Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hizi hapa ahadi ya Serikali kwa wakulima kuhusu pembejeo

Mbolea 1 Hizi hapa ahadi ya Serikali kwa wakulima kuhusu pembejeo

Tue, 17 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeahidi kuendelea kuratibu upatikanaji wa pembejeo ikiwemo mbolea ya ruzuku kwa wakulima, lengo likiwa ni kuongeza uzalishaji na uhakika wa chakula nchini.

Ahadi hiyo imetolewa mjini Kigoma leo Oktoba 16, 2023 na Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

Akihitimisha maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yaliyofanyika Kitaifa mjini Kigoma, Andengenye amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha chakula kinapatikana kwa zaidi ya asilimia 100.

Utafiti ni eneo lingine litakalopewa kipaumbele baada ya Serikali kuahidi kuongeza bajeti kufanikisha tafiti zitakazowezesha upatikanaji wa mbegu bora na hatimaye tija katika kilimo.

‘’Huduma ya ugani, kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji, kuanzisha mpango wa mashamba makubwa pamoja na mpango wa ajira kwa vijana katika kilimo (BBT) ni eneo lingine la kipaumbele katika mipango ya Serikali ya kuongeza tija katika sekta ya kilimo,’’ amesema Andengenye

Ofisa Mfawidhi wa Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) Kanda ya Ziwa, Martine Nsongoma amesema taasisi hiyo inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali kudhibiti ubora wa mbegu ikiwemo kuongeza matumizi ya lebo za ubora.

Ametaja mkakati mwingine kuwa kuhakikisha wafanyabiashara wa mbegu wasio waaminifu hawapenyezi mbegu zisizo na ubora.

“Elimu kwa umma kuhusu matumizi ya mbegu zilizothibitishwa na Tosci na usajili wa wafanyabiashara wa mbegu pia imesaidia kudhibiti mbegu feki nchini,’’ amesema Nsongoma

Mwakilishi kutoka Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) kupitia mradi wa Mpango wa Pamoja wa Kigoma (KJP), Theresia Masoe amewahimiza wakulima kutumia ushauri kutoka kwa wataalam wa ugani kuongeza tija katika uzalishaji wa chakula nchini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live