Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gawio kila hisa NMB lapungua kwa Sh40

8844 Pic+gawio TZW

Tue, 12 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kutokana na kushuka kwa faida ya Benki ya NMB mwaka 2017, gawio kwa kila hisa limepungua kutoka Sh104 iliyotolewa mwaka 2016 mpaka Sh64.

Kupungua kwa faida hiyo kunakoathiri gawio la wanahisa kulitokana na changamoto nyingi ambazo benki hiyo ilikabiliana nazo mwaka jana.

Mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Ineke Bussemaker alisema matokeo hayo yamechangiwa na ugumu wa biashara waliopitia katika mwaka huo, kubwa zaidi likiwa ni ongezeko la mikopo chechefu. “Faida yetu imepungua lakini tumetengeneza theluthi moja ya faida nzima iliyotengenezwa na sekta nzima ya benki. Biashara yetu iliathiriwa na mikopo chechefu ambayo kwa ujumla katika sekta ilikuwa ni asilimia 12 sisi tukifikisha asilimia 6.4,” alisema Bussemaker.

Mkutano mkuu wa wanahisa wa benki hiyo uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, ulipitisha Sh32 bilioni kwa ajili ya gawio zilizopungua kutoka Sh52 bilioni zilizoidhinishwa kwenye mkutano wa mwaka 2016.

Hali hiyo inajidhihirisha kwenye hesabu za fedha za benki hiyo zinazoonyesha faida iliyopatikana imepungua kutoka Sh154 bilioni mwaka 2016 hadi Sh93 bilioni mwaka jana.

Bussemaker alisema mikopo iliyotolewa ilipungua kwa asilimia 0.3 lakini ilifanikiwa kuongeza amana kwa asilimia 14 na matawi mapya 23 bila kuajiri wafanyakazi wapya, hivyo kupunguza gharama za uendeshaji kwa asilimia mbili. “Faida ya benki yetu imepungua kwa asilimia 39 lakini tunajipanga kuhakikisha tunaiongeza mwaka huu, mpaka sasa hesabu za robo ya kwanza ya mwaka zinatia matumaini. Kwa robo hii moja kiwango cha mikopo kimeongezeka kwa asilimia 18,” alisema Bussemaker.

Naye mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa NMB, Profesa Joseph Semboja alisema benki ilijitahidi kupata faida kwani taasisi nyingi zilifanya uamuzi wa kupunguza biashara na wengine wakifunga maduka. “Ninaona fahari kwamba tuliweza kupambana na dhoruba iliyokuwapo,” alisema.

Wamliki wakubwa wa NMB ni Rabobank Group yenye asilimia 34.9 itakayopata gawio la Sh11.16 bilioni na Serikali inayomiliki asilimia 31.78, hivyo kustahili gawio la Sh10.16 bilioni.

Chanzo: mwananchi.co.tz