Janga la kingo za bwawa la majitope la mgodi wa almasi wa Williamson Diamond Limited (WDL) eneo la Mwadui kupasuka limeacha hisia hasi na chanya kwa wakazi wa vijiji vya Nyenze na Ng'wanholo, wilayani Kishapu.
Kwa upande mmoja, tukio hilo limeacha hisia hasi kwa wananchi 304 baada ya makazi, samani za ndani, mifugo na mashamba yao kuharibiwa kwa ama kufunikwa au kusombwa na majitope kutoka bwawa hilo Novemba 7, mwaka jana.
Majitope hayo yalisambaa umbali wa takribani kilomita nane na kuacha kilio kwa kaya 19 zinazopakana na mgodi huo na waathirika kuhifadhiwa eneo salama na wasimamizi wa mgodi.
Hata hivyo, janga hilo lilikuwa na upande chanya ambapo waathirika walilipwa fidia ya zaidi ya Sh1.8 bilioni, samani za ndani na kujengewa nyumba mpya.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwangholo, William Bulugu alisema tukio hilo la kwanza kushuhudiwa eneo hilo lilisababisha wananchi kupewa hifadhi ya muda eneo maalumu, wakihudumiwa na mgodi.
“Eneo lile lililoathiriwa limethibitika kutokuwa salama kuishi, wananchi wanalazimika kuhamia maeneo mengine na hii imeathiri siyo tu shughuli za kiuchumi, bali pia za kijamii kwa sababu waathirika bado wanaishi kwenye kambi ya muda,’’ alisema Bulugu.
Alisema majitope pia yameharibu vyanzo asili vya maji, vikiwemo visima na mito iliyokuwa ikitegemewa kwa matumizi ya binadamu na mifugo.
Akilizungumzia hilo, mmoja wa waathirika wa tukio hilo, Revocatus Kurwa alisema janga hilo siyo tu limeharibu makazi yao, bali pia mashamba, hivyo kukosa maeneo ya kilimo.
Mwathirika mwingine, Maimuna Kasala alisema Novemba 7, 2022 ni siku itakayosalia kuwa yenye kumbukumbu mbaya katika maisha yake baada ya kupoteza makazi, samani za ndani na mazao yaliyokuwa shambani.
Kwa upande wake, Maria Juma alisema hajui atakavyomudu maisha baada ya nyumba, mazao shambani na mifugo yake wakiwemo ng’ombe 15 na mbuzi sita kusombwa na majitope.
Uzembe wabainika
Kamati iliyoundwa na Serikali, ikijumuisha wataalamu kutoka taasisi mbalimbali, zikiwemo Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), Tume ya Madini Tanzania (TMC), Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kuchunguza tukio ilibaini uzembe kuwa miongoni mwa sababu.
Katika taarifa yake, kamati ilibaini uongozi wa mgodi haukuchukua hatua mapema kuzuia janga hilo, licha ya kuta za bwawa kuonyesha dalili za kupasuka.
Katika mahojiano na Mwananchi kuhusu tukio hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Nemc, Dk Samuel Gwamaka alisema licha ya uchunguzi wa kina kubaini kuwa majitope kutoka bwawa hilo hayakuwa na kemikali, uzembe wa kutodhibiti viashiria vya awali vya kingo za bwawa kubomoka umechangia madhara kwa wananchi na mazingira.
Fidia ya mali, nyumba mpya
Kutokana na taarifa za uchunguzi na uwajibikaji, mgodi wa WDL umelazimika kubeba dhamana siyo tu ya kuwalipa fidia, bali pia kujenga nyumba mpya 47 kwa walioathiriwa.
Ofisa Mahusiano wa WDL, Bernard Mihayo alisema zaidi ya Sh1.8 bilioni zimetumika kuwalipa fidia wananchi 294 kati ya 304 walioathirika na majitope kutoka mgodini, wakati malipo kwa watu sita waliosalia yakisubiri maelewano kati ya wanafamilia baada ya kuibuka mgogoro kati yao.
"Fidia inahusisha fedha taslimu, mali na samani za ndani zilizoharibiwa. Pia tutajenga nyumba 47 kwa ajili ya waathirika katika maeneo mapya salama yatakayoamuliwa na Serikali,’’ alisema Mihayo.
Alisema ujenzi wa nyumba mpya unatarajiwa kuanza wakati wowote mwezi huu baada ya utaratibu kukamilika.
Charles Mang'ombe, mkazi wa Kata ya Mwadui Luhumbo aliyeathiriwa na majitope hayo, aliishukuru Serikali kwa kusimamia haki ya malipo ya fidia kwa wananchi.
“Naipongeza Serikali kwa kuuwajibisha mgodi kwa kuagiza ujenzi wa bwawa upya lenye uimara na ukubwa unaohimili majitope kutoka mgodini. Hii imeondoa uwezekano wa janga lingine na hivyo kutuhakikishia usalama,’’ alisema.
Kwa upande wa Mhandisi Mkuu wa mgodi wa WDL, Mipawa Shagembe alisema bwawa jipya lina urefu wa mita 8,000 na upana wa mita 760 na limejengwa kwa ubora na uimara zaidi.
Uzalishaji kurejea
Baada ya kusitisha uzalishaji kwa takribani siku 253 tangu janga hilo lilipotokea, uzalishaji umeanza Julai 15, mwaka huu.
Uzinduzi wa shughuli za uzalishaji mgodini hapo uliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme ambaye aliagiza kujengwa bwawa la akiba la dharura ili kuepusha uzalishaji kusimama kwa muda mrefu kama ilivyotokea.
“Pia nauagiza uongozi wa mgodi kupanda miti kuzunguka bwawa la majitope kuongeza uimara wa kingo, kutunza na kulinda mazingira,’’ aliagiza Mndeme.
Hasara ya Sh149 bilioni
Akitoa taarifa wakati wa uzinduzi huo, Meneja Mkuu wa WDL, Ayoub Mwenda alisema mgodi umepata hasara ya zaidi ya Sh149 bilioni tangu shughuli za uzalishaji zilipositishwa Novemba 11, 2022.
Alisema hasara hiyo imetokana na kukosa uzalishaji wa kati ya kareti 25,000 hadi 30,000 za almasi iliyokuwa ikipatikana kila mwezi kwa kipindi cha miezi tisa, ambapo kareti moja ya almasi katika soko la dunia ni Dola za Marekani 270.
“Hasara hii siyo tu imeathiri mapato ya kampuni, bali pia Serikali Kuu na Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kukosa kodi na ushuru mbalimbali. Utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia miradi ya sera ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) pia imeathirika,’’ alisema Mwenda.
Akifafanua jambo katika hafla hiyo, Mbunge wa Kishapu, Boniface Butondo aliuomba uongozi wa mgodi huo kuendelea kutekeleza sera ya CSR kwa kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili wananchi waone faida ya kuwapo kwa mgodi huo.