Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

FAO yaainisha maeneo sita ya kuimarisha kilimo nchini

59862 Pic+fao

Mon, 27 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mzigo kwa mkulima nchini umeanza kupungua baada ya Serikali kuondoa tozo 105 ili kuongeza mchango wa sekta ya kilimo kwenye Pato la Taifa (GPD).

Kikiajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania, mchango wa kilimo kwenye GDP kwa sasa ni asilimia 28 lakini Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) linaamini kuwa bado kuna fursa za kuongeza mchango wa sekta hiyo.

Wadau wa maendeleo wanaamini kwamba kutokana na shughuli zilizopo kwenye kilimo nchini, bado sekta hiyo ina uwezo mkubwa wa kusaidia kukuza na kufikia uchumi wa kati ndani ya miaka sita iliyobaki ya kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.

Katika mjadala wa awamu ya nne wa Jukwaa la Fikra ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) uliofanyika Alhamisi iliyopita na kuwakutanisha wadau kujadili hali iliyopo, kuainisha changamoto na kupendekeza suluhisho katika kuendeleza sekta ya kilimo, mwakilishi wa FAO nchini, Fred Kafeero alisema Tanzania ina nafasi nzuri ya kufikia Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG), Dira ya ‘Afrika tunayoitaka’ hadi mwaka 2063, Azimio la Malabo na wito wa Afrika kutokomeza njaa ifikapo mwaka 2025.

Ili kufikia malengo hayo, Kafeero alibainisha maeneo sita yatakayosaidia kuimarisha kilimo nchini ikiwamo kuongeza utashi wa kisiasa na uwekezaji wa Serikali ili kuongeza uzalishaji na kupunguza utapiamlo nchini.

Jambo la pili ni kuongeza uwezo wa wakulima ili kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Pia Soma

“Tukiangalie kilimo kwa mapana na kwa njia jumuishi inayogusa sehemu zote za mnyororo wa thamani kuanzia uzalishaji, miundombinu ya utunzaji baada ya mavuno, uchakataji hadi kwenye meza ya mlaji, hatua hii itawasogeza wadau katika mchakato wa maendeleo ya kukuza sekta hiyo kwa manufaa ya uchumi wa Taifa,” anasema Kafeero.

Kafeero ametaja pia uwekezaji ili kuendeleza kilimo kwa mahitaji ya watu na ulinzi wa mazingira. Mbali na hatua hiyo, amesisitiza matumizi ya teknolojia na pembejeo za uhakika za uzalishaji na uchakataji wa mazao ya kilimo.

Jambo la sita anasema ni kuongeza mtaji katika sekta hiyo ili kuwawezesha wakulima wadogo hatua itakayowajengea uwezo wa kushindana katika masoko ya ndani na kimataifa kwa faida. Hali hiyo, anasema inahitaji uwazi ili kuvutia sekta binafsi.

Kafeero ametoa maoni hayo kwenye mjadala wa wiki iliyopita uliohusu ‘kilimo, maisha yetu’ ukifanyika takriban miezi 11 baada ya jukwaa la kwanza lililowakutanisha wadau Juni 28, 2018 likiwa na mada kuu ya ‘afya yetu, mtaji wetu.’

Awamu ya pili ya jukwaa hilo iliyofanyika Oktoba 4, 2018 lilijadili fursa na changamoto kuelekea uchumi wa viwanda na kufuatiwa na awamu ya tatu, Februari 7, 2019 likijadili ‘mkaa, uchumi na mazingira yetu.’

Akichangia hoja katika mjadala huo, mkurugenzi mtendaji wa Benki ya Maendeleo Kilimo Tanzania (TADB), Japhet Justine amesema taasisi za fedha zinapaswa kuongeza mikopo ya sekta ya kilimo kutoka asilimia nane za sasa hadi walau asilimia 25.

Kafeero ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa wadau wa sekta ya kilimo nchini ameahidi FAO kuendelea kuisaidia wizara kutafuta wawezeshaji wa mfumo wa uzalishaji chakula na kilimo na kuhamasisha kilimo sahihi.

Kwa mujibu wa Kafeero hatua hiyo inaenda sanjari na uimarishaji wa masoko ya kimataifa ikiwamo kukidhi viwango na ubora wa kimataifa kuhusu usalama na usafi.

Mwakilishi huyo wa FAO anasema hakuna nchi iliyoendelea bila kuwekeza katika rasilimaliwatu na kwamba Tanzania inahitaji kukuza uwezo, maarifa na ubunifu, kuboresha mazingira ya uwekezaji katika taasisi za elimu, mafunzo na utafiti. Hilo ni muhimu katika kuleta mapinduzi ya sekta ya kilimo na hiyo ni hatua muhimu hususan katika zama za mabadiliko ya tabianchi.

“FAO itaendelea kutoa msaada wa kitalaamu kwa Serikali kuendeleza na kutekeleza sera na programu tukiweka mkazo katika masuala ya usalama wa chakula na lishe. Tutahamasisha kilimo endelevu chenye tija kitakachokidhi mahitaji yanayoongezeka huku tukisisitiza umuhimu wa utunzaji wa rasilimali za asili,” amesema.

Katika kufanikisha hilo, amesema watafanya kazi kwa karibu na watafiti, wasomi na wataalamu wa huduma za ugani katika usambazaji wa teknolojia za kilimo himilivu ikiwamo kinachotilia maana ikolojia.

Hali mbaya SADC

Kuhusu uzalishaji wa chakula kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Kafeero anasema licha ya kilimo kuajiri watu wengi zaidi, kwa mataifa mengi ni nguzo ya kutomokeza njaa na umaskini.

Anasema nchi nyingi hasa za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ikiwamo Tanzania hazijatilia mkazo mchango wa sekta hiyo katika ukuzaji uchumi.

“Uwekezaji bado ni mdogo sana. Kilimo kilichopo kinahusisha wakulima wadogo wanaozalisha kwa ajili ya kujikimu. Kilimo kinategemea mvua hata mahali penye vyanzo vya mito na maziwa, mbegu zisizo na ubora unaotakiwa na matumizi madogo ya mbolea na zana duni, jembe la mkono linatumika zaidi hatua inayosababisha upotevu wa mazao mengi,” anasema.

Chanzo: mwananchi.co.tz