Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Foleni barabarani zinavyowapa ahueni wafanyakazi mijini

44337 Pic+foleni Foleni barabarani zinavyowapa ahueni wafanyakazi mijini

Fri, 1 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Amini, usiamini lakini ndivyo ilivyo: kila baada ya miaka mitatu Tanzania hupoteza Sh1.2 bilioni kutokana na foleni za magari barabara.

Na kiwango kikubwa kati ya fedha hizo kinapotea jijini Dar es Salaam.

Kama hiyo haitoshi, kila katika siku 10 za kazi, siku tatu hupotea bure bila kuwa na uzalishaji wowote kutokana na wafanyakazi wengi kutumia muda mwingi kwenye foleni.

“Utafiti unaonyesha watu wanatumia saa mbili wakiwa kwenye foleni barabarani. Na kwa maana hiyo katika kila siku 10 za mfanyakazi kazini, tatu zinapotea hivi hivi kutokana na foleni,” alisema Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Damas Ndumbaro wakati wa utiaji saini wa mradi wa upanuzi wa barabara ya New Bagamoyo kutoka Morocco hadi Mwenge jijini Dar es Salaam.

“Mwishowe mfanyakazi anakuwa kazini kwa siku saba tu.”

Alikuwa akitoa neno la shukrani kwenye hafla hiyo iliyofanyika jana katika jengo la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (PTA).

Dk Ndumbaro alisema kwa sasa wanafanya jitihada za kukaribisha wabia na wahisani kushiriki katika kuboresha sekta ya usafirishaji na miundombinu.

Alisema mbali ya hasara za kiuchumi zinazotokana na foleni za magari barabarani, kuna uchafuzi wa mazingira unaotokana na hewa ya ukaa inayotoka kwenye magari hayo.

Upanuzi wa barabara hiyo ambayo itakuwa ya njia nne kutokana na makubaliano ya Serikali na Shirika la Maendeleo la Japan (Jica), utakamilika ndani ya miezi 24 na utahusisha pia barabara ya mabasi yaendayo kasi itakayoanzia makutano ya barabara ya Kawawa na New Bagamoyo na kuishia kituo cha Mwenge.

Kipande cha eneo la Morocco hadi Mwenge ndicho kilichokuwa kimebakia baada ya kukamilika kwa barabara ya Mbezi ambayo mkataba wake ulisainiwa mwaka 2008.

Kukamilika kwa kipande hicho kunatarajiwa kupunguza adha ya foleni na hata kurahisisha usafiri wa barabara ya Shekilango eneo la Sinza ambalo barabara yake iko mbioni kupanuliwa na kuwa njia nne.



Chanzo: mwananchi.co.tz