Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo ameitaka jamii kutunza na kuhifadhi mazingira ili kuokoa ikolojia kutokana na takribani hekta 469,420 za misitu kuharibiwa kila mwaka.
Jafo alisema hayo jana alipokuwa akitoa tamko la serikali la maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo Juni 5 na kwa mwaka huu kitaifa itafanyika jijini Dodoma.
Alisema mbali na misitu kuharibiwa, pia kuna tatizo la utupaji holela wa taka pamoja na uwapo wa athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Hali hii inaathiri maisha ya viumbe mbalimbali ikiwamo ya mifumo ikolojia ambapo hadi sasa imeliletea taifa hasara ya takribani asilimia tano ya Pato la Taifa…Maadhimisho ya Siku ya Mazingira yaendelee kuwa chachu ya kuongeza kasi ya uhamasishaji wa jamii kushiriki shughuli za kuhifadhi na kutunza mazingira nchini,” alisema.
Kaulimbiu ya kitaifa inayoongoza maadhimisho ni ‘Tanzania ni moja tu: Tutunze Mazingira’.
Wakati huo huo Jafo aliwataka Watanzania wote kufahamu kuwa utunzaji na uhifadhi wa mazingira ni jukumu la kila mtu. Alisema kilele cha maadhimisho kitatanguliwa na Wiki ya Mazingira inayoanza Mei 28 hadi Juni 4, mwaka huu.
“Katika wiki hii shughuli mbalimbali za hifadhi na usafi wa mazingira zitafanyika katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma zikihusisha wananchi, taasisi, shule, vyuo na viongozi mbalimbali,” alisema.
Alisema maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Mazingira ya mwaka huu pia yatahusisha maonesho ya wadau ya shughuli mbalimbali za kuhifadhi mazingira yatakayoanza Juni 1-5 mwaka huu katika viwanja vya Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Dk Jafo alisema Juni Mosi, Waziri Mkuu ataongoza watumishi kupanda miti pembezoni mwa barabara za mji wa serikali wa Magufuli City na leo miti 3,000 itapandwa eneo ya Iyumbu.
Alisema siku ya kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, Rais Samia Suluhu Hassan atahutubia wadau wa mazingira na taifa kwa ujumla kupitia vyombo vya habari, sambamba na kuzindua Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira.
Mpango huo umebainisha changamoto za mazingira kuanzia ngazi ya mamlaka za serikali za mitaa, mikoa pamoja na mifumo-ikolojia mahususi nchini huku ukitoa mapendekezo ya hatua za kukabiliana na changamoto husika kuendana na mahitaji ya kila eneo.
Mpango huo wa hifadhi na usimamizi wa mazingira utakuwa nyenzo muhimu katika kutoa muongozo wa kuandaa na kutekeleza miradi na programu za kuhifadhi mazingira nchini.