Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Februari mwezi wa ATCL kwenda kimataifa

38253 ATCL+PIC.png Februari mwezi wa ATCL kwenda kimataifa

Fri, 25 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Miongoni mwa maeneo ambayo Rais John Magufuli ameyapa kipaumbele ni kulifu-fua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ambalo wakati anaingia madarakani lilikuwa na ndege moja tu aina ya Bombardier Q300.

Ikiwa na ndege hiyo, ATCL ilikuwa inahudumia asilimia mbili tu ya wasafiri wa anga nchini. Hivi sasa, shirika hilo lina jumla ya ndege tisa lakini zilizo kwenye biashara ni sita. Zote hizo zimenu-nuliwa na Serikali ndani ya miaka mitatu iliyopita.

Ndege hizo sita zenye ukubwa tofauti, tatu ni Bomberdier Q400-8, kuna Airbus A220-300 mbili na Boeing 787-8 (Dreamliner) moja.

Ndege ambazo sasa hazifanyi biashara ni Bom-bardier Q300 ambayo sasa ipo katika matengene-zo, Fokker 28 na Fokker 50 ambazo awali zilikuwa zinatumiwa na Ofisi ya Rais kabla Dk Magufuli hajazitoa kwa Shirika hilo la Taifa.

Ndege nyingine mpya aina ya Bombardier Q400 na Boeing 787-8 zinatarajiwa kuwasili nchini mwa-ka huu.“ATCL sasa ni shirika lenye ndege za ukubwa na uwezo tofauti kukidhi mahitaji ya safari mbalim-bali za masafa marefu na mafupi huku zikiwa na uwezo wa kubeba abiria na mizigo kwa pamoja,” anasema Mkurugenzi wa ATCL Ladislaus Matindi.Licha ya safari za ndani, hivi sasa ATCL ina-fanya safari kutoka Dar es Salaam kwenda Comoro, Uganda na Burundi.

Kwa safari za ndani, ndege zake zinatoka Dar es Salaam kwenda Bukoba, Dodoma, Kigoma, Kilimanjaro, Mtwara, Mbeya, Mwanza, Songea, Tabora na Zanzibar.Kulingana na mpango biashara wa ATCL wa hadi mwaka 2023, shirika hilo litakuwa likifanya safari za kimataifa hivyo kulitangaza taifa nje ya mipaka kutokana na ndege zake kuonekana katika viwanja vya mataifa mengine.

Kwenda kimataifa ndiyo kiu ya Watanzania wengi sasa kwani tayari mabawa ya Kilimanjaro (The Wings of Kilimanjaro) yanakatiza anga la nchi hii kila mara lakini tangu kutolewa kwa ahadi ya kwenda kimataifa bado mpaka leo haijatimizwa kama ilivyosemwa.

Ukiachilia mbali safari ya Comoro ambayo imekuwapo kwa kipindi kirefu, safari ya kwanza ya kimataifa kutangazwa na shirika hilo ilikuwa ya kwenda Mumbai nchini India ambayo ilitarajiwa kuanza Septemba mwaka jana.

Bei iliyotangazwa na ATCL kama bei yao kwa safari za Mumbai ni Dola 286 za Kimarekani (zaidi ya Sh653,000) kwa safari moja na Dola 455 (Sh1 milioni) kwa safari ya kwenda na kurudi lakini shirika hilo halikusema lini litaanza safari ya kwanza badala yake lilikuwa linasogeza mbele mara kwa mara.

“Sisi tutakwenda kwa saa sita mpaka Mumbai, tutakuwa tunaenda ‘direct’ (moja kwa moja) ndiyo maana tutafika haraka. Mara ya mwisho Air India ndiyo ilikuwa inafanya safari lakini siku hizi haiji. Safari ya kwanza inatarajiwa Novemba (bila kutaja tarehe rasmi),” alisema Matindi wakati akizungumza na gazeti hili Septemba 24 mwaka jana.

Ukiachilia mbali safari ya Mumbai Shirika hilo pia lilitangaza kuwa Novemba mwaka jana lingeanza safari ya kwenda Guangzhou nchini China kupitia Bangkok nchini Thailand lakini haikuwa hivyo badala yake safari za Bujumbura, Burundi na Kampala zilizotangazwa baadaye zilianza kabla ya zilizotangazwa awali.

Aidha, baada ya kuwasili kwa Airbus A220-300 siku chache zilizopita, ATCL imetangaza kuanza safari za Harare, Zimbabwe na Lusaka, Zambia Februari 22 na tayari bei kwa safari hizo imetangazwa.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili Matindi amewahakikishia wasafiri watarajie kumuona Twiga akienda kimataifa kupoza kiu yao kuanzia Februari hivyo kuufanya kuwa mwezi ambao shirika hilo litazindua safari nyingi kuliko kipindi chochote baada ya kukamilisha utaratibu kwa asilimia zaidi ya 90.

Kama ATCL itafanya kama inavyoahidi, huenda ikazindua zaidi ya safari nne Februari kwani lilishabainisha lengo lake la kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Afrika Kusini kati ya Februari na Juni mwaka huu.

Matindi anasema licha ya kurudishiwa uanachama wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (IATA) Oktoba mwaka jana, kuna madai ya kisheria yalijitokeza lakini yamekamilishwa tayari.

“Tulirudishiwa uanachama tukajua tumemaliza lakini yalikuja madai mengine ambayo yalihitaji uchunguzi lakini sasa yamekamilika na sasa tunamaliza kuunganishwa na mifumo mikubwa ya uuzaji wa tiketi duniani kati ya mifumo mitano tayari tumeunganishwa na miwili bado mitatu,” anasema Matindi.

Anasema mpaka sasa wameungwa na mfumo wa Travelsky, Travel Port bado kuunganishwa na Amadeus, Sabre na Worldspan na nyingine zitafuata kulingana na mahitaji.

Anasema wakati ndege za masafa marefu zikinunuliwa, mchakato wa kuanza kutumia jukwaa la IATA ulikuwa unaonekana unakamilika mapema lakini kuna mambo yalijitokeza ndani ya shirikisho hilo na vibali vya nchini ndege inakotarajia kutua ambayo yamesababisha kutoanza kwa safari hizo mpaka sasa.

Matindi anasema utaratibu uliobaki utakamilika Februari na kabla ya kuisha kwa mwezi huo tayari tiketi za kwenda China na India zitakuwa zinauzwa na tarehe ya safari ya kwanza itakuwa imepangwa.

Uwezo wa ATCL

Dreamliner moja ya ATCL ina uwezo wa kubeba abiria 262 na kusafiri umbali wa kilomita 13,620 bila kusimamana na ndege mbili aina ya Airbus A220-300 kila moja inabeba abiria 132 ikiwa na uwezo wa kusafiri kilomita 5,920 bila kusimama.

Ndege tatu aina ya Bombardier Q400-8 kila moja ina uwezo wa kupakia abiria 76 na kutembea umbali wa kilomita 2,084 bila kusimama.



Chanzo: mwananchi.co.tz