Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Flyover Tazara yabadili upepo wa daladala

18053 Pic+flayover TanzaniaWeb

Wed, 19 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kilio kipya kimeibuka kwa abiria wa daladala eneo la Tazara jijini Dar es Salaam baada ya madereva wa daladala za Mnazi mmoja - Gongo la Mboto kupitiliza vituo, wakitumia zaidi barabara ya juu na kuwaacha abiria waliopo vituo vya Tazara.

Hali hiyo ilijitokeza jana ikiwa ni siku nne baada ya kuanza kutumika kwa barabara hiyo (flyover), iliyopo makutano ya barabara za Nyerere na Mandela eneo la Tazara).

Kwa daladala zinazotokea Gongo la Mboto kwenda Mnazi Mmoja kupitia barabara ya chini, zinasimama katika vituo vyote kama ilivyo kawaida, lakini zinazopita barabara ya juu zimekuwa zikisimama kituo cha Karakana kabla ya kufikia barabara ya juu na kituo cha Mtava baada ya kuvuka barabara ya juu.

Hali hiyo inawafanya abiria kufuata daladala umbali wastani wa mita 500.

Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabarani wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Johansen Kahatano alisema tayari changamoto hiyo wameshaibaini na jana aliwaagiza maofisa wao kukutana na watalaamu wa Wakala wa Barabara (Tanroads).

“Changamoto hiyo tumeipata na tunaifanyia kazi, maofisa wamekwenda kuzungumza na Tanroads kuhusu design ya mradi, baada ya mazungumzo hayo tutapata majibu ni namna gani tunaweza kushughulikia changamoto hiyo,” alisema Kahatano.

Kilio cha abiria

Baadhi ya abiria waliozungumza na gazeti hili walisema kwa sasa wanatumia zaidi ya dakika 10 hadi 60 kabla ya kupata daladala za Gongo la Mboto -Mnazi mmoja zinazopitia barabara ya chini.

Aprili 16, 2016 Rais John Magufuli aliweka jiwe la msingi katika barabara hiyo huku Agosti 29, 2018 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akieleza ujenzi huo umekamilika kwa asilimia 98 na ufunguzi utafanyika Oktoba.

“Nimeshuhudia jana (juzi) na leo (jana), yaani ili upate kwa haraka daladala ya kuelekea Mnazi mmoja inakubidi kusubiri kituo cha mbele kiitwacho Mtava badala ya kituo cha Tazara kwa sababu (Tazara) kipo katikati ya flyover chini,” alisema Abdul Waisa

Alisema, “daladala wanapitiliza hadi vituo vya mbele na umbali wa kituo hadi kituo ni zaidi ya mita 200 kutembea. Kwa hiyo abiria wa kituo hiki tunateseka sana.”

Kwa upande wao, madereva wa daladala walikiri kukwepa barabara ya chini wakisema wanapokuwa wamejaza abiria kutoka katika vituo vikuu hupitiliza ili kuwahi.

“Tunalazimika kuwahi kufika ili tuwahi kurudi na kuchukua abiria wengine kutokana na kuwa magari yetu yanakuwa yamejaza abiria,” alisema mmoja wa madereva hao.

Chanzo: mwananchi.co.tz