo

Uchumi Uchumiiii (600 X 300) Hizi hapa nondo tano kufikia maendeleo

Thu, 24 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

akati Rais Samia Suluhu Hassan akitimiza mwaka mmoja madarakani, baadhi ya wataalamu wa uchumi, siasa na diplomasia wamempongeza huku wakitaja mambo matano yatakayoifikisha Tanzania kwenye ukuaji wa uchumi.

Wakizungumza katika kongamano la ujenzi wa viwanda kufikia uchumi shindani lililoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na kijamii (ESRF), wasomi hao walitaka kuwepo mkakati wa kitaifa wa maendeleo utakaokuwa ramani ya utendaji, kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma, kudhibiti deni la Taifa, kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na kutumia diplomasia ya uchumi kuvutia wawekezaji.

Akitoa mada katika mkutano huo, Profesa wa uchumi, Samuel Wangwe alisema ndani ya mwaka mmoja Rais Samia ameleta mabadiliko makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

“Katika kipindi hicho tumeshuhudia kufunguliwa kwa uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari. Katika kipindi kifupi, kipimo cha furaha (Happiness Index) kwa Watanzania kimeongezeka,” alisema.

Alitaja uhuru wa demokrasia na vyama vya siasa vilizuiwa kufanya kazi zake, lakini sasa vifungo hivyo vimelegezwa.

“Hata utawala wa sheria umeanza kufuatwa. Tumeona wale watu waliokuwa wakitukana watu na kufanya uhalifu wakati ule, sasa wamefikishwa mahakamani,” alisema. Akizungumzia uhusiano wa uhuru wa kisiasa na uchumi, Profesa Wangwe alisema kufunguliwa kwa demokrasia na uhuru wa kujieleza kumefungua milango ya kiuchumi. Aligusia hatua ya Rais Samia kuwashirikisha wadau wa biashara ikiwemo sekta binafsi katika ziara zake nje ya nchi, imewasaidia wadau hao kuwakutanisha na masoko na wabia katika biashara hizo.

“Ukuaji wa uchumi uliofikia asilimia 4.8 na 4.9 unatarajiwa kufikia asilimia 5.5 mwaka huu na mfumuko wa bei kufikia asilimia 4. Mikopo chechefu imeshuka kutoka asilimia 9.3 hadi asilimia 8.2 na mapato ya ndani yameongezeka kwa rekodi ya Desemba 2021 Sh2.5 trilioni,” alisema.

Mambo matano

Pamoja na hayo, Profesa Wangwe alisema bado hakujawa na mkakati wa kitaifa unaobainisha mwelekeo na majukumu ya Serikali za mitaa kama wakala wa Serikali.

“Mkakati huo utaweka ramani kwa viongozi wote, hivyo hakutakuwa na ubishani, bali wote watafuata mwongozo,” alisema.

Katika hilo pia alieleza haja ya chama tawala (CCM) kuwa na sera na mikakati inayoendana na kasi ya ukuaji wa uchumi hasa ujenzi wa viwanda.

“Swali la kujiuliza ni kama muundo wa ndani wa CCM una uwezo wa kubeba dhana ya maendeleo ya Taifa ya utajirisho na ukuaji wa viwanda?” alihoji.

Kuhusu udhibiti wa fedha za umma, alisema, “Ni kweli tumeona taarifa za CAG (Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kuhusu matumizi ya fedha za umma, lakini tusiwe tunangojea tu taarifa hizo. Hatua zichukuliwe kila inapobainika.”

Pia alizungumzia deni la Taifa akisema, japo halijafikia kwenye hali mbaya, lakini kuwe na mikakati ya kuzuia lisiongezeke. “Kila Serikali inapoulizwa inasema bado deni ni himilivu, lakini hawaelezi wanafanya nini ili deni lisiongezeke,” alisema. Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19, Hivi karibuni Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alikaririwa akisema Deni la Taifa ni himilivu.

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa na kituo cha Biashara (WTO), Modest Mero alieleza haja ya Serikali kulipa uzito suala la mabadiliko ya tabia nchi.

“Watanzania wengi wanafanya kazi katika mazingira hatarishi ikiwemo kilimo cha kujikimu na uvuvi. Mabadiliko ya tabia nchi yameathiri maeneo ya pwani, uzalishaji wa chakula na vyanzo vya maji kwa gharama ya asilimia moja ya pato la ndani (GDP),” alisema.

Alisema gharama hizo zinatarajiwa kuongezeka miaka 10 ijayo na itaongeza matukio ya ukame na mafuriko.

“Kuna haja ya kuimarisha sekta ya uzalishaji kwa kuwa na teknolojia bora na mikakati ya fedha itakayodhibiti athari za mabadiliko ya tabia nchi,” alisema.

Akizungumzia diplomasia ya uchumi, Mero alisema kuna umuhimu wa kujihusisha na ushirikiano wa kimataifa na kuweka mazingira bora, ili kuvutia wawekezaji.

‘Mazingira ya biashara yanatuma ujumbe kwa wawekezaji na wafanyabiashara wa kimataifa kuhusu vihatarishi vya biashara zao. Diplomasia ya uchumi ina wajibu wa kuwahamasisha wadau kuandaa mazingira wezeshi kwa ajili ya uwekezaji na biashara,” alisema.

Mkakati wa Serikali

Akizungumzia mikakati inayofanywa na Serikali, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara (Uwekezaji), Ally Gugu alisema mkakati uliopo ni kufikia malengo ya 2025 ikiwa pamoja na kuzalisha ajira milioni nane na uzalishaji wa viwandani utakaofikia asilimia 18.

Awali akifungua mdahalo huo, Mkurugenzi mtendaji wa ESRF, Dk Tausi Kida alisema lengo ni kuwaleta karibu wadau wa uchumi na jamii na kutafakari maendeleo ya uchumi na kijamii ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live