Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Handeni kuwa ya mfano ufugaji wa kisasa

Cyriel Ulega na DC Handeni wakizungumza ofisini kwa Mkuu wa Wilaya

Tue, 12 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega amesema kuwa Serikali imeweka mipango mizuri ya kuhakikisha kijiji cha Msomera kilichopo Wilayani Handeni, Mkoani Tanga kinakuwa na miundombinu ya kisasa ya kuhudumia mifugo ikiwemo Majosho, Malambo na Nyanda za malisho ili wafugaji kutoka hifadhi ya Ngorongoro watakaohamia katika eneo hilo waweze kufuga kisasa na kwa tija.

Ulega aliyasema hayo alipofanya ziara katika Kijiji hicho cha Msomera ambapo kuna eneo limetengwa maalum kwa ajili ya wafugaji kutoka katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro kuhamia hapo kwa hiari yao ili kuendeleza shughuli zao za ufugaji.

Baada ya kukagua maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya Malisho, Majosho na Malambo, M Ulega alitoa maelekezo kwa Wataalam wanaosimamia uendelezaji wa maeneo hayo kuweka mikakati mizuri ya kukamilisha ujenzi wa miundombinu hiyo ili wafugaji hao kutoka ngorongoro watakapohamia eneo hilo wakute miundombinu ipo tayari na waweze kuendelea na shughuli zao.

“Tunataka wafugaji watakaokuja kufanya shughuli zao katika kijiji hiki cha msomera, wafanye shughuli zao za ufugaji kisasa, wafanye ufugaji wa kibiashara na tunataka hapa pawe ni shamba darasa ili hata mtu akitaka kujifunza ufugaji wa kisasa aletwe hapa”,alisema

Aliongeza kwa kusema kuwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa pesa kwa ajili ya kujengwa Majosho kumi (10) Wilayani humo ili mifugo iweze kuhudumiwa vizuri huku akisisitiza kuwa ufugaji huo wa kisasa utakaofanywa kijijini hapo utasaidia viwanda hapa nchini kupata malighafi bora na za uhakika.

Ulega aliwataka watendaji hao wanaosimamia uendelezaji wa maeneo hayo kuwa na mkakati wa pamoja ambao utaonesha utendaji wa shughuli zao kwa kila wiki na wawe wanaanda taarifa na kuzipeleka katika mamlaka husika.

Aidha, alitumia nafasi hiyo pia kuwahimiza wafugaji watakaohamia Wilayani hapo kuwa tayari kubadilika na kufanya ufugaji wa kisasa na kuachana na ufgaji wa mazoea ambao wamerithi kutoka kwa wazee wao kwani kwa sasa tija yake ni ndogo.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Siriel Mchembe alisema kuwa ujio wa Naibu Waziri Ulega Wilayani humo ni faraja kwao na anaamini utasaidia kutoa msukumo kwa Wataalam kuongeza nguvu katika utendaji hususan katika sekta ya mifugo.

Aliongeza kwa kusema kwa sasa kipato cha mwananchi wa kawaida wilayani humo ni kiasi cha shilingi laki nane na kumi kwa mwaka (810,000) lakini wamejiwekea malengo kuwa ifikapo mwaka 2025 kipato hicho kiongezeke kufikia shilingi Milioni moja (1000,000) kwa mwaka na hiyo itafanikiwa kupitia shughuli za ufugaji wa kisasa unaotegemewa kufanyika katika kijiji cha Msomera.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live