Mkoa wa Geita umetajwa kuwa kinara wa uzalishaji wa madini ya dhahabu yanayochimbwa kwenye maeneo mbalimbali katika mikoa ya kimadini nchini.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa mkoa Geita, Grace Kingalame ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Nyang'hwale, wakati akiahirisha semina kuhusu fursa za kijamii na kiuchumi zinazopatikana mkoani Geita wakati wa maonesho ya sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani humo.
Akizungumzia shughuli za madini zinazofanyika katika mkoa wa Geita Kingalame amesema, shughuli hizo zimegawanyika katika makundi manne ambayo ni Utafiti, Uchimbaji, Uchenjuaji na uuzaji.
Mkoa wa Geita kwa sasa una leseni mbalimbali zikiwemo kubwa mbili za uchimbaji, leseni za utafiti 127, leseni za uchimbaji mdogo 803, uchimbaji wa kati 8, leseni za biashara kubwa (Dealers) 47 na biashara ndogo (Brokers) leseni 33, leseni za uchakataji 33 na mitambo ya kuchenjulia madini leseni 265.
Takwimu za uzalishaji wa dhahabu kutoka Tume ya Madini mkoani Geita zinaonesha kuanzia mwaka 2017 mpaka 2023, kilo 111,585.56 za dhahabu zimezalishwa.
Mkoa wa Geita una migodi mikubwa miwili ambayo ni mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na Mgodi wa Buckreef .