Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fedha za HEET zaanza kuleta mabadiliko TIA

Pesa Fedhaddd Fedha za HEET zaanza kuleta mabadiliko TIA

Fri, 29 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), imeanza utekelezaji wa mradi wa mageuzi ya kiuchumi kwa vyuo vikuu nchini (HEET) kupitia Sh27.6 bilioni ilizotengewa, huku ikizindua kamati ya ushauri wa kitasnia katika utekelezaji wa mradi huo.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo leo Desemba 29, 2023, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa William Palangyo amesema baadhi ya mambo katika taasisi hiyo yameshafanyika ikiwemo ujenzi wa mabweni mawili katika kampasi ya Mwanza.

"Kupitia fedha za mradi huo tumesaini mkataba wa usimamizi na mshauri wa ujenzi wa mabweni mawili katika kampasi ya Mwanza na pia tumenunua vifaa vya Tehama (Teknolojia Habari na Mawasiliano) kwa ajili ya kufundishia," amesema Palangyo.

Amesema pia wamegharamia kazi za ushauri wa tathmini ya athari za mazingira za kijamii kwa ajili ya ujenzi wa jengo la taaluma katika kampasi ya Singida.

"Tumefanikiwa kugharamia mafunzo ya kujenga uwezo kwa viongozi wakuu sita wa taasisi nchini Eswatini na kupeleka watumishi 13 wa kitengo cha Tehama kwenye mafunzo ya usimamizi na usalama," amesema Profesa Palangyo.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Amina Shabani aliyemwakilisha Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, amesema taasisi za elimu ya juu duniani hususani katika nchi zinazoendelea, zinakabiliwa na changamoto ya miundombinu ya kusomea na kufundishia.

Kwa mujibu wa Amina, miundombinu hiyo ni pamoja ile ya kidigitali, uhaba wa wahadhiri wa ngazi mbalimbali pamoja na kuwa na mitaala isiyoendana na uhalisia wa soko la ajira.

"Kama Serikali tumeyaona haya, ndiyo maana Serikali ikaja na mradi huu ambao ni matokeo ya mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia," amesema.

Amina ameitaka kamati hiyo kutambua malengo na kazi zake, ili ibaini, kushauri na kupendekeza mahitaji na mwelekeo wa mahitaji ya tasnia.

"Kwa kufanya hivyo kamati itaendeleza malengo ya programu. Hatua hii itaisaidia taasisi kushughulikia mahitaji ya ajira na taaluma kwa ujumla," amesema.

Pia ameitaka TIA kutoa ushirikiano kwa kamati hiyo, ili kuhakikisha inatelekeza majukumu yake kikamilifu na hatimaye kufikia malengo yaliyokusudiwa.

"Taasisi itoe ushirikiano wa dhati kwa kamati ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Ushirikiano wa taasisi ni muhimu katika kutekeleza malengo yaliyokusudiwa," amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live