Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fidia ya Sh75 bilioni zingefanya haya

Pesa Fedhaddd Fidia ya Sh75 bilioni zingefanya haya

Thu, 19 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Uamuzi wa Serikali kuifanyia marekebisho Sheria ya Madini ya mwaka 2010 yaliyofanyika mwaka 2017 na kanuni zake ni chanzo cha Serikali kulipa Sh75 bilioni kwa mwekezaji Winshear Gold iliyemfutia leseni.

Fedha hizo zingeweza kutumika kuboresha sekta kadhaa za maendeleo, lakini zimeishia mikononi mwa mwekezaji kutokana na uamuzi uliofanywa na Serikali miaka michache iliyopita.

Fedha hizo zimelipwa kwa kampuni ya Winshear Gold ikiwa ni stahiki ya kampuni hiyo baada ya kukamilika mazungumzo nje ya mahakama kati yake na Serikali.

Kampuni hiyo ilipinga uamuzi huo wa Serikali na kufungua kesi mwaka 2020 katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) nchini Marekani, ikiwakilishwa na kampuni ya uwakili ya Lalive.

Hata hivyo, pande hizo mbili ziliamua kumaliza kesi hiyo nje ya mahakama kwa Serikali kukubali kulipa kiasi hicho cha fedha ambacho kimethibitishwa na Mwanasheria Mkuu, Dk Eliezer Feleshi aliyekiri malipo hayo kufanyika.

Licha ya Serikali kulipa mamilioni ya fedha kwa kampuni ilizofuta leseni au kuvunja mikataba, marekebisho sheria ya madini ya mwaka 2017 ndiyo yaliyowezesha kuanzishwa kwa Wizara ya Madini, Tume ya Madini na kufutwa kwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini.

Ni kupitia marekebisho hayo, Serikali ilikuja na dhana ya kuhakikisha kunakuwa na usawa kwa pande mbili, kila moja kunufaika kwa usawa katika mikataba ya uchimbaji wa madini.

Nini kingeweza kufanyika

Kiasi cha fedha kilicholipwa kwa kampuni ya Winshear Gold ni kikubwa kuliko bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwa mwaka 2023/2024.

Akiwasilisha hotuba ya bajeti bungeni, Waziri wa wizara hiyo, Dk Dorothy Gwajima aliliomba Bunge kuidhinisha Sh74.2 bilioni kwa ajili ya matumizi ya wizara hiyo.

Kwa mujibu wa tovuti ya Ofisi ya Rais Tamisemi, ili kujenga kituo cha afya kimoja na kuweka vifaa muhimu, gharama za ujenzi ni Sh1.1 bilioni na Sh280 milioni kwa zahanati.

Kwa msingi huo, fedha zilizolipwa kwa kampuni hiyo zingeweza kujenga zahanati 267 na vituo vya afya 68.

Kwa upande wa magari ya kubebea wagonjwa, yangeweza kununuliwa 250, moja likigharimu Sh300 milioni na kila mkoa ungeweza kupatiwa magari tisa.

Bado kukiwa na upungufu wa madarasa na madawati nchini, kiasi hicho cha fedha kingeweza kujenga madarasa 3,750 kwa gharama ya Sh20 milioni kila moja au kununua madawati 2.5 milioni kwa gharama ya Sh30,000 kwa kila moja.

Kwa mujibu wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kipimo cha CT Scan kinauzwa Sh900 milioni, hivyo fedha hizo zinaweza kununua mashine 83.

Katika sekta ya maji, gharama za kuchimba kisima kifupi ni kati ya Sh1 milioni na Sh3 milioni kulingana na jiografia ya eneo husika, hivyo Sh75 bilioni zingeweza kuchimba visima 75,000 au 25,000.

Kama fedha hizo zingeelekezwa kwenye mikopo ya elimu ya juu, zingeweza kugharimia wanafunzi 18,750 wa mwaka wa kwanza kwa asilimia 100 kwa wastani wa Sh4 milioni kwa kila mmoja kwa ajili ya chakula, malazi na ada.

