Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Faida, hasara mkataba wa kutotoza kodi mara mbili

Tra Kodi.jpeg Faida, hasara mkataba wa kutotoza kodi mara mbili

Fri, 14 Oct 2022 Chanzo: Mwananchi

Wiki kadhaa zilizopita Tanzania ilisaini Mkataba wa Kutotoza Kodi Mara Mbili (DTA) na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Kwa Tanzani mkataba huu ni wa 10, baada ya mingine tisa kusaniwa katika vipindi tofuti, huku UAE yenyewe ikiingia mkataba kama huo na nchi 139.

Miongoni mwa mikataba hiyo ni kati ya Tanzania na Afrika Kusini uliosainiwa mwaka 2005, Canada mwaka 1995, nchi za Scandinavia zinazojumuisha Denmark, Finland, Norway, Sweden (1976), India (1979), Italia (1973) na Zambia mwaka 1969.

Kwa mujibu wa utafiti wa “The Tax that We Want” uliofanywa na mtaalamu wa masuala ya kikodi, Dk Balozi Morwa, malengo makuu ya mikataba ya aina hii ni kuondoa utozaji kodi mara mbili (kisheria au kiuchumi) na kutoa ruzuku ya kodi itakayosaidia kuchochea uwekezaji.

Mbali na malengo hayo, mengine ni kutoa uhakika kwa mabadiliko ya mara kwa mara ya kodi (mkataba unaomlinda mwekezaji na sheria za kodi za ndani) na kutoa usaidizi wa kiutawala kati ya mamlaka za kodi (ukusanyaji wa kodi na taarifa).

Malengo mengine ya mkataba yanaendana na alichosema Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kwamba, kusainiwa kwa mkataba huo ni jitihada za kuondoa changamoto za biashara ili kukuza uhusiano wa kiuchumi, kuimarisha ushirikiano wa kodi na kuchochea mazingira wezeshi ya uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.

“Ni matumaini yetu baada ya mkataba huu tutaona uwekezaji mkubwa ukikua kati ya nchi zetu hizi, hasa kutoka Uarabuni ambako wana mitaji mikubwa, lakini utozaji kodi mara mbili ulikuwa unawakwaza,” alisema Dk Nchemba.

Faida nyingine za kikodi alizitaja Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo alipozungumza na gazeti hili, “ina lengo jema la kuvutia uwekezaji. Uwekezaji unapokuwepo ndio ajira zinatengenezwa na ndipo tunazidi kutanua wigo wa mapato.” Mtaalamu wa Masuala ya Kodi, Martin Chambai alisema nchi inaweza kuingia mkataba wa namna hii sio kwa faida za kikodi pekee.

“Zipo faida nyingine za kiuchumi, mwekezaji anaweza kujenga kiwanda akazalisha ajira na kuwawekea uhakika wafanyabiashara wengine wa malighafi kwa nchi husika,” anasema Chambai.

“Mfano ni Serikali ya Ireland, Jumuiya ya Ulaya (UE) na Kampuni ya Apple. EU waliitaka Ireland kuitoza kampuni hiyo kodi, lakini kutokana na faida za kiuchumi zilizotokana na kampuni hiyo hawakufanya hivyo." Je kuna upungufu?

Hata hivyo, licha ya faida lukuki zinazotegemewa, utafiti huu wa ‘The Tax that We Want’ unabainisha upungufu saba wa DTA (Mkataba wa Kutotoza Kodi Mara Mbili) ukieleza kuwa, mpaka sasa hakuna ushahidi wa kumbukumbu yoyote au utafiti kuhusu faida za mapato ya DTA dhidi ya hasara zake (upotevu wa kodi unaosababishwa na mkataba huo) nchini.

“Kwa hivyo, tunajihusisha na DTA bila kuelewa ikiwa ukuaji wa uchumi uliongezeka kama matokeo ya mkataba hii, mfano je, kukubali kuachia baadhi ya mapato ili unufaike wa uwekezaji kutafidiwa na faida za uwekezaji huo?” unaeleza utafiti huo.

Mkurugenzi mtendaji wa Policy Forum, Semkae Kionzo alikubaliana na lengo la mkataba, lakini alisema ili kupatikane matokeo chanya kwa nchi zote usawa wa kiuchumi ni muhimu.

“…ili matokeo chanya yapatikane kwa pande zote inapaswa angalau nchi zisitofautiane sana kiuchumi. Inapotokea hali ya nchi moja kiuchumi inapishana sana na ya nchi ya pili na kwa namna mifumo iliyopo inavyotumika, nchi yenye uchumi wa chini inapoteza zaidi ya kufaidi,” anasema Kionzo.

Anasema tafiti zilizofanyika, ukiwamo uchambuzi wa makubaliano haya uliofanywa na Policy Forum mwaka 2016 na mwaka 2018 zinaonyesha hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya utiaji saini wa makubaliano haya na uwekezaji nchini.

“Kwa maana nyingine hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa utiaji saini wa makubaliano haya unachochea biashara kati ya Tanzania na nchi mbia; ndiyo maana ukiangalia takwimu nchi nyingi zinazowekeza zaidi hapa nchini ni zile ambazo Serikali haina makubaliano nayo juu ya ulipaji kodi mara mbili.

“Tanzania haina rasilimali za kutosha kukabiliana na ukwepaji kodi unaohusisha uwekezaji usio wa nchi kavu, hivyo uwekezaji wa aina hiyo uleta hatari kubwa kwa ukusanyaji wa mapato,” unaeleza utafiti. “DTI zilizopo sasa kati ya Tanzania na Denmark, Norway, Sweden na Finland ni za muda mrefu, hivyo kushindwa kuendana na mabadiliko ya sheria za kodi yaliyofanywa hivi karibuni.” Pia, mikataba mingi inaonyesha kuwa ina viwango vya chini kwa Kodi ya Zuio (WHT) ambavyo ni chini ya sheria za ndani, hivyo kuwanufaisha zaidi wageni.

Ushauri kwa Serikali

Kwa kuzingatia sehemu kubwa ya matumizi ya umma yanaendana kwa elimu ya umma na huduma za afya, juhudi za ziada zitahitajika ili kupunguza ukwepaji wa kodi na uepukaji unaofanywa kupitia mikataba ya ushuru.

Utafiti huo unaeleza kuwa, “Serikali inahitaji kujadiliana au kuacha kazi kwa kufuta mikataba ya kodi ambayo hainufaishi Tanzania katika suala la upotevu wa mapato.”

Hata hivyo, Kionzo anashauri kabla ya Serikali kuendelea na utiaji saini wa mikataba mingine, ni vyema kufanya mapitio ya mikataba yote iliyopo kwa sasa na kubaini upungufu uliopo ili kuboresha na kufanya mapitio ya viwango vya kodi vinavyowekwa kwenye makubaliano ili kuona ni namna gani viwango hivi vinaisaidia nchi kupata au kupoteza mapato.

“Bunge linatakiwa kuhusishwa kimkakati kupitisha na kusimamia makubaliano haya, kuhakikisha uelewa wa kutosha juu ya makubaliano haya, hasa kwa wale wanaopitisha na kusimamia, na kuandaliwa na kutumika kwa mfumo utakaoziwezesha nchi zinazopokea mitaji kuweza kufaidi zaidi kwenye makubaliano haya,” anasema Kionzo.

Chanzo: Mwananchi