Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Haya hapa maeneo 6 udhibiti bei ya mafuta

Mafuta Ya Petrol (1) Haya hapa maeneo 6 udhibiti bei ya mafuta

Wed, 13 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wadau wa mafuta nchini wametaja maeneo sita mwarobaini wa kudhibiti mfumuko wa bei nchini na kusema yakifanyiwa kazi kikamilifu yatakuwa dira.

Akizungumza kwenye mjadala wa sababu za ongezeko la bei ya mafuta na athari zake uliofanywa kwa njia ya mtandao wa zoom jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Godfrey Chibulunje alitaja maeneo hayo ni kusimamia mfumo wa uagizaji mafuta wa pamoja.

Chibulunje alisema mfumo wa uagizaji mafuta kwa pamoja ni eneo mojawapo walilojipanga kuendelea kulisimamia ili liwe tija zaidi ya kuleta uimara wa bei ya mafuta nchini.

Alisema tangu mfumo huo uanze kutumika nchini mwaka 2011 hadi leo, bei ya mafuta imekuwa imara na hakujatokea uhaba wa bidhaa hiyo.

Alisema wataendelea kuusimamia na pale kunapohitaji maboresho wako tayari mfumo ufanyiwe ili uwe na tija zaidi.

“Tutaendelea kuusimamia mfumo huu ni mzuri, tangu uanze kutumika nchini hatujawahi kuwa na uhaba wa mafuta, pia umepunguza muda mwingi uliotumika kupakua mafuta kwenye meli kwa sababu kila kampuni ilileta mafuta kwa meli yake, hivyo zilijipanga baharini kusubiri nafasi, lakini sasa hakuna hiyo kusubiri,” alisema Chubulunje.

Alitaja eneo jingine mwarobaini wa kudhibiti mfumuko wa bei kuwa ni kuongeza ushindani katika sekta ndogo ya mafuta kwa kuweka mazingira rafiki kuvutia wawekezaji wengi.

Alisema sekta hiyo ikiwa na wawekezaji wengi watafanya kuwepo na ushindani wa bei kwa sababu watawekeza vituo vingi vya mafuta hadi vijijini.

Eneo la tatu ni kushawishi vyombo vya fedha kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama mbalimbali kama tozo na kodi za ndani kwenye mafuta ili kutoa unafuu wa kodi ambao utafanya bei kutopanda.

Akizungumzia hatua hiyo kupunguza tozo na kodi kwa upande wa serikali, Waziri wa Nishati, January Makamba alisema tayari serikali imeshaanza kuchukua hatua na uchambuzi unaendelea ili kushughulikia hilo.

“Ya kikodi tumeshaanza kuchukua hatua, yawezekana taasisi ziko nyingi zinazotegemea mapato kupitia mafuta kila mmoja anataka apate kidogo, tulifanya uchambuzi na tumeondoa baadhi na tunaendelea ili kuleta unafuu,” alisema January katika mjadala huo.

Eneo la nne, Chibulunje alilitaja ni kuishauri serikali kuangalia uwezekano wa kujenga njia mbadala ya kusafirisha mafuta kwa kujenga bomba la mafuta badala ya kutumia malori kwa njia ya barabara ili kupunguza gharama za usafiri.

“Huu ni mpango wa muda wa kati na mrefu, tutaendelea kuishauri serikali iangalie kwenye hili kwa sababu tukiwa na bomba la mafuta na ujenzi wa vituo ukajengwa kwenye maeneo ya mkakati kama Dodoma na mikoa mingine tutapunguza gharama za kuyasafirisha,” alisema Chibulunje.

Aidha, alisema katika kuboresha miundombinu ya usafirishaji mafuta pia mpango wa ujenzi wa eneo la pamoja la kupokelea mafuta (SRT), bandarini likijengwa litaongeza ufanisi katika kushusha na kutawanya mafuta hivyo kuondoa gharama nyingine katika bidhaa hiyo.

