Mwekezaji wa Klabu ya Simba, Mohammed Dewji 'MO' Dewji amepanda kwa nafasi mbili katika orodha ya watu matajiri zaidi Afrika kwa mujibu wa jarida la Forbes akishika nafasi ya 13 kwa sasa huku akiongoza chati hiyo kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Katika ripoti ya utafiti iliyotolewa na Forbes jana, aliyekuwa nafasi ya 15 hapo awali, amepanda kwa nafasi mbili kutokana na utajiri wake unaokadiriwa kufikia Dola 1.5 bilioni (Sh 3.5 Trilioni).
Bilionea wa Nigeria aliyefanya uwekezaji wa uzalishaji saluji hapa nchini, Aliko Dangote anaongoza orodha hiyo ya watu matajiri zaidi Afrika akiwa na utajiri wa Dola 13.5 bilioni akifuatiwa na Johann Rupertwa Afrika Kusini mwenye utajiri wa Dola 10.7 bilioni.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf), Dr. Patrice Motsepe ambaye anamiliki klabu ya soka ya Mamelodi Sundowns, anashika nafasi ya tisa katika orodha hiyo akiwa na utajiri wa Dola 3.2 bilioni.
Ni orodha ambayo 10 bora yake imetwaliwa zaidi na mabilionea kutoka nchi za Nigeria, Afrika Kusini na Misri mtawalia.
Nafasi ya tatu katika orodha hiyo inashikiliwa na Nicky Oppenheimer (Afrika Kusini), nafasi ya nne yupo Abdulsamad Rabiu (Nigeria), nafasi ya tano kuna Nassef Sawiris (Afrika Kusini), akifuatiwa na Mike Adenuga (Nigeria),Issad Rebrab (Algeria), Naguib Sawiris (Misri), Motsepe (Afrika Kusini) na Mohamed Mansourwa misri.