Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kufanya tafiti za madini katika wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro na wilaya ya Mufindi mkoani Njombe kwa lengo la kubaini aina ya madini yaliyopo katika wilaya hizo.
Dkt. Kiruswa ametoa agizo hilo wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Jimbo la Kilombero Abubakari Asenga katika kipindi cha maswali na majibu Bungeni jijini Dodoma Septemba 20, 2022.
Akijibu swali hilo amesema, Taasisi ya GST imefanya utafiti wa awali sambamba na kuchora ramani kwenye maeneo yote yaliyopo katika Jimbo la Kilombero katika mfumo wa Quarter Degree Sheet (QDS).
Aidha, Dkt. Kiruswa ameainisha maeneo mbalimbali yenye madini ya dhahabu na vito katika wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro ambapo tafiti za awali zilizofanyika katika wilaya hiyo zilionesha uwepo wa madini ya dhahabu na madini ya vito katika Kata ya Chisano.
Ameongeza kuwa, GST ilifanya utafiti wa awali na kuchora ramani ya eneo la Hifadhi ya Milima Udzungwa na maeneo jirani ambapo utafiti wa madini uliofanyika katika maeneo hayo hauoneshi taarifa zozote za uwepo wa madini ya thamani katika milima hiyo.
Mkoa wa Morogoro umebarikiwa kuwa na aina mbalimbali za madini ikiwemo dhahabu, Shaba, Kinywe, madini ya viwandani (Ulanga, Kaoline), madini ya ujenzi (mchanga, kifusi) na madini ya vito ( Rubi, Rodolite).