Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Geita kuwa kitovu cha uchumi Afrika Mashariki

Rais Samia Kilele Cha Mwenve Samia suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania

Sun, 16 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imelenga kuufanya mkoa wa Geita kuwa kitovu cha uchumi ndani ya Taifa na ukanda wa Afrika Mashariki na kuwataka wananchi kutumia fursa hiyo hasa kwenye uwekezaji wa mwambao wa Ziwa Victoria ili kufanya mkoa huo kuwa lango la biashara.

Akizungumza na wananchi wa mkoa huo kwenye viwanja vya Kalangalala mjini Geita jana Jumamosi Oktoba 15, 2022, Rais Samia Hassan Suluhu amesema licha ya mkoa huo kuwa na fursa ya madini lakini Serikali inaona mkoa huo umekaa vizuri kwenye eneo la kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Tumieni fursa hii kwenye mwambao wa Ziwa Victoria ambalo ndilo ziwa kubwa kuliko yote Afrika, Geita sasa inaenda kuunganishwa na nchi nyingine tumeanza kujenga daraja kubwa la Kigongo Busisi hii itawaunganisha na nchi jirani na niwahakikishie kuwa daraja hili litakamilika mapema ili kuongeza chachu kwenye shughuli za kiuchumi katika mkoa huu”amesema Rais Samia

Mkuu huyo wa nchi amesema muunganiko wa mkoa wa Geta na mikoa mingine ya kanda ya Ziwa na nchi za Afrika Mashariki kupitia mtandao wa barabara na Ziwa Victoria itaimarisha Geita kuwa lango la biashara. Akizungumzia sekta ya madini Rais Samia amesema Serikali inatambua mchango wa wananchi wa mkoa wa Geita katika ujenzi wa uchumi hasa kwa kupitia uchimbaji wa dhahabu.

Ameiagiza Wizara ya Madini kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha shughuli za uchimbaji, uchenjuaji, utafiti na biashara unafanywa kwa kazingatia kanuni, sheria na miongozo inayosimamia sekta ya hiyo.

Amesema Wizara hiyo inafanya vizuri lakini inapaswa kuongeza bidii kwenye usimamizi na kutaka elimu ya sheria na kanuni za madini itolewe kwa wachimbaji huku akitaka Wizara hiyo kushirikiana na vyombo vya dola kudhibiti vitendo vya utoroshaji madini.

Waziri wa Madini Doto Biteko amesema mkoa wa Geita ni mkoa wa kwanza kwenye uzalishaji wa dhahabu hapa nchini na kusema asilimia 40 ya dhahabu inayozalishwa inatoka mkoani Geita.

Amesema wakati Rais Samia anaingia madarakani wizara hiyo ilikuwa ikikusanya Sh475 bilioni na sasa wanakusanya Sh 622bilioni kwa mwaka na mwaka huu wa fedha wamelenga kukusanya Sh800 bilioni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live