Wahandisi na mafundi sanifu zaidi ya 500 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa wanatarajiwa kukutana jijini Mwanza katika mkutano yao ya kujadili maendeleo ya fani yao itakayopambwa na maonyesho ya ubunufu yakiwemo magari ya umeme yaliyobuniwa na Watanzania.
Miongoni mwa Watanzania watakaoonyesha ubunifu wa magari yao katika mkutano huo utakaofanyika Mei 4 na 5, 2023 Rock city mall jijini humo ni Ali Masoud (Masoud Kipanya) aliyebuni gari la umeme.
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini (ERB), Bernad Kavishe amewataja wabunifu wa Kitanzania watakaoonyesha ubunifu wao wakati wa maonyesho yatakayofanyika viwanja vya Rock City jijini Mwanza kuanzia Mei 4, 2023 kuwa ni Ali Masoud maarufu kama Masoud Kipanya aliyebuni gari la umeme.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza jana Jumanne Mei 2, 2023, Kavishe amesema mkutano huo utatumika kujadili mchango wa mafundi sanifu katika utekelezaji wa mpango wa Taifa wa maendeleokwa miaka mitano ijayo.
“Masoud Kipanya ni mtundu ana mawazo mengi mazuri ambayo naamini atayatoa kwa Watanzania wenzake kila anapopata nafasi; sisi tutatoa nafasi kwake kuonyesha na kuzungumza na Watanzania kuhusu gari lake alilobuni,” amesema Kavishe
Ametaja mambo mengine yatakayoambatana na mkutano huo unaotarajiwa kufunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Balozi Aisha Amour kuwa ni viapo kwa wahandisi ambao hawajaapishwa.
“Bodi ya Usajili wa Wahandisi ina utaratibu wa kuwakutanisha mafundi sanifu kuwapa fursa ya kujadiliana, kushauriana na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazohusu fani zao; hawa ndio askari wa mstari mbele katika tasnia ya uhandisi,” amesema
Akizungumzia usajili, Kavishe amewaonya wahandisi na waajiri wao kuacha kufanya kazi zinazohusu tasnia hiyo bila usajili na leseni huku akifichua kuwa ERB inaweza kufikia uamuzi wa kuchapisha majina ya wahandisi waliosajiliwa ambao ndio wataruhusiwa kufanya kazi za uhandisi.
“Kwa sasa tunafanya ushawishi kuwahimiza wahandisi kujisajili na kupata leseni, lakini itafika wakati tutaanza kutoa mkeka wa majina ya wahandisi waliosajiliwa ambao wanaruhusiwa kufanya kazi za uhandisi,” amesema Kavishe