Akizungumzia hilo, January alisema serikali ilishaanza mpango huo wa ujenzi wa SRT ili kupunguza gharama na kuondoa upotevu wa muda unaotumika na meli kushusha mafuta na kuyatawanya.

“Tukijenga hiyo SRT, meli itashusha mafuta kwa mpigo mara moja kisha yanatawanywa kwenda kwa wahusika, pia tuko kwenye mazungumzo na baadhi ya nchi rafiki ili kipindi hiki tuweze kuagiza mafuta kwa bei nafuu,” alisema.

Alisema katika kuongeza ushindani, serikali inaendelea kuliwezesha Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), liagize mafuta na kushindana kwa kulijengea uwezo ili liombe zabuni kama kampuni nyingine za mafuta.

Akichangia hoja hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Erasto Simon alisema hivi sasa TPDC sasa inaweza kushiriki kwenye zabuni mbalimbali za mafuta na hiyo itasaidia kuleta ushindani.

“Kwa uhalisia sasa tuna mafuta ya akiba ya zaidi ya siku 30 kwa aina zote na sheria inatutaka tuwe nayo kwa angalau siku saba, sisi tuko zaidi vizuri, ila eneo hili la kuboresha mazingira ya uwekezaji na miundombinu ya kupokea mafuta bandarini likifanyiwa kazi, tutapunguza kama sio kuondoa tatizo la bei kupanda,” alisema Simon.

Kwa mujibu wa Chibulunje, eneo la tano ni kuishawishi serikali kuangalia uwezekano wa kuanzisha mfuko wa kupunguza ongezeko la bei ya mafuta, utakaosaidia kupunguza makali ya bei ya bidhaa hiyo wakati wa mfumuko wa bei duniani kama kipindi hiki.

“Tukiwa na mfuko huo wa ruzuku utasaidia kupunguza makali ya bei kwa sababu utatumika na bei za mafuta ndani hazitakuwa na makali kama haya ya sasa pindi mfumuko wa bei duniani ukitokea na sisi tutashauri namna bora ya kuuanzisha mfuko huo,” alisisitiza Chibulunje.

Profesa Hamza Mokiwa, Diaspora aishiye Afrika Kusini, alisema ni vyema serikali ikaona umuhimu wa kuanzisha mfuko huo wa ruzuku utakaosaidia kupunguza makali pindi bei zinapopanda katika soko la dunia.

Eneo la sita kwa mujibu wa Profesa Mokiwa ni serikali kuangalia jinsi ya kuwekeza kwenye nishati mbadala na kufata tafiti zaidi ili kuja na matumizi ya vyombo vya moto kama magari yatumiayo nishati hizo badala ya kutegemea mafuta.

“Ni wakati sasa serikali ishirikiane na Diaspora na kuwekeza kwenye tafiti na ije na mipango ya uwekezaji wa nishati mbadala, tutumie magari ya nishati hiyo tusitegemee mafuta ya petroli au dizeli pekee. Hapa Afrika Kusini tunatengeneza magari yanayotumia nishati ya sola, tufike huko sasa,” alishauri Profesa Mokiwa.

Simon alishauri uboreshwaji wa miundombinu ya kupokea mafuta bandarini kutoka kwenye meli ukifanywa, meli za ukubwa wowote zitaweza kupakua mafuta kwa muda mfupi na hiyo itaondoa gharama nyingi za kusubiri upakuaji.

Diaspora Issa Shabani Kashingo aishiye Norway alisema nishati mbadala ndio suluhu ya mfumuko wa bei hivi sasa kwa mafuta ya petroli duniani.

Dk Ezra Chomete anayeishi Uingereza alisema tatizo la mfumuko wa bei sio kwa Tanzania pekee, bali tatizo la kidunia hivyo wote wanapaswa kushirikiana na serikali na diaspora kuangalia jinsi ya kusaidia badala ya kulaumu serikali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live