Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hasunga aeleza mpango Serikali ya Tanzania kununua ndege ya mizigo

43938 Koroshopic Hasunga aeleza mpango Serikali ya Tanzania kununua ndege ya mizigo

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya kununua ndege za abiria, Serikali ina mkakati wa kuwa na ndege ya mizigo itakayotumika kusafirisha nje mazao ya kilimo yanayoharibika kwa muda mfupi, hasa mbogamboga na matunda.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amesema hayo leo Februari 26, 2019 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano la kimataifa la kilimo biashara linalotarajiwa kufanyika Machi 20 hadi 22, 2019.

Kongamano hilo lina lengo ya kuwahamasisha vijana kushiriki katika  kilimo biashara kama njia ya kuunganisha uchumi wa viwanda na sekta ya kilimo.

Hasunga amesema hatua hiyo ni  jitihada za kuipa nguvu sekta ya kilimo na kuwawezesha wakulima kupata soko la uhakika wa mazao yao.

Amesema kwa sasa Serikali imeweka mkakati wa kutafuta masoko ndani na nje ya nchi na tayari Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda ameongoza jopo la wataalam kwenda kutafuta masoko nje ya nchi.

“Nchi yetu ambayo msingi wa uchumi wake kwa kiwango kikubwa unategemea kilimo ni muhimu kuwekeza kwenye kilimo kwa maana ya kuwa na mtaji, teknolojia na mambo mengine bila kusahau nguvu kazi ambayo ni vijana,” amesema Hasunga.

Waziri huyo amesema wakati umefika kwa vijana kuchangamkia fursa zilizopo kwenye kilimo na kujitengenezea ajira na kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao.

“Sehemu pekee ambayo ina ajira za wazi, uhitaji utembee na bahasha wala kufanyiwa usaili ni muhimu kwa vijana kuangalia kwa kina sekta hii na kujitengenezea ajira upande huo ambao unahitaji utaalam wa hali ya juu kama ilivyo sekta nyingine," amesema.

“Tunahitaji viuatilifu vya kwenye mazao, hivi tunaviagiza kutoka nje wakati hapa vijana wapo niwakumbushe kuwa hii ni fursa, anzisheni viwanda mtengeneze viuatilifu ili tuache kuagiza kutoka nje tununue hapa."

Kwa upande wake mwenyekiti wa kongamano hilo, Majabi Emmanuel amesema zaidi ya vijana 1,000 watakutana kujadili fursa zilizopo kwenye kilimo na namna ya kuzitumia kwenye biashara.

“Tunataka vijana washiriki kwenye kilimo biashara kuelekea kwenye uchumi wa viwanda na hasa kuwapa hamasa vijana kushiriki kwenye sekta hii, wahitimu wengi wa vyuo vikuu wanahangaika kupata ajira wakati kilimo kina fursa kubwa,” amesema.

Soma Zaidi: Serikali ya Tanzania yakaribisha wafanyabiashara kununua korosho



Chanzo: mwananchi.co.tz