Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fahamu Mfumo wa Uagizaji Mafuta wa Pamoja ulivyoepusha bei kupaa zaidi

Mafuta Pamojaa.jpeg Matanki ya mafuta

Tue, 3 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Licha ya taifa kupitia changamoto ya ongezeko la bei ya mafuta  ya petrol na dizeli inayotokana na ongezeko la bei ya nishati hiyo kwenye soko la dunia, imebainishwa kwamba huenda changamoto hiyo ingekuwa kubwa zaidi iwapo taifa lisingekuwa linatumia mfumo wa uagizaji wa pamoja wa nishati hiyo.

Kwa mujibu wa  Kamishina wa Petroli na Gesi Wizara ya Nishati,Bw Michael Mjinja, uwepo wa mfumo wa uagizaji wa nishati ya mafuta kwa pamoja unaotekelezwa kupitia  Wakala wa ununuzi wa mafuta kwa pamoja (PBPA) umeliokoa taifa kutoingia kwenye changamoto ya ukosefu wa nishati hiyo kabisa kama ilivyotokea kwa baadhi ya mataifa jirani.

“Bei za mafuta bado zinapanda na huenda utulivu usiwepo hivi karibuni lakini jambo la uhakika hapa kwetu upatikaji ni wa uhakika, mafuta yaliyopo yanatosha na yataendelea kuwepo kadri ilivyopangwa. Uhakika huu tunaupata kwa kuwa mfumo tunaoutumia kuingiza nishati hii unatuwezesha kuwa na mipango thabiti sambamba na uhakiki wa taarifa zote muhimu kuhusu hali ilivyo’’ alinukuliwa Bw Mjinja wakati akihojiwa na moja kituo cha televisheni hapa nchini mwishoni mwa wiki..

Alisema kabla ya kuanzishwa kwa mfumo wa unununzi wa mafuta kwa pamoja, Tanzania nayo ilikuwa ikikumbana na changamoto za kukosekana kwa mafuta kwa kuwa mfumo uliokuwepo ulitoa fursa kwa wafanyabiashara kuagiza nishati mmoja mmoja kwa wakati anaoona unafaa kulingana na mahitaji yake.

“Gharama za kuleta mafuta zilikuwa juu sana, shehena ilikuwa inaletwa na meli ndogo ndogo hivyo zilikuwa zinajazana bandarini na zilikuwa zinatumia muda mwingi kushusha hadi siku 40 jambo ambalo lilikuwa halitoi uhakika wa upatikanaji wa nishati hiyo,” alisema Mjinja.

Alisema utaratibu huo ulikuwa hautoi uhakika wa utulivu wa bei kwani Serikali ilikuwa haina uwezo wa kufuatilia na kujua bei halisi ya mafuta na gharama za usafirishaji , lakini pia hakukuwa na uwezo wa kuhakikisha upatikanaji wa nishati hiyo unaenda sambamba na mahitaji.

Kwa mujibu wa Bw Mjinja, ni kutokana na sababu hiyo ndipo serikali iliona umuhimu wa kuanzisha utaratibu huo wa ununuzi wa pamoja ili kumlinda mwananchi na athari za bei isiyoendana na uhalisia pamoja na kulihakikishia taifa upatikanaji wa uhakika wa nishati hiyo muhimu.

“Kwa sasa kampuni za uuzaji wa mafuta ya jumla zipo 39 kila mmoja anawasilisha mahitaji yake kisha mafuta yanaagizwa kwa pamoja, miezi miwili kabla ili kuhakikisha hakuna upungufu.Hii inatusaidia serikali kujua mahitaji na kiasi tulichonacho” aliongeza Bw Mjinja.

Akihojiwa kupitia kipindi hicho hicho cha televisheni, Meneja wa Biashara ya Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura),Bi Kemilembe Kafanabo  alibainisha kuwa zabuni za kuingiza mafuta hayo nchini zimekuwa zikitangazwa kwa uwazi ili kuruhusu kampuni zote zote uwezo na vigezo vya kuingiza nishati hiyo kwa bei shindani aweze kushiriki.

“Kwa hiyo kama kuna muagizaji anajua namna anavyoiweza kupata nishati hii kwa bei nafuu zaidi fursa ndio hiyo kushiriki katika zabuni hizi. Kuna kampuni 23 ambazo ndizo hushiriki zabuni hizi na kwakuwa washiriki wa zabuni hizi ni wengi pia inakuwa sio rahisi kwao hata kupanga njama ya kibiashara ya kupandisha bei ya mafuta,” alisema Kafanabo.

Kwa mujibu wa Bi Kafanabo, pamoja na mambo mengine majukumu ya PBPA ni pamoja na kukusanya mahitaji na kuratibu uagizaji wa nishati hiyo kabla ya mahitahi hayo kupelekwa EWURA kwa ajili ya uhakiki ili kuona kama yanaendana na uhalisia kabla ya kuruhusu mchakato kuendelea.

Kauli hizo zinaungwa mkono na Mtaalamu wa uchumi na mtafiti mwandamizi Dk Hoseana Lunogelo aliesema mfumo wa ununuaji mafuta kwa pamoja una manufaa makubwa kwa walaji wa mwisho (wananchi) kuliko changamoto zake.

Kwa mujibu wa Dk Lunogelo utaratibu wa ugazaji wa mafuta kwa pamoja unapunguza gharama kwa kuwa anayepewa zabuni ya kuleta mafuta ni yule anayetoa gharama ya chini lakini pia gharama za meli zinakuwa chini kwa kuwa mzigo unaletwa kwa wingi kwa wakati mmoja huku pia kukiwa hakuna gharama ya usubirishaji wa meli.

“Siku zote gharama za usubirishaji wa meli zinabebwa na mnunuzi wa mwisho ambae ni mwananchi. Pia mambo yangekuwa tofauti kama mafuta yangekuwa yanaingizwa kwa mfumo huria kwa kuwa ingekuwa ni vigumu hata kuweka bei elekezi kwani kila mzigo ungekuwa na gharama zake kwa hiyo kila muagizaji angejipangia bei yake na kwa kipindi hiki ndio ingekuwa balaa zaidi,” alisema Dk Lunogelo.

Hata hivyo Dk Lunogela alibainisha changamoto nyingine iliyopo katika sekta ya mafuta hapa nchini ni usambazaji baada ya mzigo kufika bandarini kwa kuwa mfumo wa kutumia maroli unaongeza bei ya nishati hiyo, hivyo ameshauri iwepo haja ya kuendelea kutanua mtandao wa reli ili mafuta yasafirishwe kwa njia hiyo ili kuleta unafuu wa bei.

Dk Lunogelo alisema endepo mfumo huo wa uagizaji wa pamoja (BPS) usingekuwepo taifa lingepitia changamoto ukosefu wa uhakika katika usambazaji wa mafuta, bei kubwa, ukwepaji wa kodi, mlundikano wa meli, soko lisiloshindani pamoja na kukoma kwa matumizi ya bandari za Mtwara na Tanga katika uingiza wa mafuta.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live