Serikali duniani zinapanga kuzalisha nishati chafu mara mbili zaidi ya kiwango zilichojiwekea cha kupunguza uzalishaji ifikapo 2030, ripoti mpya imeonyesha.
Kwenye Makubaliano ya Paris mwaka 2015 (Cop21) nchi ziliweka mikakati ya kupunguza matumizi ya nishati chafu ili kudhibiti ongezeko la joto chini ya 1.5 za ‘centigrade’.
Taarifa iliyochapishwa Novemba 8, 2023 kwenye tovuti ya Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP), ilibainisha kuwa ripoti mpya imeonyesha serikali zinapanga kuzalisha takribani asilimia 110 zaidi ya nishati chafu (makaa ya mawe, mafuta na gesi) tofauti za malengo yaliyowekwa.
Haya yanatokea licha ya mataifa hayo 151 kukubaliana kufikia uzalishaji sifuri wa hewa joto kwa kupunguza taratibu matumizi ya nishati hizo. Ripoti hiyo mpya iliongeza kuwa wakati nchi 17 kati ya 20 zilikuwa zimeahidi kufikia uzalishaji sifuri wa hewa joto na nyingi zikibainisha mipango ya kupunguza matumizi ya nishati safi, hakuna iliyojitolea kupunguza uzalishaji wa nishati chafu.
Zaidi, Mtandao wa Covering Climate now ulinukuu Gazeti la New York Times lililoripoti, “ikiwa makadirio ya sasa yatatokea mpaka mwaka 2030, Marekani itachimba mafuta na gesi zaidi kuliko wakati wowote katika historia yake. Urusi na Saudi Arabia zinapanga kufanya hivyo pia".
Mtandao huo ulitaja uwepo wa miradi 422 ya mafuta, gesi na makaa ya mawe inayofanya kazi na kuzalisha hewa joto kiwango kinachoondoa kabisa matumaini ya kuzuia ongezeko la joto chini ya nyuzijoto 1.5°C.
Biashara ya kaboni na maoni mgongano
Akizungumza na gazeti hili mdau wa uwekezaji na biashara za kimataifa, Kiiza Afrika alisema kinachowafanya wachafuzi waendelee kufanya hivyo ni biashara ya kaboni.
“Wanufaika wa masoko ya kaboni ni kampuni zinazotumia nishati chafu, kwa vile inaruhusu waendelee kufanya hivyo kama watanunua haki ya biashara sehemu nyingine na wengine ni madalali wa ambao hununua na kuuza kaboni” alisema.
Aliongeza kuwa biashara ya kaboni ni sawa kabisa na vibali vya kuruhusu uchafuzi na biashara iliyoundwa kunufaisha zaidi wazalishaji na nchi husika na si kwa manufaa ya mabdiliko ya tabianchi.
“Uhalisia ni kwamba unamruhusu mzalishaji aendelee kuzalisha (hewa joto) kwa kiasi anachotaka kwa sababu tu anaweza kulipia” alisema Afrika. Mshauri wa nishati mpito Afrika kutoka Shirika la Kufuatilia Usimamizi wa Rasilimali za Asili (NRGI), Silas Olang’ anasema biashara hiyo ina pande mbili zikiwamo fursa kwa wanaouza na kikwazo kwenye kufikia malengo ya muda mrefu ya dunia bila kaboni ifikapo 2050.
“Ni fursa kwa nchi kama zetu ambazo zina misitu na zinaweza kuuza kaboni kwa hao wengine. Kwa vyovyote vile uzalishaji wa kaboni utaendelea na hata itakapofika mwaka 2050 hivyo ni fursa ambayo tunatakiwa kuitumia” anasema.
Olang’ anasema hata tukikataa biashara hiyo haimaanishi uzalishaji wa kaboni utaisha mapema. “Wataendelea tu, kwani wazalishaji hewa chafu wanafahamu kuna mahali wanaweza kufidia, hivyo wataongeza uzalishaji,”anasema.
Mtaalamu wa mazingira kutoka Wizara ya Muungano na Mazingira nchini, Dk Kanizio Manyika anasema bishara hii ni fursa kwa Tanzania kwenye kuchangia kupunguza hewa joto, licha ya kuwa nchi za Afrika hazichangii kwa kiwango kikubwa kwenye uzalishaji huo.
“Mimi huwa natoa mfano wa kupambana na mtu aliyechoma msitu na moto unakuja mpaka nyumbani kwako, sasa badala ya kushiriki kuuzima unakaa pembeni kwa sababu haujauwasha, lakini moto huo utaleta madhara kwa wote hivyo bora kuuzima kwa ushirikiano,” anasema Manyika.
Dk Manyika ambaye pia ni mwakilishi wa nchi kwenye Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) anasema, “Tanzania tuna miradi mingi ya kuhifadhi misitu na ilikuwepo muda mrefu.
Wadau watofautiana uwepo wa biashara ya kaboni
Olang’ anasema haoni biashara kama biashara hiyo ni endelevu, kwa sababu hivi sasa uzalishiji wa hewa chafu upo juu lakini kuna matarajio kuwa nchi zitapunguza uzalishaji na biashara itapungua. “Dunia inabadilika haraka na teknolojia inakua pia, kuna uwezekano wa nchi kugundua teknolojia itakayoweza kukamata au kuzuia kaboni, pia mikakati iliyopo nchi lazima zitapunguza ununuzi” anasema.
Dk Manyika alitofautiana na maoni hayo akisema biashara ni endelevu na ndio maana nchi ilitoa sera, miongozo, na kwa sasa sehemu nyingi duniani hata ukihitaji kukopa fedha wanahitaji kufahamu utachangia vipi kwenye kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mbadala wa biashara hii
Azizungumza katika majadala wa mtandaoni (media café) ulioandaliwa na Chombo cha habari za mazingira, sanyansi Afya na Kilimo (Mesha) na Ofisi ya Afrika ya IDRC Mashariki na Kusini mdau kutoka Taasisi isiyo ya serikali ya Power Shift Africa, Amos Wemanya alisema Afrika inahitaji mtiririko mbadala wa kifedha ili kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi na si kutengemea biashara hii.
“Nchi za afrika zinachangia chini ya asilimia nne ya uchafuzi hivyo hazina kiasi kikubwa cha kupunguza uzalishaji. Hili linalazimisha tufikirie njia sahihi za kuwekeza kwenye kukabiliana mambo haya” asliema
Wemanya alisema nchi zinahitaji kuwekeza kwenye nishati jadidifu na kuhakikisha mifumo ya kilimo inayokidhi mahitaji ya watu na sio wazalishaji wa kaboni.
Kutokana na mchango wake mdogo katika uchafuzi Afrika inapaswa kupokea ufadhili wa ruzuku kutoka
Uelekezaji upya wa ruzuku za mafuta na uwekezaji kuelekea nishati mbadala.
Miradi ya kaboni nchini
Miongoni mwa mradi wa kaboni nchini ni ule wa Milima ya Ntakata iliyopo Wilaya ya Tanganyika katika Mkoa wa Katavi ambao ulianza tangu 2016 kwa muhibu wa tovuti ya Kaboni Tanzania. Mradi huu unahusisha vijiji 12, na takriban watu 61,000. Eneo la mradi ni Hekta 110,527. Tangu mradi kuanza hadi sasa jumla ya Sh1.85 bilioni zimetolewa na inakadiriwa wastani wa miti 171,700 iliokolewa kukatwa.
Miradi mingine miwili ya Makame Savannah na mradi wa mazingira wa Yaeda – Eyasi ambayo ina thamani ya Sh836 billion na Sh1.63 bilioni mtawalia.