NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi ameipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kutoa fursa za ajira kwa Watanzania zaidi ya asilimia 90 ndani ya mgodi huo pamoja na kuwapatia wazawa fursa za kutoa huduma za kuuza bidhaa za ndani kwenye kampuni hiyo.
Amepongeza pia kampuni hiyo kwa kuibuka mshindi wa ubunifu na banda bora kwenye maonesho ya afya na usalama mahali pa kazi yaliyofanyika katika Viwanja vya Tumbaku mkoani Morogoro kuanzia Aprili 26 hadi 30, mwaka huu.
Katambi alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la kampuni kwenye maonesho hayo yaliyoratibiwa na Wakala wa Afya na Usalama mahali pa kazi (OSHA).
“Niwapongeze hasa kwa kupunguza ulemavu kazini, magonjwa yanayotokana na kazi, lakini pia kuhakikisha kwamba mazingira yote ya kufanyia kazi yanakuwa salama,” alisema.
Alisema: “Nafurahi kuona kwamba banda zima na hata ndani ya kampuni asilimia kubwa ya wafanyakazi ni Watanzania wenzetu kwa maana hiyo tunazidi kusisitiza kwamba kwenye maeneo yote ya kazi Watanzania ni kipaumbele.”
Alisema GGML imekuwa mfano wa kuigwa katika ununuzi unaofanyika kwenye migodi yake kwa sababu serikali kupitia mpango wa ‘local content’ inasisitiza kama vitu vipo nchini, vinunuliwe kuongeza ukwasi ndani ya nchi ili fedha nyingi isitoke nje.
“Lakini pia mmezingatia usalama wa mazingira kwa ujumla ili tusipate watu wenye ulemavu unaotokana na migodi hata pia mazingira na ardhi yetu inabaki kuwa salama. Kwa hiyo ninyi Watanzania mliopo huko ni wawakilishi wa kuhakikisha usalama unakuwepo…wa kwetu sisi, viumbe hai,” alisema.
Aidha, akimkaribisha katika banda hilo, meneja anayehusika na usalama kazini kutoka GGML, Isack Senya alisema zaidi ya wananchi 3,000 wametembelea banda hilo na kujifunza mambo mbalimbali kuhusu teknolojia zinazotumika kufanya kazi katika mazingira yenye afya na usalama.
Alisema mwaka huu, GGML ilileta vifaa vya kiteknolojia na kisasa kiasi cha kuiwezesha kampuni hiyo kuibuka kampuni bora yenye ubunifu kwenye vifaa hivyo.
Pia alimuahidi Naibu Waziri kuendelea kutekeleza miradi inayosaidia jamii kuondokana na umaskini pamoja na kupata huduma bora kwa kushirikiana na serikali.
Pamoja na mambo mengine, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na watu wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako alipita katika banda hilo na kuipongeza kampuni hiyo kwa kuwa mdau muhimu katika kuzingatia matakwa ya sheria yanayosisitiza afya na usalama mahali pa kazi.