Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Halmashauri ya Temeke yatishia kufungia stendi binafsi

Stendi Binafsiiiii.png Halmashauri ya Temeke yatishia kufungia stendi binafsi

Wed, 17 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Mkoa wa Dar es Salaam ukitangaza maeneo hatarishi yanayoweza kukumbwa na Ugonjwa wa Kipindupindu, Halmashauri ya Wilaya ya Temeke imetishia kuzifungia stendi zinazomilikiwa na watu binafsi watakaoshindwa kuzifanyia ukarabati.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuwapo malalamiko kwa baadhi ya madereva na abiria wanaotumia stendi za Mbagala Rangitatu na Tandika kuhusu uchafu uliokithiri pamoja na miundombinu mibovu.

Mwananchi ilitembelea maeneo hayo jana Januari 17, 2024 na kujionea hali mbaya ya miundombinu ya stendi hizo pamoja uchafu.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Elihuruma Mabely amesema wameshatoa notisi kwa wamiliki wa stendi hizo kuhakikisha wanazifanyia usafi na kuziboresha kabla hawajazifunga.

Amesema hawezi kukubali halmashauri hiyo kuwa ya kwanza kutokea mlipuko wa kipindupindu kutokana na uzembe wa watu wachache.

"Hizi stendi zinamilikiwa na watu binafsi, tumeshazitembelea mara kwa mara na kuwapa maelekezo, lakini tumeshawapa notisi kwa ajili yakuzifanyia usafi pamoja na kuzikarabati vinginevyo tutazifunga," alisema Mabelya.

Alipoulizwa kuhusu halmashauri kuwa na stendi yao amesema tayari wameshatenga Sh2 bilioni kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa stendi kwa upande wa Mbagala Rangitatu.

"Kwenye Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (BRT) ipo stendi lakini kama mnavyojua ujenzi ule umegharimiwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, mchakato wake unahitaji kuhusisha mamlaka mbalimbali," amesema.

Alipotafutwa Mwenyekiti wa Madereva Kusini mwa Tanzania (Umakuta), Gulamal Kipengele amesema hawana mgogoro na Serikali kwa kuwa taratibu zote zinafuatwa.

Gulamali amesema stendi hiyo ni ya mtu hivyo wanasubiri Serikali itakapokamilisha ujenzi wa stendi yake iwahamishe kwa kuwa eneo hilo ni finyu.

"Ni kweli asubuhi na jioni magari yanajaa kutokana na ufinyu wa eneo hili ni eneo la mtu binafsi lakini kinachopatikana wanagawana na Serikali,"amesema Gulamali.

Pia, amesema kinachofanyika ni kutoa huduma kwa jamii wakati wakisuburi kufunguliwa kwa stendi mpya na kuiomba Serikali kuwasaidia kupaboresha kutokana na adha wanayoipata hasa wakati wa mvua.

Kwa upande wa watumiaji wa stendi hizo wakiwamo madereva, abiria na wafanyabiashara

wameeleza kero wanazokutana nazo ikiwa ni pamoja na mvua zinaponyesha maji husambaa eneo zima.

Jackson John mfanyabiashara katika Stendi ya Rangitatu ameiomba Serikali kuingilia kati akidai hali ni mbaya na kusababisha hofu ya mlipuko wa magonjwa.

Amesema mvua inaponyesha chemba za vyoo zimekuwa zikifurika na kusababisha maji machafu kusambaa kwenye eneo zima la stendi na kuingia kwenye maduka yanayozuka hiyo.

"Baada ya kusikia taarifa za mlipuko wa kipindupindu watu wamekuwa na hofu, wengine wanatamani hata kufunga biashara kutokana na hali ilivyo mbaya," amesema John.

Dereva wa daladala, Ahimidiwe Rogers amesema stendi hiyo ni finyu licha ya uchafu uliokothiri imekuwa ni chanzo cha foleni.

Amesema stendi hiyo inatumiwa na daladala na mabasi ya mkoani kitendo kinachofanya kuzidiwa.

"Kila siku tunasikia Serikali ina mpango wa kujenga stendi yake, hii ni ya mtu binafsi, tunatoa ushuru kila siku hatujui fedha inapokwenda," amesema Rogers.

Abiria ambaye hakutaka jina lake liandikwe amesema, stendi hiyo inatia aibu kwa kuwa haikustahili kuwepo kwenye Manispaa ya Temeke.

Tahadhari ya kipindupindu

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mohammed Mang'una ameanisha maeneo hatarishi zaidi yenye uwezekano wa kupata mlipuko wa Ugonjwa wa Kipindupindu.

Ameyataja maeneo ambayo yapo katika hatari zaidi ya kupata na mlipuko huo kuwa ni Halmashauri ya Jiji kwenye kata za Mnyamani, Kivule,Tabata, Mvuti, Kiwalani na Mchikichini.

Kwa upande wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni amezitaja kata za Mwananyamala,Tandale, Kigogo, Makumbusho, Hananasif, Msasani, Kunduchi, na Magomeni.

Katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ameyataja maeneo ya Azimio, Keko , Kibonde Maji, Tandika, Sandali, Yombo Vituka, Mianzini, Chalambe, Makangarawe, Mtoni, Mbagala na Buza.

Pia, kwa Manispaa ya Ubungo maeneo hatarishi ni Mburahati, Makurumla, Manzese, Ubungo, Mbezi, Goba na Makumbusho huku Halmshauri ya Manispaa ya Kigamboni maeneo yaliyotajwa ni Kigamboni, Kungwi, Vijibweni, Mji Mwema na Kibada.

Mganga mkuu huyo hakuishia kuyataja maeneo hayo tu, pia ameeleza hatua ambazo wamezichukua mpaka sasa ni kutenga kambi katika halmashauri zote, vituo viwili kwa ajili ya mawasiliano na maafa pamoja na kuongeza idadi ya maofisa afya katika kituo cha mabasi ya mikoani cha Magufuli.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live