Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Faida yaongezeka sekta ya benki

82441 Benki+pic Faida yaongezeka sekta ya benki

Fri, 1 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ufanisi wa benki tano za biashara kati ya nane kubwa nchini umeongezeka kwenye robo ya tatu mwaka huu baada ya kukuza faida na kupunguza kiasi cha mikopo isiyolipika.

Kwenye orodha ya benki zilizofanya vizuri kuna CRDB, NBC, Standard Chartered, Stanbic na Azania ambazo ufanisi wake umeimarika iilinganishwa na ilivyokuwa robo ya tatu mwaka jana.

Katika orodha hiyo pia kuna NMB, Exim na Diamond Trust ambazo kila moja inamiliki mali zenye thamani ya zaidi ya Sh1 trilioni.

Faida ya Benki ya CRDB ilipanda kwa asilimia 35.5 na kufika Sh31.06 bilioni kutoka Sh22.92 bilioni za kipindi kama hicho mwaka jana.

Mafanikio hayo yalitokana na ongezeko la mapato ya riba yaliokua kwa asilimia 8.7 na yale yatokanayo na mauzo ya fedha za kigeni yaliyoimarika kwa asilimia 25.

Benki hiyo iliingiza Sh8.53 bilioni kutokana na mauzo ya fedha za kigeni zikiwa zimeongezeka kutoka Sh6.78 bilioni ilizopata kwenye robo ya tatu mwaka jana. Mapato halisi ya riba kwa CRDB yalikuwa Sh131.88 bilioni yakipanda kutoka Sh121.28 bilioni mwaka 2018. Mapato haya yaliimarika wakati uwiano wa mikopo isiyolipika na jumla ya mikopo ghafi ukishuka kutoka asilimia 12.9 hadi asilimia 7.8.

Pamoja na ukweli huo, mali za benki hiyo zilipungua kidogo ikilinganishwa na robo iliyopita. Katika robo iliyoishia Juni, mali za CRDB zilikuwa na thamani ya Sh6.38 trilioni ambayo ilishuka hadi Sh6.2 trilioni ilipofika Septemba.

Akizungumzia kupungua kwa mali hizo, mkurugenzi mtendaji wa CRDB, Adbulmajid Nsekela alisema kumechangiwa na kushuka kwa akiba waliyonayo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), taasisi nyingine pamoja na kupungua kwa uwekezaji wao kwenye amana za Serikali.

“Kutunza fedha nyingi zaidi BoT sio jambo jema kwa taasisi ya fedha. Kwenye robo zilizopita, benki nyingi ziliwekeza kwenye amana za Serikali ukiwa ni mkakati wa kupunguza mikopo chechefu. Tunachokifanya sasa ni kutoa mikopo zaidi kwenye sekta zinazofanya vizuri ili kuongeza mzunguko wa fedha kwenye uchumi,” alisema Nsekela ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Wakurugenzi wa Benki Tanzania (TBA).

Ikiwa na uwiano wa asilimia 1.1 wa mikopo isiyolipika, thamani ya mali za Benki ya Standard Chartered ilipungua na kufika Sh1.56 trilioni kutoka Sh1.64 trilioni za robo ya Juni.

Hii ilitokana na kupungua kwa mikopo iliyotoa kwa benki nyingine ya Sh162 bilioni ingawa ilikuza faida yake kwa asilimia 550 na kufika Sh5.8 bilioni kutoka Sh893 milioni ilizopata Septemba 2018.

Benki ya NBC ilipata faida halisi ya Sh3.1 bilioni baada ya kupata hasara ya Sh5.56 bilioni mwaka uliopita. Katika kuimarisha ufanisi wake, benki hiyo ilifanikiwa kupunguza tengo la mikopo isiyolipika kutoka Sh11.53 bilioni iliyokuwapo kwenye robo ya pili hadi Sh1.27 bilioni Septemba huku uwiano wa mikopo chechefu ukishuka hadi asilimia 6.9 kutoka 7.2.

Faida ya Benki ya Stanbic iliongezeka kutoka Sh4.35 bilioni iliyopata Septemba 2018 hadi Sh6.02 bilioni mwaka huu.

Benki ya Azania ambayo imeingia kwenye orodha ya benki kubwa baada ya kuinunua Benki M mwaka huu, faida yake iliongezeka kwa asilimia 400 na kufika Sh4.4 bilioni.

Chanzo: mwananchi.co.tz