Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hii ndiyo app ya ‘Vsomo’ kwa wanafunzi wa ufundi

TanzaniaWeb

Wed, 12 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Julai mwaka huu, VSomo, programu ya simu inayotoa kozi fupi za mafunzo ya ufundi kupitia simu ya mkononi, iltimiza miaka miwili tangu kuanzishwa kwake ikilenga kuongeza wigo wa upatikanaji maarifa nchini.

Pamoja na kipindi hicho kuwa na watu karibu 10,000 waliojisajili huku ikiwa imepakuliwa mara 34,000, bado huduma hiyo ya kibunifu haijawafikia vijana wengi wanaohaha kutafuta ujuzi ili wajiajiri au kuajiriwa kukabiliana na changamoto ya maisha.

Pamoja na kwamba Vsomo ni moja ya programu chache za kibunifu nchini zinazolenga kuongeza ujuzi miongoni vya vijana hasa wakati nchi ikijikita kuwekeza katika uchumi wa viwanda, ni wachache wanafahamu umuhimu wa programu hiyo.

Vsomo ilibuniwa na mjasiliamali wa teknolojia aitwaye Geofrey Magila ambaye ni moja ya wajasiliamali walioingia kwenye orodha ya vijana 30 mabilionea wajao wenye chini ya miaka 30 Afrika mwaka 2017.

“Hadi sasa waliomaliza kozi hiyo ni watu 91 kutoka mikoa mbalimbali nchini na tayari baadhi wameshafungua biashara zao,” anasema Charles Mapuli, Mratibu wa Mradi wa Vsomo.

Inafanyaje kazi?

Vsomo inatoa mafunzo ya kozi fupi za ufundi za Veta za wiki nane ndani ya kipindi kifupi tu kisichozidi wiki nne kwa kutumia simu ya mkononi. Msomaji anatakiwa kupakua app hiyo kutoka kwenye Play store kwa wanaotumia simu za Android na kisha kujisajili kwa kutumia laini ya simu ya Airtel. Vsomo ina mpango wa kuweka app kwenye App Store kwa wanaotumia simu au tabiti zinazotumia mfumo wa iOS wa Apple.

Sifa kubwa anayejiunga na kozi hiyo ni uwezo wa kusoma na kuandika na awe na uhakika wa kuwa na simu ya kisasa wakati wote ili kumsaidia kujifunza nadharia ambayo sehemu kubwa ni maandishi na picha.

Kwa anayejisajili anaweza kuona tu kozi zilizopo na maudhui yake bila kuweza kusoma kozi yenye mpaka atakapolipia ada ya Sh120,000 kupitia Airtel Money ambayo inajumuisha hadi gharama za mafunzo kwa vitendo.

Wastani wa ada ya kozi fupi zinazotolewa na Veta kwa mujibu wa Mapuli ni kati ya Sh250,000 hadi Sh320,000 kwa kozi, hivyo kufanya Vsomo kuwa nafuu zaidi ya mara mbili ya gharama ya kawaida.

Mwanafunzi anayesoma kupitia Vsomo atasoma nadharia ya kozi husika na kufanya mitihani yote na kufanya miadi katika chuo cha Veta kilichopo jirani kwa ajili ya kufanya mafunzo ya vitendo kwa saa 60 ndani ya wiki mbili.

‘’Mtu anayesoma kupitia Vsomo anakuwa na uhuru na muda wake na anapunguza gharama za masomo. Ukiamua kusoma kwa siku mbili au mwezi au miezi mitatu sawa tu ilimradi mitihani yote ufaulu,” anasema Mapuli.

Mwanafunzi anayemaliza katika mafunzo hayo hupewa cheti sawa kabisa na yule aliyesoma kozi fupi ya wiki nane katika chuo chochote cha Veta nchini.

Mapuli anasema wahitimu wa kozi hizo wanatambulika na mamlaka zote nchini zikiwemo Mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji (Ewura), Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Wakala wa nishati vijijini (Rea) na nyinginezo.

Vsomo ni sehemu ya mradi wa huduma za jamii wa Airtel kwa kushirikiana na Veta ili kuwapa fursa zaidi vijana kupata ujuzi.

Makala haya kwa hisani ya wavuti wa nukta. www.nukta.co.tz



Chanzo: mwananchi.co.tz