WAKULIMA nchini Tanzania wameshauriwa kulima viazi vitamu vya njano kwa kuwa vina vitamin A kwa wingi, lengo likiwa ni kuwasaidia watoto, wajawazito na wamama wanaonyonyesha.
Meneja kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Kibaha Dk Nesia Luambano amesema hayo alipozungumza na HabariLeo katika maonesho ya mazao yaliyofanyika katika viwanja vya Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Kilimo cha Kitropiki (IITA), ikiwa ni sehemu ya program ya kongamano kubwa la chakula linaloendelea mkoani Dar es Salaam.
Dk Luambano amesema jukumu mojawapo katika kituo chao ni kufanya utafiti wa mazao ya mizizi yakiwemo mihogo na viazi vitamu.
“Kwenye viazi vitamu tunashughulika na uzalishaji wa mbegu bora za viazi vitamu aina zile bora lakini mbegu safi ili ziende kwa wakulima. Na sasa hivi katika aina tunajitahidi kuzifanyia kazi ni hizi zinaitwa viazi vya njano,” amesema.
Amesema wanafanya utafiti ili kuwezesha mbegu hizo kufika maeneo mengi hapa nchini kwa kuwa bado hazijawafikia wakulima wote.
“Mbegu hizi za viazi vya njano kadiri muda unavyoenda zinaendelea kukubalika. Watoto wanazipenda kwa sababu zina rangi nzuri kama kiini cha yai,” amesema na kuongeza kuwa mbegu hizo zinapatikana katika Kanda ya Ziwa, Kanda ya Mashariki na Pwani.
Amesema kama watafiti wanaendelea kuwahamasisha wakulima kuendelea kuzalisha aina za mbegu hizo za viazi vya njano kwa kuwa hivi sasa zinatumiwa pia na waokaji wa mikate na bidhaa nyingine.
Amesema taasisi hiyo imekuwepo kwenye maonesho hayo kwa kuwa wanafanya kazi kwa ukaribu na IITA hususani kwenye zao la mihogo lakini pia na viazi hivyo lishe.
Kwa upande wake Mkulima na mzalishaji wa mbegu bora za viazi vitamu vikiwemo viazi lishe hivyo, Daniel Lupanga amesema mkoa huo unazalisha kwa wingi viazi vitamu.
Lupanga ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Uzalishaji mbegu bora za viazi vitamu mkoani Geita amesema shughuli zao nyingi ni kuhakikisha wakulima wa Mwanza, Shinyanga na Simiyu wanapata mbegu bora za viazi vitamu.
“Kama chama sisi ni kiunganishi kati ya utafiti TARI ambao wamepewa kazi ya kutafiti mbegu kwa ajili ya uzalishaji lakini hawana uwezo wa kuzalisha mbegu za kutosha nchi nzima,
“Kama wazalisha mbegu kazi yetu ni kuhakikisha tunachukua mbegu mama zilizozalishwa na TARI, tunazalisha mbegu nyingi ili ziwafikie wakulima kwa urahisi katika maeneo tunayofanyia uzalishaji,” amesema.