Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hivi ndivyo jinsi ufugaji unavyo na tija

F62dbf2750f8e8d1a59e3ca06bc10887.jpeg Hivi ndivyo jinsi ufugaji unavyo na tija

Fri, 17 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema ufugaji wa kibiashara ni jawabu la ukosefu wa ajira kwa vijana nchini. Ulega aliyasema hayo juzi wilayani Kongwa alipozungumza na viongozi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) na Taasisi ya PASS Trust baada ya kutembelea Kituo cha Taliri Kongwa na Kituo atamizi cha kilimo biashara kwa vijana cha PASS-AIC.

Alisema ufugaji na uvuvi wa kibiashara na kisasa ni suluhisho kubwa katika ajira kwa vijana na kuongeza kipato. “Tukifanya shughuli hizi kibiashara kutasaidia watu kuondokana na maisha duni, kwa hiyo kazi tunayoifanya hapa ya uatamizi ni kutengeneza wafanyabishara wa ufugaji wa kisasa,” alisema.

Aliongeza: “Tunanenepesha mbuzi ambao wanaingia sokoni na kazi hii tumeianza hapa Kongwa na tunatamani iende sehemu nyingi sana na wengine tunawakaribisha waje wajifunze hapa.

Halmashauri zitakazopendezwa na mradi huu waingize kwenye maeneo yao ili kutoa ajira zaidi kwa vijana wetu.” Aidha, Ulega aliahidi kuwa serikali itawasaidia kupata maeneo vijana watakaovutiwa na kazi hiyo.

“Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa sasa tutawapa ardhi wale wanaokwenda kufuga na si kuchunga, pia serikali yetu imefungua milango ya kibiashara tuna viwanda viwili vikubwa vya nyama na mahitaji ni makubwa,” alieleza Ulega. Ulega alisema dhamira ya serikali ni kuhakikisha vijana wanapata mikopo ya kuboresha ufugaji wao na wengi kujiingiza kwenye shughuli hiyo.

Akitoa taarifa ya kituo atamizi, Mkurugenzi wa PASS-AIC, Tamimu Amijee, alisema kwa kipindi cha miaka miwili ya kituo hicho zaidi ya mbuzi 2,500 wa kienyeji wamenunuliwa na PASS kutoka kwa wafugaji katika maeneo tofauti kwa ajili ya vijana ambao wanaendesha biashara hiyo ya unenepeshaji wa mbuzi.

Alisema kuna tatizo la upatikanaji wa mitaji kwa vijana kwa ajili ya kilimo biashara kutokana na kuwepo na dhana kuwa vijana hawakopesheki. Amijee alisema mipango ya mwaka 2022/23 kituo kinategemea kuongeza idadi ya vijana kutoka 20 hadi 50.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Remidius Emmanuel, alisema wilaya hiyo imekuwa ikishirikiana na taasisi hizo ili kuleta matokeo chanya na kuinua uchumi kwa wananchi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live