Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hatimaye mjadala uchumi wa viwanda kuwasha moto leo

20720 Pic+uchumi TanzaniaWeb

Thu, 4 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Leo ndio leo, asiye na mwana aeleke jiwe kwani wadau wa viwanda nchini wanakutana jijini Dar es Salaam kujadili namna nzuri ya kuzichangamkia fursa kuelekea uchumi wa viwanda.

Katika Ukumbi wa Kisenga uliopo Kijitonyama, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage atakuwa mgeni rasmi akisikiliza maoni ya watoa mada watano watakaokuwa wanapokea maoni ya wataalamu, wafanyabiashara na wananchi wa kawaida.

Wazungumzaji wakuu usiku wa leo watakuwa ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Edwin Mhede, mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Lindam Group, Zuhura Muro na Filbert Mponzi, mkuu wa idara ya wateja wakubwa na Serikali.

Wengine ni mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Subash Patel na mkurugenzi wa maendeleo na biashara wa kampuni ya General Electric International, Gilman Kasiga.

Kama ilivyo ada, hakuna shughuli isiyo na washughulishaji. Katika kipengele hicho, mchumi na mtafiti mwandamizi wa Repoa, Dk Blandina Kilama akishirikiana na mjasiriamali Felix Mlaki, watakuwa waendesha mada watakaokuwa wanatoa nafasi ya washiriki wa jukwaa hilo kuchangia mada zitakazowasilishwa.

Wadhamini

Shughuli hii imeandaliwa kwa umakini mkubwa uliochangiwa na wadhamini walioifanikisha. Kwenye orodha hiyo kuna benki za NMB, KCB na Stanbic ambazo watendaji wake watapata fursa ya kumsikiliza kila mteja mwenye wazo, maoni au mkakati wa kumiliki kiwanda.

Sekta ya fedha ni muhimu sana katika utekelezaji wa mkakati huu wa kuwa na uchumi wa viwanda kwani wajasiriamali na wafanyabiashara wanahitaji fedha kufanikisha mipango yao.

Mchanganuo sahihi wa biashara au mradi wowote huzishawishi taasisi za fedha kutoa mkopo kwa riba ya soko kuufanikisha.

Shirika la Viwanda la Umoja wa Mataifa (Unido) na Chemba ya Madini na Nishati Tanzania (TCME).

Wengine ni kampuni ya ukaguzi wa hesabu za fedha KPMG, kampuni ya Sayona, Best – Dialogue na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji miongoni mwa wengi waliojitokeza kufanikisha jukwaa hilo kwa namna moja au nyingine.

Mkuu wa idara ya masoko na mawasiliano wa Stanbic, Desideria Mwegelo anasema benki hiyo inaunga mkono juhudi za maendeleo zinazochukuliwa nchini kwa kuwawezesha wajasiriamali kuanzia wadogo kufanikisha mipango yao ya uwekezaji na biashara.

Anasema dhamira ya Tanzania ya viwanda imekuwa ikipigiwa debe ila upatikanaji wa mtaji ni changamoto kwa wajasiriamali na wafanyabiashara ndogo na kati zinazochangia asilimia 27 ya Pato la Taifa (GDP) na kuajiri zaidi ya Watanzania milioni 5.2.

“Tumejikita katika kuwezesha mafanikio ya mpango wa maendeleo ya Taifa, benki inaunga mkono jitihada zitakazotatua changamoto zinazotatiza upatikanaji wa mtaji,” anasema Mwegelo.

Kupitia mjadala mzito wa washika dau kutoka sekta mbalimbali za uchumi, anaamini Jukwaa la Fikra la Mwananchi litatoa undani wa changamoto zilizopo na kutafuta njia stahiki zitakazoisaidia Serikali kuufikia uchuni wa kati mwaka 2025.

Maono ya Serikali ni kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 inayojikita kusisitiza kuipata Tanzania yenye uchumi wa kati unaotegemea viwanda kwa asilimia kubwa tofauti na sasa kilimo ndicho kinachochangia zaidi.

“Tukiwa benki bora katika uwezeshaji biashara ndogo na za kati nchini, Stanbic imejikita katika kukuza na kuendeleza biashara. Ushiriki wetu katika jukwaa hili ni sehemu ya kudhihirisha ushiriki wetu katika kuchochea maendeleo na kuwezesha uchumi wa viwanda,” anasema Mwegelo.

Waandaaji

Jukwaa hili la fikra linaratibiwa na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) wachapaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.

Kufanikisha shughuli hii ya kuwaleta pamoja wadau na kutoa fursa ya majadiliano yenye lengo la kuchochea mpango wa maendeleo ya Taifa kwa malengo yanayotekelezeka, MCL inashirikiana na kituo cha runinga cha ITV pamoja na Redio One.

Kuanzia saa 3:00 hadi 5:00 usiku wa leo, washiriki 500 watajumuika kwenye Ukumbi wa Kisenga wakijadili mada zitakazowasilishwa huku Watanzania wengine wote, ndani na nje ya nchi pamoja na wadau wa maendeleo ya Taifa hili wakifuatilia matangazo yatakayorushwa moja kwa moja kupitia ITV na Redio One.

Mkurugenzi mtendaji wa MCL, Francis Nanai baada ya mafanikio ya jukwaa la kwanza lililofanyika Juni 28 likijadili magonjwa yasiyoambukiza, awamu hii mjadala unaelekezwa kwenye fursa na changamoto kuelekea uchumi wa viwanda.

“Kila kitu kipo sawa. Maandalizi yote yamekamilika. Watakuwepo wafanyabiashara, wasomi na watafiti watakaotoa maoni na uzoefu wao kuhusu viwanda,” anasema Nanai.

Nanai anasema watu wengi walioalikwa wamethibitisha kuhudhuria jambo linalomaanisha kiu ya uhakika ya lengo kutimia kwa manufaa ya wananchi.

“Kila mmoja anataka kutoa maoni yake. Licha ya vituo vya ITV na Redio One, kutakuwa na fursa ya kufuatilia mjadala huo kupitia majukwaa ya mtandaoni ya MCL kama vile Facebook na Youtube yatakayorusha matangazo ya moja kwa moja,” anasema Nanai.

Mkurugenzi mtendaji wa ITV, Joyce Mhavile anawakumbusha wananchi watakaokuwa nyumbani wakifuatilia jukwaa hilo kuwa watapata vitu adimu kutoka kwa wajuvi wa masuala ya biashara, uchumi na uwekezaji.

“Ni kipindi kitakachowashirikisha watazamaji watakaoweza kutoa maoni, uzoefu wao au kushauri cha kufanya. Ikumbukwe, viongozi wa Serikali na sekta binafsi watakuwepo wakifuatilia na kuchukua kila mchango unaotolewa. Watazamaji wa ITV na wasikilizaji wa Redio One wasikae mbali na runinga au redio zao,” anasema Mhavile.

Chanzo: mwananchi.co.tz