Wakati makali ya ukosefu wa ajira yakitajwa kuwaumiza zaidi vijana, bado urasimu na sera zisizotoa kipaumbele katika ubunifu na ujasiriamali vinatajwa na baadhi ya vijana kuwa chanzo tatizo hilo.
Hayo yamebainishwa na Zawadi Ching’o mmoja kati ya vijana waliohudhuria hafla ya kugawa ufadhili wa Sh1.2 bilioni katika awamu ya pili ya mpango wa Funguo unaotekelezwa na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa wabunifu 17 iliyofanyika Jumatatu Novemba 20, 2023.
“Nimefurahi kuona vijana wenzangu wakipata udhamini huu nina Imani bunifu zao zitaenda kutatua changamoto, japo bado sera na urasimu zetu hapa nchini hazitupi vijana vipaumbele na kutuamini katika masuala haya,”alisema.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Mazingira ya Biashara, Wizara ya Uwekezaji na Mipango, Baraka Aligaesha ambaye pia alihudhuria hafla hiyo alisema Serikali imejipanga kuondoa urasimu na kuboresha sera.
"Kama serikali, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, tunarahisisha taratibu za kisheria, kisera na kikanuni, kupunguza urasimu, na kutekeleza sera zinazopendelea ujasiriamali.
“Lengo letu ni kuifanya iwe rahisi kwa biashara kama hizi za startups kuelekea kwenye upeo wa biashara na kufanikiwa. Baadhi ya mipango hii inasaidiwa na marafiki zetu wa Umoja wa Ulaya kupitia Mpango wa Mazingira ya Biashara, Ukuaji, na Ubunifu (BEGIN),”alisema.
Jumla ya vijana 17 walipata ufadhili huo wa awamu ya pili ambao upo chini ya Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ambao unafanya jumla ya Sh3.8 bilioni zitolewe kwa kampuni changa tangu awamu ya kwanza hadi sasa kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).
Mmoja kati ya wanufaika wa mradi huo wa wamu ya pili, Mohamed Awami, Mwanzilishi mwenza wa kampuni ya Settlo alisema ufadhili huo utawasaidia kuwafikia wafanyabiashara wengi wadogo.
“Kampuni yetu inatangeneza mifumo inayosaidia wafanyabiashara wadogo kutunza rekodi nzuri ambazo zitawasaidia kupata mikopo, awali tulikuwa tunawafikia wachache lakini kutokana na ufadhili huu huduma itaongezeka na gharama zetu zitapungua,”alisema.