Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Faida iliyoingizwa na NMB baada ya kuongoza sekta ya Benki Tanzania

Bosi Afisa Mtendaji Mkuu wa Benk ya NMB Ruth Zaipuna

Mon, 2 Aug 2021 Chanzo: ippmedia.com

Benki ya National Microfinance Bank (NMB),imepata faida ya Shilingi za Kitanzania bilioni 134.

Hayo yamesemwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Ruth Zaipuna,alieeleza kuwa faida hiyo imetokana na ufanisi wa utendaji kazi uliochangia ongezeko la biashara na miamala, udhibiti wa gharama za uendeshaji na ubora wa mikopo inayotolewa.

“Mapato ya benki yameongezeka kwa asilimia 20 hadi kufikia Sh. bilioni 463 katika kipindi kilichomalizikia Juni mwaka huu, ikilinganishwa na Sh. bilioni 387 zilizopatikana katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Mapato haya yamechangiwa na ongezeko la mikopo kwa wateja na uwekezaji kwenye hati fungani za serikali,” alisema Zaipuna.

“Pia, mapato yasiyotokana na riba yameongezeka kwa asilimia 17 hadi kufikia Sh.bilioni 140 ikilinganishwa na Sh. bilioni 119 ya kipindi kama hicho mwaka jana. Ongezeko la mapato yasiyo ya riba yalichangiwa na ongezeko la miamala ya kibenki kutokana na huduma nzuri zinazotolewa na benki, mahusiano mazuri na wateja, na uwekezaji katika mifumo ya kidigitali.”

Bi Zaipuna Alisema katika kipindi hicho cha nusu ya kwanza ya mwaka huu, uwiano wa matumizi yasiyo ya riba na mapato halisi umeimarika mpaka kufikia asilimia 47 kutoka asilimia 56 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Alisema katika kipindi hicho, ubora wa mali za benki hiyo uliimarika kutokana na mikakati ya kuimarisha mikopo ya benki na kwamba uwiano wa mikopo chechefu uliimarika hadi asilimia 4.3 kutoka asilimia 6.9 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Zaipuna alisema mikopo ilikuwa kwa asilimia 11 hadi kufikia Sh. trilioni 4.2 kufikia mwisho wa Juni mwaka huu ukilinganisha na Sh. trilioni nne(4) katika kipindi kama hicho mwaka jana.

“Amana za wateja zilikuwa kwa asilimia nane(8) hadi kufikia Sh. trilioni 5.8 ikilinganishwa na Sh. trilioni 5.5 katika kipindi kama hiki mwaka jana, hii ikionyesha mazingira mazuri yaliyowekwa na benki katika uhusiano wake na wateja. Katika kipindi hiki mali za benki zimeongezeka kwa asilimia sita (6) hadi kufikia Sh. trilioni 7.6 ikilinganishwa na Sh. trilioni 7.2 katika kipindi kama hiki mwaka jana.

Akizungumzia mafanikio hayo yaliyopatikana, Zaipuna alisema, “Tunajivunia ufanisi bora na uimara wa benki yetu ya NMB. Mafanikio haya makubwa ya nusu ya mwaka 2021 ni kielelezo cha imani kubwa ya wananchi na wateja kwa benki yao ya NMB, ufanisi wa wafanyakazi wa benki ya NMB, utekelezaji bora na usimamizi mzuri wa mpango mkakati wa benki”.  

Aliongeza kusema kuwa, “Tunazidi kujikita katika misingi imara ambayo tumeshaijenga ikiwa ni pamoja na mizania bora ya benki, mtaji mkubwa, matawi mengi, uwezo mkubwa kidijitali, na wafanyakazi bora ili kuweza kusukuma mbele biashara yetu ya benki.

Tukitazama mbele tunahamasika tukiona  fursa mbalimbali zilizo mbele yetu kutokana na kuzidi kuimarika kwa uchumi wa dunia hasa baada ya madhara makubwa yaliyosababishwa na janga la COVID-19 pamoja na hatua stahiki zinazochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania kuimarisha sekta ya kibenki”.

Alisema; “Tutaendelea kuweka mkazo katika kuwahudumia wateja wetu kwa ufanisi na kutoa huduma bora ili kuhakikisha benki inaendelea  kuleta mafanikio kwa wawekezaji wake na pia kuwajibika katika jamii inayotuzunguka.

Chanzo: ippmedia.com