Serikali ya Ghana inafanyia kazi sera mpya ya kununua mafuta kwa dhahabu, badala ya akiba ya Dola za Marekani ili kukabiliana na kupungua kwa akiba ya fedha za kigeni, kushuka thamani kwa fedha ya nchi hiyo na kudhibiti mfumuko wa bei ambao hadi Septemba ulifikia 37%. Utaratibu huo utaanza Januari 2023.
Makamu wa Rais wa Ghana Mahamudu Bawumia amesema hatua hiyo inalenga kukabiliana na kupungua kwa akiba ya fedha za kigeni pamoja na mahitaji ya dola kutoka kwa waagizaji wa mafuta, jambo ambalo linadhoofisha cedi ya ndani na kuongeza gharama za maisha.
Akiba ya jumla ya Kimataifa ya Ghana ilifikia $6.6bn mwishoni mwa Septemba 2022, sawa na chini ya miezi mitatu ya bima ya bidhaa kutoka nje. Hiyo ni chini kutoka $9.7bn mwishoni mwa mwaka jana.
Akifafanua zaidi Bawumia alisema "kimsingi itabadilisha malipo na kupunguza kwa kiasi kikubwa kushuka kwa thamani ya sarafu yetu.”
Alisema Kutumia dhahabu kunaweza kuzuia kiwango cha ubadilishaji kuathiri moja kwa moja bei ya mafuta au matumizi kwani wauzaji wa ndani hawatahitaji tena fedha za kigeni kuagiza bidhaa za mafuta kutoka nje.