Iwapo zingeelekezwa katika pembejeo, zingeweza kununua mifuko ya mbegu za mahindi 6,250,000 kwa gharama ya Sh12,000 kwa kila mmoja.

Maoni ya wadau

Baadhi ya wanasiasa na mchumi wamepongeza hatua ya Serikali ya kusuluhisha mgogoro huo nje ya mahakama.

Ilivyo ni kwamba, Serikali imeokoa mabilioni ya fedha ambazo ingetakiwa kulipa iwapo kesi ingesikilizwa mpaka mwisho na ikashindwa.

Kampuni ya Winshear Gold ilikuwa imeomba kufidiwa takribani Sh250 bilioni na gharama za kesi zinazofikia Sh25 bilioni.

Mbali ya kuokoa fedha, hatua hiyo pia inaelezwa imepunguza muda wa usikilizwaji wa shauri hilo na kulinda taswira ya uwekezaji nchini.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora alisema Serikali ilichofanya ndiyo uchumi wa sasa unavyotaka.

Alisema zamani uchumi ulitafsiriwa kama namba, lakini kadiri siku zinavyokwenda uchumi ni utawala, uongozi na akili za watu.

“Sasa unakuta tumefanya kosa wakati wa kutengeneza sera, tunaamini ni bora kufanya makubaliano kuliko kwenda mahakamani ambako gharama ingekuwa kubwa zaidi,” alisema.

Janeth Rithe, Naibu katibu wa habari, uenezi na mahusiano na umma wa Chama cha ACT- Wazalendo, alisema Serikali ifanye mazungumzo na watu wote wenye kesi katika mahakama za kimataifa ili kumaliza migogoro nje ya mahakama.

Alisema Serikali iheshimu mikataba ya wawekezaji ili kuepuka hasara kubwa ambayo nchi inapata.

“Serikali iweke wazi mashtaka yote yaliyopo mahakama za kimataifa dhidi ya Tanzania na thamani yake ili kuweka uwazi na wananchi wajue gharama hii kubwa ya kutoheshimu mikataba ya kimataifa,” alisema Rithe.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, alisema Rais Samia Suluhu Hassan, anapaswa kuwachukulia hatua waliohusika na uzembe ulioisababishia Serikali kulipa fidia hiyo.

“Tunapelekwa mahakama za kimataifa na tunatakiwa kulipa fedha nyingi. Serikali ifanye ukokotoaji wa hasara zilizotokana na mikataba mibovu,” alisema Mnyika.

Taarifa ya kampuni

Kampuni ya Winshear iliweka wazi taarifa ya kumalizika mgogoro kati yake na Serikali baada ya kulipwa kiasi hicho cha fedha walichokubaliana.

Mkurugenzi Mtendaji wa Winshear, Richard Williams alisema hatua hiyo ni nzuri kwa pande zote.

"Ni wakati mzuri wa pande zote kuendelea na mambo yake na tunaitakia Tanzania mafanikio katika kuvutia uwekezaji mpya," alisema.

Katika taarifa hiyo, Williams alipongeza mawakili waliosimamia kesi hiyo.

Hii si kesi ya kwanza kwa Tanzania kushindwa na kujikuta ikitakiwa kulipa mabilioni ya fidia.

Julai mwaka huu, Serikali ilitakiwa kulipa fidia ya Sh260 bilioni kwa kampuni ya Indiana Resources, iliyoshinda kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID), baada ya kujiridhisha ukiukwaji wa mkataba wa uwekezaji katika mradi wa Nikel wa Ntaka Hill mwaka 2018.

Uamuzi kama huo pia ulitolewa na ICSID mwaka 2019 ukiiamuru Serikali kuilipa kampuni ya IPTL fidia ya Sh426 bilioni kwa ukiukwaji wa masharti ya mkataba.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live