Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hivi hapa vipaumbele uvuvi uchumi wa buluu

16f9484698f65a43959a4cd4e84b2195 Hivi hapa vipaumbele uvuvi uchumi wa buluu

Wed, 20 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema katika uchumi wa buluu lengo la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ni kuwapatia wavuvi zana za kuvulia, masoko, vyumba vya baridi, bandari za uvuvi na vyumba vya kuchakata samaki.

Dk Mwinyi alitoa agizo hilo alipozungumza na viongozi, watendaji wakuu na maofisa wa serikali baada ya kukamilisha ziara ya siku tatu katika Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alizitaka taasisi ziwe na ubunifu na zitafute wawekezaji na mikopo ili kuwawezesha wananchi katika sekta ya uvuvi kwa kuwa wananchi wengi Zanzibar ni wavuvi.

Dk Mwinyi alisema SMZ itaendelea kutoa mikopo kwa wajasiriamali na kuwataka wananchi wachangamkie fursa hizo kwa kuwa kuna fedha za kutosha zilizotengwa wa ajili hiyo.

Aliipongeza Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kwa kusimamia uwapo wa miradi ya uwekezaji kupitia sekta binafsi ukiwamo ujenzi wa shule za kisasa, nyumba za kukodisha na maduka.

Alisema kumekuwa na maeneo finyu kwa shughuli za wafanyabiashara na akazitaka idara za manispaa kutafuta fedha ili kupanua wigo wa maeneo ya kufanyia biashara hizo.

Alisisitiza umuhimu wa manispaa kuwa na ubunifu kupata mikopo itakayowezesha kuwa na miundombinu ya kutosha ya kufanyia biashara na akasema serikali ipo tayari kuweka dhamana.

Alizitaka idara za manispaa ziweke fedha za kutosha katika kuendeleza miradi ya maendeleo kutokana na makusanyo wanayofanya kwa kuwa fedha zinazotengwa hivi sasa hazikidhi mahitaji ya kuendesha miradi.

Alisema serikali imeamua kuendeleza ujenzi wa masoko ya Jumbi, Mwanakwerekwe na chini kwa kikosi cha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), baada ya kugundua kuwa sekta binafasi ilishindwa kukamilisha miradi hiyo kwa wakati.

Hata hivyo, alikitaka kikosi hicho cha JKU kifanye kazi ya kujenga masoko kwa kasi usiku na mchana kwa kuzingatia serikali iliwaweka pembeni wafanyabiashara ili kupisha ujenzi huo.

Alisema kuna maendeleo mazuri yaliofikiwa katika uendelezaji wa miradi ya ujenzi wa hospitali za wilaya na ya mkoa iliyopo Lumumba na kubainisha matumaini yake ya kukamilika ujenzi huo na kuzinduliwa katika kipindi cha sherehe za Mapinduzi, Januari 12, 2023.

Aliiagiza wizara hiyo kuandaa bajeti ili kuwe na mazingira bora katika maeneo ya hospitali na kujenga uzio, sambamba na kuweka utaratibu wa kuwaondoa watu wanaofanya shughuli karibu na maeneo ya hospitali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live