Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hazina yazitaka Tanesco, NHC kuchangia zaidi mfuko mkuu

Tanesco Hazina Hazina yazitaka Tanesco, NHC kuchangia zaidi mfuko mkuu

Mon, 21 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu amesema anakusudia kukutana na Bodi na Menejimenti ya Shirika la Ugavi wa Umeme nchini -- Tanesco na Shirika la Nyumba NHC ili wakubaliane namna ya mashirika hayo makubwa kuongeza mchango wa gawio katika mfuko mkuu wa Serikali.

Akizungumza katika Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma unaondelea jijini Arusha, Mchechu amesema NHC na Tanesco zimekuwa zikichangia zaidi ya Sh bilioni 2 kila moja hata hivyo kiasi hicho ni kidogo.

“Tunataka wachangie zaidi, hamuwezi kutupa Sh bilioni 2,” amesema akifafanua kuwa Hazina inahitaji taasisi hizo kuchangia zaidi ili sehemu ya mapato hayo yakawe mtaji kwa taasisi zingine za umma zenye uhitaji.

Katika taarifa za Ofisi ya Msajili wa Hazina Idadi ya taasisi zilizochangia katika mfuko mkuu wa Serikali kupitia gawio zimepungua kutoka 236 mwaka 2019 hadi taasisi 108 mwaka 2023 huku mapato yakiongezeka kutoka Sh bilioni 695.8 hadi Sh bilioni 777.1.

Vilevile michango ya taasisi binafsi ambazo serikali inahisa chache (minority shareholder) imeongezeka kutoka Sh bilioni 58 mwaka 2019 hadi Sh bilioni 231.2 mwaka 2023. Ongezeko hilo hata hivyo linatokana na taasisi 15 tu ambazo ni nusu ya taasisi 30 zilizochangia mwaka 2019.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live