Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

FURSA: Watanzania kuongeza ushindani wa biashara Afrika Mashariki

Palm U.png RC Mwanza akizindua kivuko cha Mv Palm kilichotengenezwa hapa nchini

Fri, 29 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Tanzania ikijinadi kukuza demokrasia na uchumi wa kimataifa, Watanzania wametakiwa kuchungulia fursa za kiuchumi kwenye nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kati ikiwa ni pamoja na kujizatiti katika uboreshaji wa huduma na bidhaa ili kuitangaza vyema nchi.

Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Azizi Mlimi akizungumza wakati wa hafla fupi ya kushusha kivuko cha Mv Palm cha Serikali ya Uganda ambacho kimejengwa na kampuni ya kizalendo ya Songoro Marine jijini Mwanza, amesema hiyo ni alama nzuri ya ushirikiano katika kukuza uchumi wa nchi zote mbili.

Balozi Mlimi ameitaka kampuni hiyo kutoishia nchini Uganda pakee katika kuchungulia fursa za ajira bali pia iangalie na nchi nyingine wanachama za Afrika Mashariki ambazo kuna maziwa ili kupanua wigo wa kibiashara.

“Kitendo kilichofanywa na kampuni ya Songoro ni alama nzuri, rai yangu isiishie nchini Uganda pakee bado kuna nchi nyingi ambazo zina maziwa wanaweza kuchungulia huko pia kuona fursa zingine za kibiashara,” amesema Balozi Mlimi.

Amewataka wawezekezaji wengine kuiga mfano wa kampuni ya Songoro ili kuweza kukuza uchumi wa nchi.

Kampuni hiyo imekuwa na mchango katika ujenzi wa vivuko na meli ambazo zimekuwa zikirahisisha huduma za usafiri wa majini hivyo kuchagisha biashara nchini. Awali akizungumzia ujenzi wa kivuko hicho, Mkurugenzi wa Songoro Marine, Meja Songoro amesema kivuko hicho ni cha kwanza kwa ukubwa nchini Uganda ambacho kina uwezo wa kubeba abiria 500, magari madogo 24 ya tani 2 na mengine makubwa manne yenye tani 34.

“Kivuko hiki kimejengwa kwa gharama ya Sh7.8 bilioni fedha za kitanzania, lakini pia kampuni imeendelea kupata tenda nyingine za kujenga vivuko na meli ndogo ikiwemo ya utafiti ambayo itajengwa kwa gharama ya Sh2.7 bilioni,” amesema Meja Songoro.

Amesema vivuko vingine vitano vinavyotarajiwa kujengwa na kampuni hiyo vya nchini Uganda vitagharimu zaidi ya Sh21 bilioni fedha za kitanzania.

Mkurugenzi huyo pia amesema mbali na miradi hiyo nchini Uganda, pia wameendelea kupata tenda ya ujenzi wa vivuko katika maeneo tofauti nchini Tanzania ambapo jumla ya miradi tisa yenye thamani ya zaidi ya Sh25 bilioni itajengwa na kukarabatiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amewataka wawekezaji na taasisi za kifedha kuwa na uthubutu pale kunapotokea fursa za kimataifa ili kuendeleza mashirikiano na kukuza uchumi

Chanzo: www.tanzaniaweb.live