Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gesi ya Tanzania kukutanisha kumpuni 60 za kimataifa

Wed, 19 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es salaam. Kongamano la kimataifa katika sekta ya mafuta na sesi litakalofanyika jijini Dar es salaam.

Katika kongamano hilo mada sita zinazolenga kuongeza ufanisi wa sekta hiyo katika shughuli za uchimbaji, uzalishaji, biashara na utoaji huduma kwa jamii zitatolewa.

Kongamano hilo litakalofanyika Septemba 24 na 25 litaunganisha wageni na kampuni 68 kutoka mataifa zaidi ya 30 ikiwamo Canada, Italia, Qatar, Oman na Uingereza.

Akizungumza na wanahabari leo, Makamu wa Rais wa Jumuiya ya Watoa Huduma katika sekta ya Gesi na Mafuta Tanzania (Atogs), Abdulsamad Abdulrahim alitaja mada hizo ni pamoja na kuithaminisha gesi ili kuendeleza viwanda na kukuza uchumi.

Mada nyingine ni kujadili nafasi ya ushiriki wa kampuni za ndani katika miradi, uchimbaji na uzalishaji wa gesi asilia, kutoa fursa na maendeleo ya miradi mikubwa ya gesi ikiwamo LNG na bomba la mafuta kutoka Uganda hadi bandari ya Tanga.

"Sekta ya mafuta na gesi ina nafasi kubwa katika uendelezaji wa viwanda, kuchochea uchumi pamoja na kufungua fursa kwa watoa huduma kwa hiyo tunatarajia matokeo makubwa katika kongamano hilo," alisema Abdulrahim.

Kongamano hilo litakuwa na wazungumzaji zaidi ya 60 wakiwamo mawaziri sita kutoka wizara ya nishati, viwanda, katiba na sheria, fedha na uchumi, mambo ya nje na waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu, ambao wataongozana na makatibu wakuu watano.

Pia, wataalamu wa gesi na mafuta, kampuni za kimataifa za uchimbaji, taasisi za utafiti na taasisi zinazowajibika kwenye sekta hiyo zitashiriki kwenye kongamano hilo litakalofanyika kwa mara ya pili nchini.

Kamishna Msaidizi wa maendeleo ya petroli kutoka wizara ya nishati, Joyce Kisamo alisema kiwango cha maendeleo katika Taifa lolote duniani kinapimwa kwa matumizi ya nishati.

"Kwa hiyo tunapoelekea uchumi wa viwanda, tunataka nishati kuu iwe gesi asilia, kwa hiyo kongamano hili ni fursa ya kujadili fursa za sekta kwa wananchi pia, masuala ya kisheria na kisera yatajadiliwa kwa upana, "alisema Joyce.

Kwa mujibu wa Shirika la Taifa la Maendeleo la Petroli (TPDC), gesi iliyogunduliwa hadi sasa ni futi za ujazo 57 trilioni zinazoweza kutumika kwa miaka 40 ijayo.

Aidha, kiwango kilichotumika hadi sasa ni chini ya trilioni moja ya futi za ujazo ambacho kinachangia zaidi ya asilimia 50 ya umeme unaozalishwa na kutumika nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz