Dar es Salaam. Wakati sikukuu ya Eid el Fitr ikikaribia kuadhimishwa, baadhi ya wafanyabiashara na wateja katika soko la Kariakoo na Buguruni jijini Dar es Salaam wamesema hakuna mabadiliko ya bei za bidhaa mbalimbali kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Wamesema bei ni ileile na kuna baadhi ya bidhaa kama nguo za watoto imepungua kidogo kiasi cha watu wengi kuweza kumudu.
Mwananchi imeshuhudia leo Jumatatu Juni 3, 2019 baadhi ya tisheti, suruali na magauni ya dukani ya watoto yakiuzwa kati ya Sh3,000 na Sh12,000 kulingana na umri wao.
Wateja na wafanyabiashara hao wamesema kutopanda kwa bei hiyo kumetokana na hali ya uchumi kwa sababu baadhi wanaamini wakipandisha watakosa wateja.
“Nauza nguo za watoto kwa bei ileile ya siku zote kuanzia Sh5,000 mpaka Sh15,000 kulingana na aina anayotaka mtu, siwezi kupandisha bei kwa sababu mavazi mtu akikosa hayawezi kumfanya asisherehekee sikukuu yake,” amesema mfanyabiashara Hussein Abdalah.
Mfanyabiashara ndogondogo wa nguo za wanawake Jumanne Idd amesema mwaka huu ameuza zaidi ikilinganisha na mwaka jana na kwamba, idadi ya wateja wanaohitaji nguo pia ni kubwa.
Pia Soma
- Zitto ataka Bunge kukagua deni la Taifa, ahoji ushuru wa machinga
- Taharuki mlipuko wa moto jengo la Tanesco
- Atiwa hatiani kwa mauaji ya mwanafunzi wa Scolastica
Kwa upande wao baadhi ya wateja wamesema hakuna kilichobadilika sokoni jambo linalowafanya wamudu kununua mahitaji yao kama siku zote.
“Nilikuwa na Sh50,000 nimeweza kuwanunulia watoto wanne nguo za sikukuu wakati kama wangepandisha bei pesa hiyo isingetosha,” amesema Mwantumu Athman.
Amesema japo chakula pia hakijapanda bei hofu yake ni kupanda kwa bei ya nyama kwa wale watakaonunua siku ya sikukuu kwa sababu mara nyingi, bei huwa inaongezwa.
“Niwaombe wanawake wenzangu wanunue chakula mapema ili siku ikifika wasije kuumia na bei, wafanyabiashara huwa wanatukomesha siku za sikukuu kupandisha bei,” amesema Mwantumu aliyekuwa akinunua bidhaa zake soko la Buguruni.
Mfanyabishara wa Nyama katika soko hilo John Kalembi amesema hawatapandisha bei ya nyama labda kuwe na upungufu wa mifugo hiyo jambo ambalo huwa linasababisha ng’ombe kupanda bei.
“Nauza kilo moja ya nyama Sh6,000 bei ambayo sitaweza kupandisha labda wauzaji ng’ombe kule mnadani wapandishe, siwezi kutumia sikukuu ambayo ni ibada kupata faida,” amesema.