Halmashauri ya Mji Tunduma, Wilaya ya Momba Mkoani Songwe imeamua kuigeuza kero ya mrundikano wa malori katika mji huo na kuwa fursa ya kiuchumi kwa kuanza kujenga hoteli na eneo la maegesho ili kupanua wigo wa vyanzo vya mapato ya ndani.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Philmon Magesa alipofanya mahojiano na waandishi wa habari, kuwa wameamua kutumia msongamano wa magari makubwa yaendayo nchi za kusini mwa Afrika kuwa fursa hiyo kubuni mradi wa kituo cha maegesho ambao magari hayo hulipia na kuwaingizia mapato ya ndani.
Amesema maegesho hayo ni bora zaidi kutokana na kuongeza ubunifu Kwa kuongeza huduma zingine za kijamii ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba ya kulala wageni na sehemu ya kupata chakula, lengo likiwa ni kuhakikisha madereva hawapati usumbufu wowote wawapo katika mji huo, ikiwa ni pamoja na kuzungusha fedha ndani ya halmashauri na hatimaye pato hilo kuboresha miradi mingine ya maendeleo.
"Katika mradi wa maegesho halmashauri imekusanya zaidi Sh80 milioni mwaka wa fedha 2023/24 na tunatarajia mapato kuongezeka mradi wa hotel ukikamilika," amesema Magesa.
“Mji wetu wa Tunduma unakabiliwa na msongamano mkubwa wa magari hasa magari makubwa ya mizigo ambayo yanasafirisha mizigo kuingia na kutoka nchi za Kusini mwa Bara la Afrika (SADC) kutokana kuwa Tunduma ni lango kuu la kuingia katika nchi hizo," amesema Magesa.
"Tumetumia msongamano kama fursa ya kutuongezea ukusanyaji wa mapato. Tumebuni mradi wa kituo cha maegesho ya magari ili madereva wanapokumbana na msongamano huo waegeshe magari yao sehemu nzuri. Pia maegesho hayo yapo ya watu binafsi lakini sisi kama halmashauri pia tuna maegesho yetu, inayotusaidia kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri,’’ amesema Magesa.
Aidha amesema katika mwaka wa fedha uliopita halmashauri ilikusanya zaidi ya Sh60 milioni kutokana na maegesho hayo lakini mpaka mwaka wa fedha unaisha halmashauri ikawa imefanikiwa kukusanya zaidi ya Sh70 milioni kwa chanzo hicho kimoja, hivyo kudai kuwa mwaka huu wanatarajia kupata zaidi ya Sh80 milioni kupitia chanzo hicho cha kimkakati.
Mmoja wa madereva wa gari la kubebea mizigo kwenda Zambia, Susanye Kinye amesema wanapenda kuegesha magari yao katika maegesho hayo kwa kuwa bei yake ni nafuu.
Pia wanapendezwa na huduma pamoja na huduma za kiafya kama maji vyoo na huduma nyingine kama huduma za malazi na chakula ambazo zimekuwa zikitolewa hapo hapo katika eneo la maegesho.
"Ulinzi na usalama wa gari zetu pamoja na mizigo ni wa uhakika tofauti na nchi za kusini wanazokwenda ambapo huwa inatulazimu kulala ndani ya gari ili tusiibiwe mizigo na baadhi ya vifaa mbalimbali vya magari,” amesema Kinye.
Mfanyakazi katika maegesho hayo, Hakimu Fredy amesema kutokana na ubora na huduma nzuri zinazopatikana katika maegesho hayo, imesababisha kujaa mapema hivyo kushindwa kukidhi uhitaji wa wateja, kwa sababu wengi hukosa nafasi na kwenda sehemu nyingine.
Mkazi wa Chapwa yalipo maegesho hayo, Mariam Shantiwa amesema yeye pamoja na wenzake walianzisha biashara ndogondogo kando ya maegesho hayo na sasa wanajipatia kipato cha kuendesha maisha yao.
"Tunafanya huduma mbalimbali wapo ambao wameanzisha maduka madogo karibu na eneo hilo, wengine wanatoa huduma ya kufua nguo na wengine wanauza vyakula na kufanya wajipatie kipato cha kujikimu," amesema Mariam.