Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hifadhi 4 kupewa magari ya bil 2.5/- kukuza utalii

64254bb0e2a61e8890b8da7a9527b738 Hifadhi 4 kupewa magari ya bil 2.5/- kukuza utalii

Mon, 31 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIKA juhudi za kukuza sekta ya utalii kanda ya kusini na kuimarisha usalama na kupambana na majangili, serikali imekabidhi magari 14 yenye thamani ya Sh bilioni 1.5.

Magari hayo yamenunuliwa kupitia mradi wa kukuza sekta ya utalii (Re Grow) unaotekelezwa na Serikali kwa mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia.

Akizungumza katika hafla fupi ya makabidhianao ya magari hayo, Kamishina Mkuu wa Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Dk Alan Kijazi alisema magari hayo yatasaidia kupambana na ujangili na kukuza utalii katika hifadhi ukanda wa kusini.

Alisema kupitia mradi huo Serikali imepanga kuboresha miundombinu ya hifadhi zilizopo kusini mwa nchi ili kupanua wigo kwa watalii wengi kuzitembelea.

"Ukiangalia takwimu zetu zinaonesha kwa sasa hifadhi za kanda ya kaskazini ndizo zimekuwa zikifanya vizuri kwa kutembelewa na idadi kubwa ya watalii, hivyo jitihada zinahitajika kukuza utalii katika kanda ya kusini.

"Pamoja na magari haya lakini mradi huu pia utasaidia katika kuboresha hifadhi zilizopo kanda ya kusini kwa kurekebisha miundombinu kwa kufungua barabara na kujenga viwanja vya ndege kwa jili ya watalii kutua na ndege katika maeneo ya hifadhi," alisema.

Alisema kuwa magari hayo yatapelekwa katika hifadhi ya Ruaha, Mikumi na Udzungwa na magari mengine tisa yatakayoletwa hivi karibuni yatakuwa ni kwa ajili ya hifadhi mpya ya Nyerere.

Kupitia mradi huo jumla ya magari 23 yenye thamani ya Sh bilioni 2.5 yatakuwa yamefikishwa kwenye hifadhi nne za kanda ya kusini.

"Mradi huu ni wa miaka sita utagharimu dola za Marekani milioni 60, tunatoa shukrani zetu kwa Benki ya Dunia na Serikali yetu ya Tanzania kwa kusaini mkopo huu na kuthamini mchango wa sekta ya utalii nchini," alisema.

Mwenyekiti wa bodi ya Tanapa, Jenerali mstaafu George Waitara alisema mradi huo utasaidia kuimarisha sekta ya utalii nchini kwa kuboresha miundombinu kuvutia watalii zaidi.

"Hifadhi za kusini zimekuwa na changamoto ya miundombinu hususani ya barabara, hoteli na viwanja vya ndege ambayo imekua ikichangia kutopokea watalii wengi, lakini kupitia mradi huu, tunakwenda kulimaliza hili," alisema.

Waitara alisema pia mradi huo utasaidia katika kuimarisha shughuli mbadala katika hifadhi na kuimarisha usimamzi wa mazingira.

“Mradi huu pia utasaidia kuboresha hifadhi katika nyanda za kusini mwa nchi yetu."alisema.

Akizungumza kabla ya kukabidhi magari hayo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu aliagiza magari hayo yatumike kwa malengo yaliyokusudiwa.

Alisema zinahitajika jitihada kubwa za uwekezaji, katika hifadhi zilizopo kanda ya kusini ili kufikia kama zile za kanda ya kaskazini ambazo zinafanya vizuri hivi sasa katika sekta ya utalii nchini.

Chanzo: habarileo.co.tz