Mkurugenzi wa Huduma za Usalama, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Novatus Mpanda anasema: “Usalama wa meli wakati inapoingia kwenye bandari yoyote ni kipaumbele chetu cha kwanza. Tunatoa huduma mbalimbali kwa vyombo vyote vinavyoingia kwenye bandari zetu.
TPA inahakikisha usalama wa chombo chako wakati wote meli inapoingia nchini, inapotia nanga na inapoingia gatini.” Mkurugenzi huyo anasema ulinzi katika bandari unahusisha mambo mengi ambayo yanachangia katika usalama wa bandari, mali pamoja na meli zinazoingia.
Anasema kwa kuwa TPA inasimamia mfumo wa usafiri wa bandari kuu za bahari na za maziwa ambazo ni Dar es Salaam, Tanga na Mtwara na bandari ndogo za bahari kama Kilwa, Lindi, Mafia, Pangani na Bagamoyo huduma ambayo inahakikisha kila kitu kinaenda sawa ni ya usalama.
Bandari nyingine ambazo zipo katika mfumo wa usalama ni za maziwa chini ya TPA kama bandari za Mwanza Kaskazini na Mwanza Kusini, Nansio, Kemondo Bay, Bukoba na Musoma. Ziwa Tanganyika yenye Bandari ya Kigoma, Karema, Kabwe, Kibirizi na Kasanga. Ziwa Nyasa ni Bandari ya Itungi, Kiwira, Manda, Liundi na Mbamba Bay.
“Kwa kuwa dhamira na dira ya TPA ni kuendeleza na kusimamia bandari zinazotoa huduma za bahari na maziwa kwa kiwango cha kimataifa, kuhamasisha usimamizi wa vifaa/bidhaa katika kuhakikisha huduma bora inapatikana Afrika Mashariki, Kati na Kusini na kuongoza katika biashara ya bahari na maziwa kwa kutoa huduma bora na usimamizi mzuri wa bidhaa bandarini, sisi ni taasisi imara inayojali na kufuata utaratibu,” anasema Mpanda wakati akizungumzia masuala ya kwanini usalama ni suala nyeti.
Katika masuala ya uongozaji meli, bandari kubwa zote zina huduma ya mfumo wa safari za vyombo vya majini (VTS) na uongozaji wa vyombo vya majini vinapoingia na kutoka bandarini. Aidha, kwa Dar es Salaam katika eneo la uvutaji meli kuna vyombo vinne vya uvutaji wa uegeshaji meli gatini, vikiwemo A50 na 55 za kuvuta kwa kizuizi.
Pamoja na kuhakikisha kwamba meli inaingia na kutoka salama, Mkurugenzi huyo anasema kwamba kuna huduma shirikishi za usalama wa bandari na mizigo kama huduma za polisi na zimamoto, timu za matibabu na gari za kubeba wagonjwa na masuala ya udhibiti wa uchafuzi wa mazingira, maji katika gati.
“Timu zetu za polisi na zimamoto zinapatikana saa 24 kwa siku saba za wiki ili kujibu dharura yoyote bandarini na maeneo ya jirani,” anasema. Anasema kikosi cha zimamoto kinachofanya kazi kikamilifu na chenye vifaa vya kutosha kinajumuisha wataalamu wa uokoaji wenye uzoefu, wakiwa na vifaa vyenye teknolojia ya hali ya juu ili kukabiliana na chochote kinachotokana na moto au milipuko inayotokana na hatari za kemikali na kibayolojia.
“Kikosi hiki hufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kuhakikisha wafanyakazi, wageni na watumiaji wengine wa bandari wamejiandaa vyema kwa tatizo lolote la dharura. Mazoezi hayo hutumika kupima muda wa kukabiliana na hali hiyo na kutumika zaidi kuwafunza wahudumu wa dharura, wafanyakazi na watumiaji wa bandari ili kudumisha hali ya utayari na ufahamu mara kwa mara,” anasema Kaimu Mkurugenzi wa Masoko, Nicodemus Mushi.
Pamoja na kushughulika na usalama wa bandari, kikosi hiki pia kinashiriki katika juhudi za kuzima moto nje ya maeneo ya bandari kwa kushirikiana na mamlaka za mitaa husika inapobidi. Kutokana na kuwapo kwa shughuli mbalimbali na jamii kwa ajiliya kushughulikia usalama wao pia kuna timu za matibabu na ambulensi kwa ajili ya kubeba wagonjwa. Timu ya matibabu ya TPA zimejipanga kukabiliana na dharura ndani na maeneo ya karibu na bandari.
Timu hizi zinafanya kazi na ofisa mkuu wa matibabu ili kuhakikisha kuwa wafanyakazi na watumiaji wengine wowote wa bandari wako katika hali nzuri ya kiakili na kimwili. “Timu ya matibabu ina kituo maalumu cha afya chenye vifaa vya kisasa na wataalamu wenye uwezo wa kufanya upasuaji wa kuokoa maisha.
Pia kuna huduma ya ambulensi ya saa 24 ambao wako tayari kuhudumia wagonjwa wakati wowote. Pia kuna kituo cha mazoezi ya viungo chenye vifaa kamili vya mazoezi ya mwili na wakufunzi wa kitaalamu ili kuwaweka sawa wafanyakazi na wasiwe na msongo wa mawazo na magonjwa nyemelezi,” anasema Mushi.
Masuala hayo ya usalama hayapo katika Bandari ya Dar es Salaam pekee bali katika bandari zote za TPA ambayo ilianzishwa kwa Sheria ya Bandari Na.17 ya 2004 kuwa Mamlaka inayosimamia shughuli zote za bandari. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania inahudumia Tanzania na nchi zisizo na bandari ikiwemo Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Rwanda, Uganda na Zimbabwe kupitia huduma zake za kuhudumia shehena zinazokwenda au kutoka katika nchi hizo.
Kutokana na kuhudumia nchi hizo imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba kila kitu kinakwenda salama kwa ushirikiano na wadau wengine ambao wamekasimishwa kisheria kwa kuingia makubaliano na TPA. Katika masuala ya usalama Bandari ya Dar es Salaam ambalo ni lango kuu la kibiashara kwani asilimia 95 ya nchi zisizo na bandari inahudumiwa na bandari hii ni nyeti na ambalo linaendelea kuboresha muda wote kuhakikisha si usalama wa bandari pekee bali pia na shehena zinazopita hapo.
Nchi hizo zisizo na bandari ambazo zinatumia Dar es Salaam ni Malawi, Zambia, DRC, Burundi, Rwanda na Uganda. Kwa kuwa bandari ipo mahali pa kimkakati kutoa huduma za kibiashara na imesimama kama kiungo kikuu cha kibiashara si kutoka na kwenda nchi za Afrika Mashariki na Kati tu, bali nchi za Mashariki ya Kati na Mashariki ya mbali, Ulaya, Australia na Marekani idara zote za usalama zina mafunzo ya hali ya juu na pia teknolojia ya kisasa inatumika kuhakikisha usalama wa bandari.
Pia bandari inatoa maelekezo na ushauri wa watu binafsi kujilinda na kulinda bandari wakiwa katika kazi mbalimbali. “Huwa tunawashauri kufuata maelekezo ya usalama bandarini kuhusu vimiminika na namna ya kuwa salama unapofanya mambo mbalimbali bandarini,” anasema Mpanda.