Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hii ndio sababu ya ongezeko la kasi ya upakuaji mizigo Bandari ya Dar es salaam

62bef70d384d2359ba89bfbe6fdf9d7d Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Elihuruma Lema akitoa maelekezo kwa wafanyakazi wa Bandari

Mon, 13 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

UPAKUAJI wa shehena ya Salfa tani 38,500 zilizoingia Bandari ya Dar es Salaam Septemba 8 mwaka huu unatarajiwa kumalizika ndani ya siku 10.

Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Elihuruma Lema alisema jana kuwa hayo ni mafanikio ya utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam (DMGP) uliohusisha ujenzi wa gati namba moja hadi nane.

Alilieleza HabariLEO kuwa uwezo wa bandari hiyo umeongezeka na wanatarajia ukikamilika watakuwa na uwezo wa kuhudumia shehena tani milioni 30,000 kwa mwaka kutoka shehena tani milioni 16 za sasa.

“Septemba 8, mwaka huu tulipokea bandari yetu iliingia katika historia nyingine baada ya kupokea Meli ya Serene Theodore iliyokuwa na shehena ya sulphur (salfa) tani 38,500,tumeshaanza kuzipakua na ndani ya siku 10 tutakuwa tumemaliza, huu ni ufanisi wa hali ya juu wa bandari yetu,”alisema Lema.

Alisema hivi sasa wateja wa ndani na nje ya nchi zikiwemo nchi na kampuni zinaiamini bandari hiyo ndio maana wanaagiza shehena ya mizigo yao na kupitishia bandarini hapo.

“Ufanisi wa bandari yetu unakua kila siku, wateja wetu wanatoa mrejesho mzuri, hata hii meli imetoka moja kwa moja Qatar na shehena hiyo na haijasimama kusubiri nafasi bandarini, ilipofika tu Tanzania imekuja moja kwa moja bandarini na imeshaanza kushusha mzigo,”alisema Lema.

Alisema Julai mwishoni kwenda Agosti meli nyingine yenye shehena ya tani 15,000 za salfa ilishusha mzigo huo ndani ya muda mfupi na kuondoka na hiyo ikaongeza imani kwa wateja.

Alisema shehena hiyo ya tani 38,500 haijawahi kupokewa katika bandari hiyo kwa kipindi cha miaka 10 na kwamba shehena hiyo inakwenda Zambia na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC).

Alisema mradi wa DMGP wa thamani ya shilingi bilioni 337umeongeza ufanisi wa bandari hiyo kwa sababu ujenzi wa gati namba moja hadi tano ulikamilika na kuanza kutumika.

Lema alisema pia gati jipya maalumu kwa ajili ya kuhudumia meli za magari kwenye bandari hiyo iliyopewa jina la gati namba nane limeanza kufanya kazi.

Alisema mfano halisi wa mafanikio ya maboresho ni ujio wa meli za magari zilizotia nanga bandarini hapo ikiwemo yenye shehena kubwa zaidi ya magari kuwahi kuleta mzigo kama huo. Meli hiyo ya Tranqual Ace inayomilikiwa na Kampuni ya Mitsui ikitoka nchini Japan ilitia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam ikiwa na magari 3,743.

Mkurugenzi wa kampuni ya mizigo ya Epic Cargo iliyoratibu ujio wa mzigo huo wa salfa, Anthony Swai alisema meli hiyo iliyotoka Doha, Qatar ilitia nanga Septemba 8 saa mbili usiku na kwamba malori zaidi ya 1,664 yatatumika kuusafirisha.

Alisema kemikali hiyo itatumika kuchenjua madini. Swai alisema mzigo huo umeiwezesha serikali kuingiza dola za Marekani milioni 2.2, sawa na Sh bilioni 5.101, na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tazania (TPA) katika tozo ya kuhifadhi mzigo iliingiza Sh milioni 260.

Mkuu wa Usalama wa Bandari wa TPA, Mussa Biboze, alisema taratibu zote za kiusalama bandarini hapo zimefuatwa ikiwemo katika kushusha na kupakia salfa hiyo na kusimamiwa na Baraza la Taifa ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Chanzo: www.habarileo.co.tz